WFP, DLI wahimiza matumizi ya data kuboresha usalama wa chakula nchini
- Ukosefu wa data kikwazo kwa wakulima kunufaika kiuchumi
- Wabunifu kuzifikia Halmashauri zenye changamoto ya chakula
Dar es Salaam. Programu ya Chakula Duniani (WFP) kwa kushirikiana na taasisi ya Data for Local Impact (DLI) wameazimia kuwawezesha wakulima kutumia teknolojia na data kuongeza uzalishaji wa mazao na usalama wa chakula nchini.
Kwa mujibu wa WFP, wakulima hasa wanawake wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa masoko ya uhakika, mavuno hafifu, magonjwa ya mazao na mabadiliko ya hali ya hewa ambayo kwa kiasi kikubwa yanatokana matumizi ya teknolojia duni ya kilimo.
“Wakulima wanawake hawapati teknolojia baada ya mavuno, fedha, bima, taarifa, na pembejeo,” kinaeleza kitabu cha Changamoto za ubunifu cha WFP cha Julai 2018. “Huu ukosefu wa usawa unasababisha uzalishaji mdogo na kutishia usalama wa chakula.”
Uwezeshaji huo utafanyika kupitia dirisha la vijana wenye uwezo wa kutumia ubunifu, teknolojia na uchambuzi wa data ili kuwafikia wanawake nchini wenye changamoto za lishe na chakula zinazotishia ustawi wao na watoto.
“Hili dirisha la changamoto ya ubunifu ni la tano tangu DLI ianze, limejikita kutafuta suluhisho la kuhakikisha kizazi kijacho cha watanzania kinakuwa na afya njema inayotokana na kuwepo kwa chakula cha kutosha, salama na chenye virutubisho na kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo,” inasomeka sehemu ya kitabu cha WFP.
Mwaka 2015/2016, WFP na serikali walifanya mapitio ya Mkakati wa kutokomeza Njaa Tanzania ambapo walibaini kuwa juhudi mbalimbali ikiwemo matumizi ya data zinahitajika kuhakikisha wanaimarisha usalama wa chakula na lishe ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo 2030.
Dirisha hilo la ubunifu wa teknolojia litawakutanisha vijana wenye uwezo wa kutumia data kutoka vyanzo mbalimbali ambazo zinabainisha mahitaji ya wananchi, uchambuzi na data kufanya maamuzi sahihi ya kuboresha maisha ya wanawake na watoto.
Pia kuhakikisha kunakuwa na mtiririko na ushirikishwaji wa data, kuboresha vyombo vya kubadili tabia za jamii na kuimarisha majukwaa ya mawasiliano katika utolewaji wa huduma.

Wanawake ndiyo wanaoathirika zaidi kwa kukosa usalama wa chakula. Picha|SciDev.Net
Programu hiyo iliyojikita kutumia ubunifu wa data kutatua changamoto za jamii, imeelekeza nguvu zake katika Halmashauri 84 za Tanzania ambapo 12 kati ya hizo zimepewa kipaumbele kutokana na hali halisi za wananchi wake.
Baadhi ya Halmashauri hizo ni Bukombe (Kagera), Geita, Morogoro Mjini, Mji wa Ifakara (Morogoro), Urambo, Nzega (Tabora), Sengerema (Geita), Rorya, Musoma (Mara), Nkasi (Rukwa) na jiji la Mwanza.
WFP na DLI wanatekeleza programu hiyo inayoenda sambamba na Mpanga wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano (2016/17-2020/21), Mpango wa pili wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa(UNDAP II 2016-2021) na Mpango wa Taifa wa Lishe (NMNAP 2016/17) ambapo yote inalenga kupunguza umaskini na kuwawezesha wanawake kiuchumi.