Wanafunzi shule za msingi, sekondari kusoma kwa lazima masomo ya biashara Tanzania
- Itasaidia kuendana na mahitaji ya sasa ya kijamii, kiuchumi na soko la ajira.
- Vyuo vikuu kuja na zaidi ya programu 300 za uchumi.
Dar es Salaam. Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia inatarajia kuyafanya masomo ya biashara kuwa ya lazima kwa wanafunzi wa sekondari ili kuendana na mahitaji ya sasa ya kiuchumi, kijamii na ushindani katika soko la ajira.
Kwa muda mrefu wadau wa elimu pamoja na wadau wa uchumi wamekuwa wakiishauri Serikali kufundisha masomo ya uchumi kwa wanafunzi wa Tanzania ili kuwajengea uwezo wa kuelewa misingi ya uchumi toka wangali wadogo.
Naibu Waziri wa Elimu Omari Kipanga aliyekuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Zainabu Katimba, amewaambia wabunge kuwa wizara yake inatambua umuhimu wa masomo ya biashara hivyo imepanga masomo hayo kuwa ya lazima.
Awali mbunge huyo wa wa viti maalumu alimuuliza Waziri Kipanga kuwa ni lini serikali itaboresha mitaala ya elimu ili mafunzo ya biashara yatolewe kuanzia shule za msingi.
“Wizara inatambua umuhimu wa somo la biashara na hivyo somo hili limepangwa kuwa la lazima kwa wanafunzi wote kuanzia kidato cha kwanza hadi nne kwa mikondo yete miwili ya elimu ya jumla na amali,” amesema Kipanga jijini Dodoma.
Kipanga ameongeza kuwa katika maboresho ya Sera ya Elimu ya mwaka 2014, elimu ya Shule za Msingi (darasa la kwanza hadi sita) mitaala imetilia mkazo elimu ya fedha pamoja na elimu ya ujasiriamali.
“Elimu ya fedha imechopekwa katika somo la Hisabati na elimu ya ujasiriamali imechopekwa kwenye somo la Sanaa, Michezo, Lugha, Jiografia na Mazingira,” amebainisha Naibu Waziri Kipanga.
Kabla ya mabadiliko haya ya mitaala yanayoendelea kufanyika, awali masomo ya uchumi na biashara yalikuwa yanafundishwa katika baadhi ya shule kwa lazima kidato cha kwanza na cha pili pekee na wanafunzi husoma kwa hiyari kuanzia kidato cha tatu na kuendelea.
Elimu ya juu haijaachwa
Aidha, kwa mujibu wa Kipanga taasisi za elimu ya juu za Serikali na binafsi, kupitia mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya uchumi zimeshapewa mafunzo ya namna ya kutoa programu zinazoendana na mahitaji ya nchi na soko la ajira.
“Kupitia utaratibu huu zaidi ya programu 300 zitaanzishwa na kuhuishwa ikiwemo somo la biashara ili kuendana na mahitaji ya sasa ya kijamii, kiuchumi na soko la ajira,” amesema Katanga.
Latest
