Watu 10 wafariki dunia ajali ya boti Pemba, polisi wakimsaka nahodha
- Walikuwa wakienda msibani katika visiwa vya Panza
- Jeshi la Polisi lasema linamtafuta nahodha wa boti hiyo kama yupo hai kupata taarifa zaidi.
Dar es Salaam. Watu 10 wamefariki dunia baada ya boti waliyokuwa wakisafiria katika mkoa wa Kusini Pemba kuzama Jumanne jioni huku vikosi vya uokoaji vikiendelea kuwasaka wasafiri wengine waliohusika katika ajali hiyo.
Kamanda wa Mkoa wa Kusini Pemba Richard Mchomvu ameiambia Nukta kuwa watu hao walikuwa wakisafirisha msiba kwenda kwenye visiwa vya Panza kutokea Chakechake kabla ya boti yao kuzama katika Bahari ya Hindi.
Boti hiyo iliyozama, Mchomvu amesema, ilikuwa ni moja ya boti tatu zilikuwa zikienda msibani katika visiwa hivyo jirani.
“Boti mbili zilivuka salama na boti ya tatu ilizama ikiwa safarini. Jana jioni vikosi vya uokoaji vilifanikiwa kuwaokoa watu sita na wengine tisa walikuwa tayari wameshafariki dunia,” amesema Mchomvu.
Kamanda huyo amesema asubuhi ya Jumatano ya Januari 5, 2022 amejulishwa kuwa mwili mwingine umepatikana katika maeneo ya ajali hiyo na kufanya idadi ya waliofariki sasa kufikia 10.
Baadhi ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Kisiwa cha Pemba wakiwa katika Bandari ya Chokocho wakisubiria ripoti kutoka kwa maafisa wa uokozi waliokwenda kutafuta miili ya watu waliozama na boti katika eneo la Kisiwa Panza Januari, 04 2022. Picha|Hassan Msellem, Pemba.
Polisi wanaeleza kuwa boti hiyo huenda ilibeba zaidi ya watu 30 na vikosi vya uokoaji wakiwemo Kikosi Maalum ya Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM), Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na vinginevyo wanaendelea na jitahada za uokoaji.
“Hali ya hewa haikuwa ya ajabu sana kwa sababu boti mbili zilipita salama ile yenyewe ndiyo ilizama,” amesema Mchomvu alipoulizwa iwapo wanafahamu chanzo cha ajali hiyo.
Hadi sasa, Mchomvu amesema wanamtafuta nahodha wa boti hiyo iwapo kama alinusurika ili waweze kupata taarifa kamili ya kilichojiri ikiwemo idadi ya watu waliokuwemo katika chombo hicho.
Kwa kawaida, amesema boti za aina hiyo hazina tabia ya kuwa na taarifa za wasafiri ambazo zingesaidia mamlaka kuweza kubaini idadi kamili.
Latest



