Wasichana watawala 10 bora kidato cha nne 2021

January 15, 2022 9:30 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Consolata Prosper Lubuva wa St Francis Girls atajwa mwanafunzi bora kitaifa.
  • Wasichana saba waingia katika orodha hiyo.
  • St Francis Girls yaingiza wanafunzi saba 10 bora. 

Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka 2021 na kutaja wanafunzi 10 bora waliofanya vizuri kitaifa huku orodha hiyo ikitawaliwa na wasichana.

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde amewaeleza wanahabari leo Januari 15, 2022 jijini Dar es Salaam kuwa watahiniwa wa shule 422,388 sawa na 87.3 kati ya watahiniwa 483,820 wenye matokeo ya kidato cha nne wamefaulu mitihani yao muhimu kuingia katika elimu ya kidato cha tano.

Kwa mujibu wa orodha hiyo iliyotolewa na Necta wanafunzi wote 10 bora wanatoka katika shule zinazomilikiwa na watu binafsi isipokuwa Ilboru.

Orodha hiyo inaonyesha kuwa wasichana wamewagalaza wavulana katika 10 bora ambapo ni wavulana wawili tu ndiyo wamepenya katika orodha hiyo ya dhahabu.

Nafasi tano za juu zimechukuliwa na wanafunzi wasichana kutoka Shule ya St Francis Girls ya mkoani Mbeya ambapo Consolata Prosper Lubuva wa shule hiyo ndiye aliyetajwa kuwa mwanafunzi bora kitaifa.

Nafasi ya pili imeenda kwa Bhutoi Ernest Nkaganza huku Wilihelmina Steven Mijarifu akishika nafasi ya tatu, Glory John Mbele akishika nafasi ya nne na Mary George Ngoso akifunga tano bora ambayo wanafunzi wote wametoka St Francis.


Soma zaidi:


Holly Beda Lyimo kutoka Shule ya Sekondari Bright Future Girls ya jijini Dar es Salaam ameshika nafsi ya sita huku Blandina Karen Chiwawa (St Francis) amechukua nafasi ya saba.

Imam Suleiman Mogaeka kutoka Feza Boys ya jijini Dar es Salaam amepambana vikali na kuvunja ubabe wa wasichana katika nafasi ya nane.

Nafasi ya tisa imeenda kwa Mfaume Hamisi Madili wa Shule ya Sekondari ya Ilboru ya mkoani Arusha inayomilikiwa na Serikali huku Clara Straton Assenga wa St Francis ikifunga kazi ya 10 bora kitaifa.

Licha ya 10 bora kutawaliwa na shule binafsi, St Francis imefanikiwa kuingiza wanafunzi saba katika orodha hiyo na kuvunja rekodi ikizingatiwa katika matokeo ya mwaka juzi haikufanikiwa kuingiza hata mwanafunzi mmoja kwenye orodha hiyo.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW