Wiki ya huduma za fedha: Nguzo muhimu ya kuwezesha uchumi wa watu

November 6, 2021 9:20 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wiki hii itasaidia wananchi kupata maarifa juu ya fursa za kupata huduma za fedha na mahali wanapoweza kuwekeza kwa weledi bila wasiwasi.

Katika wiki ya Novemba 8 hadi 14 mwaka huu, mamia ya watu wanatarajiwa kujumuika katika Wiki ya Huduma za Fedha kitaifa itakayofanyika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Jijini Dar es Salaam.

Wiki hiyo, yenye kauli mbiu “Boresha Maisha kupitia Elimu ya Fedha”, itashamiri taarifa na maarifa kutoka kwa wataalamu wa masuala ya fedha kuhusu fursa zilizopo na namna ya kukabiliana na changamoto kwenye sekta hiyo.

Wizara ya Fedha na Mipango, inayoongoza uratibu wa wiki hii, itashirikiana na wadau wengine wa sekta ya fedha kama wizara na idara za Serikali za Tanzania Bara na Zanzibar, taasisi za fedha, asasi za kiraia,  vyombo vya habari, vyama vya wafanyakazi, taasisi za utafiti na wadau wengine muhimu kwenye sekta hii.

Kwa nini wiki hii ni muhimu kiuchumi?

Moja ya wachumi mahiri mwishoni mwa karne ya 20 na aliyewahi kuwa mkuu ya Benki Kuu ya Marekani kati ya mwaka 1987 mpaka 2006, Allan Greenspan anabainisha kuwa “changamoto ya kwanza kwenye kizazi na uchumi wa leo ni ukosefu wa uelewa wa masuala ya fedha”.

Hakuna shaka kuwa Greenspan anaeleza tatizo kubwa ambalo linasiganisha ukuaji wa uchumi na maendelo ya watu. Kimsingi anajaribu kufafanua kwa lugha nyepesi nje ya uga wa uchumi hoja ya kwa nini maendeleo ya watu hayaakisiwi kwenye ukuaji mkubwa wa sekta ya fedha duniani?


Soma zaidi: 


Hoja hii ni bayana duniani kote, lakini ina uzito mkubwa kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania.

Utafiti wa S&P wa mwaka 2014 unabainisha kuwa uelewa mdogo wa masuala ya fedha kwenye nchi za Kusini unaathiri vibaya jitihada za kutokomeza umaskini na kwa Afrika. Kikwazo hiki kinachangia zaidi ya asilimia 56 ya kuzorota kwa jitihada za kuondosha umaskini.

Nchini Tanzania, wakati Malengo ya Milenia yananza mwaka 2000, maoteo ya kiuchumi yalionesha kuwa kama uchumi wetu ungekua kwa asilimia saba (7) mfululizo kwa miaka kumi na tano (15) basi umaskini ungepungua kwa kiwango cha zaidi ya mara tatu zaidi ya hali ilivyokuwa mwaka 2000.

Lakini mpaka mwaka 2015, maoteo hayo hayakuakisiwa kama ilivyotarajiwa. Uchumi uliendela kukua kwa kasi wakati kiwango cha umaskini kikiwa hakipungui kwa vipimo halisia (In economic real terms).

Wachumi, wanasiasa, wanahabari na wachambuzi wa mambo, kwa muda mrefu wemekuwa wakiiohoji Serikali juu ya mantiki ya kukua uchumi bila matokeo halisi kwa watu. Wamekwenda mbali na kuhoji kuwa Serikali inawekeza kwenye uchumi wa vitu na siyo wa watu.

Mjadala huu ulikuwa mkali sana kuelekea uchaguzi wa mwaka 2020 na hata sasa. Ukuaji wa uchumi usiojibu matakwa ya kupunguza umaskini una sababu kuu tatu.

a) Ukuaji wa sekta zisizo na mahusiano na watu wengi.

b). Ukuaji mkubwa kwenye faida za vyanzo vya uzalishaji (factors of production) kama mitaji, ardhi na nguvu kazi zaidi ya ukuaji halisi wa uchumi.

c) Uelewa mdogo wa wananchi kwenye uchumi juu ya sekta ya fedha.

