Waziri Ummy: Kuna changamoto utekelezaji wa Sera ya matibabu bure
- Asema haijafutwa bado makundi maalum yanahudumiwa kwa awamu.
- Wingi wa watu na hali ya kiuchumi yazuia utekelezaji wake kwa asilimia 100.
Dar es Salaam. Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema bado kuna changamoto katika utekelezaji wa wa Sera ya matibabu bure kwa makundi maalum ikiwemo wanawake, wajawazito, wazee na watoto walio chini ya miaka mitano.
Kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007, Serikali imeweka utaratibu wa kila mwananchi kulipia gharama za matibabu isipokuwa kwa makundi maalum ikiwemo wanawake wajawazito, wazee na watoto chini ya miaka umri wa miaka mitano ambao hupatiwa huduma hizo bure.
Waziri Ummy, aliyekuwa akizungumza katika mkutano wa wanahabari jijini Dar es Salaam leo Januari 10, 2024 amesema Serikali haijafuta Sera hiyo na kwamba utekelezaji wake unaendelea kufanyika kwa awamu licha ya changamoto zinazoikabili
“Sera ya Afya haijabadilika…nataka kukiri kuna changamoto katika kutekeleza Sera hii kutokana na ongezeko la idadi ya watu lakini pia hali ya yetu ya kiuchumi,” amesema Ummy.
Ufafanuzi huo wa Waziri Ummy unakuja wakati kukiwa na wingi wa malalamiko kutoka kwa wananchi hususan makundi maalum yanayotozwa fedha ili kupata huduma za afya tofauti na Sera ya Afya inavyoekeleza.
Kutokana na sintofahamu hiyo, baadhi ya wagonjwa katika makundi hayo wamekuwa wakipoteza maisha kutokana na kukosa fedha za matibabu.
Soma zaidi:Waliougua kipindupindu Mwanza wafikia 34
Mathalan kifo cha mjamzito kilichoripotiwa siku 10 zilizopita katika Hospitali ya wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, na kile kilichotokea jijini Tanga Novemba, 2023 wote wakipoteza maisha wakati wa kujifungua kwa kukosa fedha za matibabu.
Akijibu malalamiko hayo Waziri Ummy amesema huduma kwa wajawazito bado zinaendelea kufanyika kwa awamu ambapo kwa sasa Serikali inagharamia dawa muhimu na chanjo ili kulinda maisha ya kundi hilo na watoto ambao hawajazaliwa.
Amesema kwa upande wa watoto wenye umri chini ya miaka mitano Serikali inatoa huduma ya chanjo bure kwa magonjwa yasiyoambukiza kama polio, dondakoo, kifaduro, limonia, katika vituo vyote vya afya vinavyomilikiwa na Serikali.
“Hakuna mtoto yoyote atakayetakiwa kwenda katika kituo cha kutoa huduma za afya cha Serikali na akashindwa kupewa hizo chanjo kwahiyo hiyo Sera inatekelezeka,” amefafanua Ummy.
Hata wakati Serikali ikitoa huduma za bure kwa wazee, Naibu Waziri wa Afya Godwin Mollel amesema bado wananchi wanapaswa kutambua watakaonufaika ni wale wasiojiweza pekee ambao watatambuliwa kwa utaratibu maalum.
“Kuna utaratibu kama tunamtambua huyu mzee kwamba ni mzee asiyeweza kujilipia hayo yaeleweke vizuri,” amesema Mollel aliyekuwa sehemu ya wazungumzaji katika mkutano huo na wanahabari.

Waziri wa Afya Ummy Mwalim (katikati) pamoja na Watendaji wengine wa Wizara ya Afya wakizungumza na wanabari kuelezea hali ya utoaji wa huduma za afya kwa mwaka 2023 pamoja na vipaumbele vya sekta ya afya kwa mwaka 2024.Picha|Wizara ya Afya/Twitter(X).
Watakaosababisha vifo vya wajawazito kushughulikiwa
Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa Serikali itawachukulia hatua wahudumu wote wa afya watakaosababisha vifo vya wajawazito pamoja na watoto wakati wa kujifungua.
Pia, amemuagiza Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu kuimarisha maadili ya madaktari kupitia Baraza la Madaktari Tanzania (MCT) na kuwachukulia hatua watoa huduma watakaohusika.
“Na hapa nikuagize Mganga mkuu Mkuu ukaimarishe Baraza la Madaktari…wananchi wanataka kupata taarifa ya hatua mnazochukua kwamba tulipokea taarifa ya madakari 20 na wamechukuliwa hatua,” amesema Ummy.