Wanafunzi, wajasiriamali Tanzania kupigwa msasa teknolojia ya ‘Internet of Things’, ‘Big Data’

Vijana wanapata fursa ya kukutana na kujifunza vitu mbalimbali wakiwa katika kituo cha Buni. Picha| https://commons.wikimedia.org
- Ni mafunzo ya kuwaongezea ubunifu zaidi wa masuala ya intaneti kwa wote (Internet of Things) na matumizi ya taarifa lukuki za kompyuta (Big Data) ili kuongeza ufanisi kazini.
- Ni wakati wa wabunifu kwenye teknolojia kujifunza mbinu mpya.
- Wanafunzi wanaopenda masuala ya teknolojia ni wakati wa kujiandikisha katika mafunzo hayo.
Dar es Salaam. Baadhi ya wanafunzi na wajasiriamali jijini hapa watabahatika kuwa mabalozi wa awali katika teknolojia za kisasa zinazochipukia kwa kasi katika ulimwengu wa Tehama baada ya kupewa fursa ya mafunzo ya teknolojia ya intaneti inayounganisha vifaa mbalimbali kwa wakati mmoja kupitia simu ya mkononi (Internet of Things) na matumizi ya taarifa nyingi zinazozalishwa na kompyuta mtandaoni (Big Data).
Katika mafunzo hayo ya siku nne yatakayotolewa na Kituo cha ubunifu cha Buni hub wakishirikiana na Wazi hub, wanafunzi na wajasiriamali wa teknolojia watasaidiwa kubuni kutengeneza mawazo yao kwa kuhusisha intaneti ya vitu ambayo inatumika zaidi katika vitavyoisaidia moja kwa moja kuleta unafuu wa kazi za kila siku kwa binadamu. Mafunzo hayo yataanza Oktoba 8 hadi 11 mwaka huu katika kituo cha Buni hub.
Intaneti ya vitu inatumika zaidi katika kusaidia kuwa na mfumo ambao unakuwezesha kuendesha vitu vyako ambavyo ungetakiwa kufanya mwenyewe kwa kutumia intaneti katika simu janja (Smartphone) yako au katika kompyuta au mashine yenye uwezo wa kufanya kazi bila wewe kuwepo.
Inayohusiana: Wanafunzi wa kike shule za kata wapata fursa ya kujifunza programu za kompyuta
Baadhi ya kazi za IoT ni kufanikisha matumizi ya simu ya mkononi kulinda au kuendesha milango ya nyumba yako , kuwasha au kuzima vifaa mbalimbali nyumbani kwako hata ukiwa mbali na nyumbani kwako.
Teknolojia ya Big Data yenyewe inatumika katika kujifunza tabia mbalimbali za wateja pamoja na kuhifadhi taarifa na kuzitumia katika sekta mbalimbali ili kuboresha huduma za kazi.
Pamoja na fursa hiyo kwa wanafunzi, watengenezaji wa programu za simu na kompyuta na wajasiriamali, bado wadau wanawashauri waandaaji kutumia njia nyingi za matangazo ili kuwafikia walengwa kwani sio wote wanaijua Buni na wamewafuata katika mitandao ya kijamii.
“Ni fursa nzuri na zinafungua uelewa zaidi ila wabuni njia ya kuwafikia watu wengi zaidi. Mimi nimeona kwa sababu nimewafuata katika mitandao ya kijamii sasa inakuwaje wale ambao hawawafuati katika mitandao hiyo?” amesema Mhandisi programu za kutengeneza kompyuta na simu, Juma Kabiero.
Latest
