‘Wezesha sasa’ yafungua fursa za ukuzaji mitaji Tanzania

Niwezeshe sasa itakuwa kimbilio la vijana na wabunifu mbalimbali hasa kwa urahisi wake kupatikana. Picha|Zahara Tunda.
- Ni mtandao mahususi kwa kuchangisha na kuchanga michango mbalimbali katika kuinua watu wa hali ya chini.
- Pia ni jukwaa muhimu kuwafungulia vijana fursa za biashara na mambo mengine ya kijamii.
Dar es Salaam. Mtandao wa “Wezesha Sasa” umezinduliwa rasmi ukiwa na lengo la kufanya harambee zitakazosaidia watu au makampuni kupata michango mbalimbali ili iliweze kuwasaidia kujikwamua katika changamoto za utendaji.
Uzinduzi huo umefanyika jana (Machi 20, 2019) katika ukumbi wa Seedspace jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wabunifu mbalimbali wa teknolojia ambao watakuwa wadau wakubwa katika kujipatia fursa zilizopo katika mtandao huo.
“Kabla ya kuanzisha Niwezeshe tulifanya utafiti na tukajifunza kuwa asilimia 10 ya kampuni changa zinatumia pesa zao kujiendesha au kupitia mashindano,” amesema Afisa miradi wa Niwezeshe Sasa Mwasapi Kihongosi.
Kihongosi amesema kilichowasukuma zaidi kuanzisha mtandao huo ni kuwasaidia vijana kupata michango kutokana na changamoto wanazokumbana nazo katika kuanzisha biashara.
Lakini imani yao kubwa ni kuwa mtandao huo utakuwa mwanga wa vijana wanaochipukia katika kujipatia mitaji na kuomba jamii iweze kuchangia kupitia mtandao huo.
Hata hivyo uanzishwaji wa mtandao huo ni mchakato wa muda mrefu wa mashindano yakutafuta vijana wabunifu wanaoweza kuleta maendeleo chanya kwenye jamii ya kutoka taasisi ya DLI (Data for Local Impact).
Inayohusiana: Wiki Ya Ubunifu inavyoangaziwa kuleta mabadiliko Tanzania
Mashindano hayo yaliyohusisha vijana wenye mawazo 367 na kati yao ni vijana 15 wabunifu wenye mawazo ya kipekee walichaguliwa ikiwemo Wezesha Sasa ambayo lengo lake ni kuinua watu kiuchumi.
“Imekuja muda muafaka na lengo lake ni kukuza uchumi wa wananchi wa kipato cha chini na wenye malengo ya kusaidia jamii,” amesema Mkurugenzi wa Mradi wa DLI, Agapiti Manday.
Pamoja na hayo, Manday ameshauri wadau mbalimbali watumie tovuti ya wezesha sasa ili waweze kujipatia fursa za kuchangiwa na kuchangia wengine ili kusaidiana kufikia malengo ya kujikwamua kiuchumi.