Watoto wa Kigoma waongoza kwa kuteswa zaidi na Malaria Tanzania – Ripoti

October 23, 2018 10:39 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Kigoma ina kiwango kikubwa cha maambukizi ya Malaria kwa watoto chini ya miaka mitano kwa asilimia 24 ikifuatiwa na Geita, Kagera, na Mtwara.
  • Kiwango hicho cha maambukizi ni zaidi ya mara tatu ya wastani wa kitaifa wa asilimia saba.
  • Sababu kubwa ni uwepo wa mvua za msimu na huduma hafifu za afya.
  • Serikali imesema imejidhatiti kuangamiza mazalia ya mbu na kuboresha vituo vya afya.

Dar es Salaam. Watoto waliopo Kigoma ndiyo wanaoongoza kwa kushambuliwa zaidi na Malaria nchini baada ya ripoti mpya kuonyesha takriban robo ya watoto hao walikutwa na maambukizi ya ugonjwa huo ambao huchangia kwa kiasi kikubwa kuangamiza maisha ya watu duniani. 

Katika orodha hiyo, Kigoma inafuatiwa na Geita, Kagera, Mtwara, Ruvuma, Lindi na Tabora.

Ripoti ya utafiti wa Viashiria vya Malaria (Tanzania Malaria Indicators Survey(TMIS) ya mwaka 2017 iliyozinduliwa leo (Oktoba 22, 2018) inaonesha kuwa Kigoma inaongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha Malaria kwa watoto wenye umri wa miezi sita hadi 59 (kwa watoto wa chini ya miaka mitano) kwa asilimia 24, zaidi ya mara tatu ya wastani wa kitaifa.

Katika ripoti hiyo, asilimia  saba ya watoto wenye miezi sita hadi 59 nchini walikutwa na malaria jambo linaloonyesha kuwa ugonjwa huo umepungua mara mbili kitaifa ukilinganisha na asilimia 14 iliyorekodiwa katika utafiti wa mwaka 2015/2016. 

Hali ya hewa ya mkoa wa Kigoma ni ya kitropiki yaani yenye joto ambayo huufanya kuwa miongoni mwa mikoa inayopata mvua nyingi jambo ambalo kwa mujibu wa ripoti hiyo husababisha viwango vikubwa vya malaria. 


Hali ya hali hewa moja ya chanzo cha malaria

Kubainika kwa kiwango hicho kikubwa cha malaria katika mkoa wa Kigoma, kumetokana na utafiti huo kufanyika kati ya Oktoba hadi Disemba mwaka jana kipindi ambacho katika maeneo mbalimbali ya nchi malaria hujitokeza zaidi.

“Nchini Tanzania kuna vipindi viwili vya mvua, mvua za muda mfupi kati ya Novemba hadi Januari na mvua kubwa za Machi hadi Mei. LIcha ya kutofautiana kwa vipindi hivi, mabadiliko ya mvua, joto na unyevunyevu ambayo yana tabia ya hali ya hewa ya kitropiki yanachangia kuenea kwa malaria kila mwaka,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.   

Miongoni mwa sababu nyingine zinazofanya watu kupata malaria ni pamoja na baadhi ya kutotumia vyandarua ipasavyo ambavyo vingesaidia kuwakinga dhidi ya mbu waenezao malaria.

Pia inakabiliwa na changamoto nyingine zikiwemo upungufu wa vituo vya afya huku usambazaji na upatikanaji wa dawa unaosababishwa na miundombinu mibovu ukiwa ni tatizo kubwa.

Katika matokeo ya utafiti huo mpya, Kigoma imechukua nafasi ya Kagera ambayo katika utafiti wa TMIS wa mwaka 2015/2016 ilikuwa ikiongoza kwa asilimia 41.

Wakati Kigoma ikiongoza kwa malaria kwa watoto chini ya miaka mitano, kuna mikoa 10 nchini ina kiwango cha chini cha malaria mingi ikiwa kutoka Zanzibar ikiwemo Mjini Magharibi, Kaskazini Pemba, Kaskazini, Songwe na Manyara. Sehemu kubwa ya mikoa hiyo kiwango cha malaria kipo chini ya asilimia moja.

Hali hiyo inatokana na juhudi zilizofanyika katika kupunguza ugonjwa huo ambao ndio unaongozwa kwa kuua watu wengi duniani unaonezwa na vimelea vya malaria Plasmodia. Vimelea hivyo hungia katika mfumo wa damu kupitia kuumwa na mbu jike aitwaye Anopheles.

Matumizi ya vyandarua yaongezeka

Ripoti hiyo imebainisha uwepo wa ongezeko la matumizi ya vyandarua vilivyowekwa dawa na idadi ya watu wanaojitokeza kutibiwa katika katika vituo vya afya.

“Zaidi ya nusu ya watoto wa Tanzania walio chini ya miaka mitano na wananawake wajawazito walio kati ya miaka 15-19 wanatumia ITN (Vyandarua vilivyowekwa dawa),” inaeleza sehemu ripoti ya utafiti huo uliofanywa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar. Wadau wengine walioshiriki katika kufanikisha utafiti huo ni taasisi ya the Global Fund na Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID). 

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema Serikali itawekeza nguvu zake zaidi katika kuboresha huduma za afya na kudhibiti mazalia ya mbu ambayo ndiyo yamekuwa kisababishi kikubwa cha malaria nchini.

“Tunataka kuwekeza kwenye kuzuia mazalia ya mbu lakini jambo la pili tuweke huduma za kupima karibu zaidi kwa kila mtu lakini kuongeza zaidi matumizi ya vyandarua,” amesema Mwalimu.

Kwa upande wake Mke wa Rais Mstaafu, Mama Salma Kikwete amezipongeza halmashauri zilizopunguza  maambukizi ya Malaria katika maeneo yao na kubainisha kuwa “Tanzania bila malaria inawezekana” ikiwa halmashauri zenye viwango vya juu zitaongeza juhudi kutokomeza mazalia ya mbu na kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kutibiwa na kupata tiba sahihi.

Enable Notifications OK No thanks