Ili kukabiliana na changamoto ya tatu, Serikali imeamua kuwa na Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa Mwaka 2020/2021- 2029/30 ambao una Programu ya kutoa Elimu kwa Umma ya Mwaka 2021/22-2025/26. Wiki ya Huduma za Fedha inaangukia kwenye progamu hiyo ya elimu kwa umma.

Elimu ya fedha inakuza uchumi wa watu

Katika kukidhi mahitaji ya uchumi mpana na maisha ya watu, mpango huu unalenga kufikisha elimu kwa watu juu ya usimamizi wa fedha binafsi, uwekaji wa akiba, mikopo, uwekezaji, bima, bima ya amana, hatifungani na mengineyo.

Haya ni maeneo muhimu kwenye kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maisha ya watu. Ni kwa njia hii viwango vya watu kuelewa kuwa fedha ipo kwenye uchumi kwa ajili yao vinaweza kuongezeka badala ya dhana kuwa haya ni masuala ya watu pekee.

Baadhi ya wajasiriamali wadogo wa Manispaa ya Kigoma Ujiji wakishona mashuka kwa ajili ya kuyapeleka sokoni Julai 3, 2021.  Wafanyabiashara wadogo wanahitaji elimu zaidi ya kifedha ili kupata mitaji na kutumia vizuri mitaji yao. Picha|Nuzulack Dausen/Nukta. 

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba aliwaeleza wahariri wa vyombo vya habari kwenye semina juu ya masuala ya fedha na maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Kifedha kitaifa jijini Dodoma Novemba, mosi mwaka huu kuwa elimu kwa umma juu ya masuala ya fedha itaongeza uwekezaji kwa mtu mmoja mmoja kwa kuwa watu wengi watafahamu mahali watakapopata fedha na kwa jinsi gani wawekeze kwa weledi.

Hoja ya Tutuba inaungwa mkono na ushahidi wa tafiti za kiuchumi kwenye uwekezaji wa ndani. Kwa mujibu wa utafiti wa mtandao wa kimataifa wa elimu ya fedha (International Network on Financial Education) wa mwaka 2019 ikiwa nchi zinazoendelea zitawekeza kwenye elimu ya fedha kwa umma kwa zaidi ya mara tano ya kiwango cha sasa, uwekezaji wa ndani wa moja kwa moja yaani (Domestic Direct Investments) utaongezeka mara mbili zaidi . Ukuaji huo utasaidia wananchi wengi kushiriki kwenye uchumi unaokua.

Itaongeza ukuaji wa wajasiriamali wadogo, kati

Wiki ya Huduma za Fedha ina mchango mkubwa katika kuongeza kasi ya ukuaji wa wajasiriamali wa kati na wadogo (MSMEs) kwa kuwa maarifa ya kuweka akiba, kuwekeza, nidhamu ya fedha, masuala ya bima ni nguzo muhimu ya ujasiriamali.

Dk Charles Mwamwaja, Kamishna Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango anasema Wiki ya Huduma ya Fedha imelenga kuongeza fedha kwenye mzunguko rasmi na kuwezesha mifumo ya mtiririko wa fedha inayowafikia rasmi na kwa urahisi wajasiriamali.

Ni muhimu kufahamu kuwa kuwa na maarifa kuhusu elimu ya fedha ni jambo muhimu sana kwako kuliko kuwepo fedha kwenye uchumi ambayo huna taarifa jinsi ya kuipata na maarifa juu ya kuiwekeza na kupata faida.

Ili kunufaika zaidi na huduma za kifedha, ni muhimu ukatenga muda na kushiriki Wiki ya Huduma za Fedha ili kupata maarifa yatakayokupatia mwanga mpya.

Dk Bravious Kahozya ni Mchumi na mwandishi wa habari za biashara na uchumi. Wasiliana naye kupitia Twitter @BraviousKahyoza. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na wala si msimamo wa Nukta. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW