Wanahabari, watafiti wakutanishwa meza moja kukuza sayansi
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dk Jim Yonazi aliyekuwa akizungumza katika semina hiyo jana. Picha|Costech.
- Wanaangalia namna ya kuyafikisha matokeo ya utafiti wa kisayansi kwa wananchi kwa njia iliyo rahisi na inayoeleweka.
- Tafiti za kisayansi ni nguzo muhimu ya kufanya maamuzi sahihi ya kisera na maendeleo.
Dar es Salaam. Huenda jamii ikaanza kunufaika na matokeo ya tafiti za kisayansi zinazofanyika nchini na wasomi, baada ya watafiti na wanahabari kuanza mchakato wa kutafuta namna ya kuyafikisha matokeo hayo kwa wananchi ili yaweze kuwasaidia katika kufanya maamuzi katika maisha.
Mchakato huo umefikiwa katika semina ya siku moja iliyoandaliwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) na Kituo cha mafunzo na utafiti cha Danida (Danida Fellowship Centre) iliyowakutanisha wadau wa vyombo vya habari na watafiti kubadilishana uzoefu na kujadili njia nzuri itakayowezesha matokeo ya kisayansi kuleta matokeo chanya kwenye jamii.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dk Jim Yonazi aliyekuwa akizungumza katika semina hiyo jana (Juni 3, 2019), amesema tafiti nyingi za kisayansi zinafanyika nchini lakini hazipati msukumo unaotakiwa kwa sababu kuna pengo kubwa kati ya watafiti na wanahabari.
Amesema pengo hilo ndilo limesababisha jamii isinufaike kwa sehemu kubwa na tafiti hizo ambazo nyingi zimekuwa zikibaki katika makabati ya taasisi za utafiti vikiwemo vyuo vikuu.
Hata hivyo, amebainisha kuwa pengo hilo linaweza likazibwa ikiwa wadau wa pande zote mbili watashirikiana kwa karibu katika shughuli zao ili kujenga mahusiano endelevu.
Amesema Wanahabari ndio wana vyombo vya mawasiliano na wako karibu zaidi na jamii hivyo ni muhimu kwa watafiti kuwatumia kikamilifu ili matokeo ya tafiti zao yafike katika ngazi ya chini kwa lugha nyepesi na inayoeleweka.
“Wanasayansi wanaweza kuwa na mawazo mazuri lakini wanatakiwa kufahamu wanahabari wanavyofanya kazi na kufikisha ujumbe kwenye jamii,” amesisitiza Dk Yonazi.
Soma zaidi:
- Kutana na Aneth David, mwanasayansi anayechipukia Tanzania
- CAG aisuta Costech kwa matumizi mabay ya fedha za wafadhili
Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu huyo, amesema ushirikiano huo ujikite katika kushughulikia changamoto za mawasiliano, maarifa, ubunifu na maslahi ya kifedha ambazo zimekuwa kikwazo kwa jamii kunufaika na matokeo ya tafiti za kisayansi.
Sayansi imekuwa sehemu muhimu ya kubaini matatizo yaliyopo katika jamii na kutafuta njia bunifu zilizohakikiwa na ushahidi wa kisayansi ili kuboresha maisha ya watu.
Kwa upande wake, Mtafiti wa masuala ya sayansi, Dk Khadija Malima amesema wameanza kuchukua hatua za kubuni miradi ya kutafsiri matokeo ya ushahidi wa kisayansi katika lugha nyepesi na inayoeleweka katika jamii.
Amesema tafiti za kisayansi ni nguzo muhimu ya kufanya maamuzi sahihi ya kisera na maendeleo kwa sababu zinaakisi hali halisi iliyopo katika jamii na mahitaji yake.
Naye mwakilishi wa Kituo cha mafunzo na utafiti wa Danida, Lise Brix amesema ili wanahabari wafanikiwe kuandika habari nzuri za kisayansi wanatakiwa kutumia dhana za kidijatali ikiwemo Google Schoolar, tovuti za www.sciencedirect.com na www.pubmed.com ili kupata tafiti mbalimbali za kisayansi zitakazowasaidia kutengeneza stori zenye manufaa kwa jamii.