Wamiliki hoteli za Ngurdoto, Impala wadai fidia Sh10 bilioni kwa kudhalilishwa

Hoteli ya Ngurdoto iliyopo mkoani Arusha. Picha|Mtandao.
- Wanaidai kampuni ya uwakili ya Locus Attorney iliyochapisha tangazo la kuuza hoteli hizo kwa madai zimeshindwa kurejesha mkopo katika Benki ya Exim.
- Pia wameitaka kampuni hiyo iombe msamaha kuwa hatarudia tena kufanya udhalilishaji huo.
- Kama itashindwa kutekeleza maelekezo hayo, watafungua kesi mahakamani.
Dar es Salaam. Wamiliki wa Hoteli za Ngurdoto na Impala za mkoani Arusha wanataka kulipwa fidia ya Sh10 bilioni na kuombwa msamaha na kampuni ya uwakili ya Locus Attorney waliochapisha tangazo la kuuza hoteli hizo kwa madai zimeshindwa kurejesha mkopo katika Benki ya Exim.
Hoteli hizo ambazo zinamilikiwa na wafanyabiashara kadhaa nchini, ambapo Mkurugenzi wake Mkuu, Melau Mrema alifariki mwaka 2017 zilitangazwa kuuzwa jana (Aprili 3, 2019) kwa tangazo lililotolewa katika vyombo vya habari ambapo mnunuzi alitakiwa kutuma zabuni kwa kampuni hiyo kupitia wakili Dk Onesmo Kyauke kabla ya April 15 mwaka huu.
Kwa mujibu barua iliyotolewa na kampuni ya uwakili ya Dexter Attorneys ya Jijini Arusha kwa niaba ya wamiliki wa hoteli hizo inaeleza kuwa madai hayo yaliyotolewa ni ya uongo na wamiliki hao hawana deni lolote kutoka benki ya Exim.
Imeeleza kuwa tangazo hilo limemvunjia heshima mteja wake na kumsababishia mfadhaiko, unyanyasaji na hasara katika biashara ya hoteli hizo za kitalii.
Kutokana na matokeo hayo hasi waliyopata wamiliki hao, kampuni ya Locus Attorney imetakiwa kuomba msamaha na kukiri kuwa hawatarudia tena kutoa tuhuma za uongo kwa kuchapisha katika gazeti lenye mzunguko mkubwa nchini.
“Kutokana na mazingira yenyewe, mteja wetu anakutaka uombe msamaha mara moja na kukiri kuwa hutarudia tena kutoa madai hayo,” ameeleza Wakili Salimu Juma katika taarifa hiyo.
Soma zaidi:
- Waziri Kanyasu ataka tathmini ifanyike ajira hoteli za kitalii Tanzania
- Tanzania yaangazia masoko 18 duniani kukuza utalii
- Tanzania yang’ara tena tuzo za eneo bora la utalii duniani
Pia wanatakiwa kulipa Sh10 bilioni kama fidia kwa kusababisha usumbufu kwa mteja wao ikiwemo kumdhalilisha na kutatiza mwenendo wa biashara ya hoteli hizo.
Juma amesema wanatakiwa kutekeleza maelekezo hayo leo Aprili 4, 2019 na endapo watakaidi watafungua kesi mahakamani kwa hatua zaidi ili kupata haki yao.
Hoteli za Impala na Ngurdoto zimekuwa maarufu kutokana na uwezo wake wa kupokea watalii wa kimataifa na watu maarufu duniani ambapo zimekuwa sehemu muhimu ya kufanyia mikutano mbalimbali.
Benki ya Exim Tanzania ambayo ilitajwa katika tangazo hilo imesema haijamteua Dk Onesmo Kyauke wa Locus Attorneys wala haina mikopo na Ngurdoto Mountain Lodge Limited au Impala Hotel Limited.
Tangazo lilichapishwa kimakosa na Locus Attorneys kwa sababu zinazojulikana na wao lakini bila ya maelekezo au idhini yoyote ya kufanya hivyo kutoka Benki ya Exim Tanzania,” imeeleza taarifa iliyotolewa kwa umma na benki hiyo leo.
Benki ya Exim Tanzania pia imeiomba radhi hoteli ya Ngurdoto na Impala kwa shida au fedheha zilizosababishwa na kosa la Locus Attorneys.
Hata hivyo, Dk Kyauke ameomba radhi kwa usumbufu uliotokea kwa wamiliki wa hoteli hiyo ambapo alipewa uwakala wa kuuza hoteli hizo na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na siyo Exim Bank Tanzania kama ilivyoripotiwa awali.