Waliosajili laini za simu kwa alama za vidole wafikia milioni 31.4, Serikali yatoa onyo
- Serikali yasema idadi hiyo ni sawa na asilimia 71.6 za laini zote za simu milioni 43.9 zilizokuwepo hadi Februari 2, 2020.
- Yasema zoezi la usajili ni endelevu lakini haitasita kuwafungia wasiosajili.
- Nida yatakiwa kuongeza kasi ya utoaji wa vitambulisho vya Taifa.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema hadi kufikia Februari 2 mwaka huu, jumla ya laini za simu milioni 31.4 zimesajiliwa kwa alama za vidole, huku akiwahimiza ambao hawajasajili laini zao kwa sababu mbalimbali kufanya hivyo ili kuepuka usumbufu wa kusitishiwa mawasiliano.
Amesema laini hizo za simu zilizosajiliwa kwa alama za vidole ni asilimia 71.6 ya laini zote za simu milioni 43.9 ambazo zilikuwepo hadi siku hiyo.
Hiyo ni sawa na kusema kwa kila laini za simu 10 basi laini tatu hazisajiliwa, jambo linalowaweka hatarini wamiliki wake kukosa mawasiliano ya simu.
Majaliwa aliyekuwa akizungumza leo (Februari 7, 2020) wakati akihitimisha mkutano wa 18 wa Bunge la 11 jijini Dodoma, amesema zoezi la usajili wa laini za simu kwa alama za vidole ni endelevu.
“Hadi kufikia tarehe 2 Februari, 2020 kulikuwa na jumla ya laini za simu milioni 43.9. Laini za simu milioni 31.4 sawa na asilimia 71.6 zilikuwa zimesajiliwa kwa alama za vidole. Zoezi la usajili wa laini za simu kwa alama za vidole ni endelevu. Uzimaji wa laini za simu unaendelea,” amesema Majaliwa.
Katika kufanikisha zoezi hilo, ameitaka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) kuongeza kasi ya utoaji namba ya utambulisho wa uraia (NIN) na vitambulisho ili wananchi wapate fursa ya kusajili laini zao.
“Ninawahimiza wananchi wote ambao hawajasajili laini za simu kwa sababu mbalimbali na wale ambao wanaendelea na zoezi la kupata vitambulisho vya uraia na wamekwishapata namba ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) waendelee kusajili laini zao za simu kwa mujibu wa sheria ili kuepuka usumbufu wa kusitishiwa huduma za mawasiliano,” amesema Majaliwa.
Soma zaidi:
- Simu za mkononi sasa kupima ugonjwa wa kifua kikuu
- Apple yaingiza sokoni simu mpya zinazotumia mfumo wa ‘eSIM’
- Mhandisi Nditiye atoa ufafanuzi usajili wa laini za simu kwa kutumia alama za vidole
Katika hatua nyingine, Majaliwa ametoa tathmini ya zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura linaloendeshwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na kubainisha kuwa mpaka sasa wapiga kura milioni 18.5 wameandikishwa.
Amesema Nec imeendelea na uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa awamu ya kwanza ambapo hadi kufikia Febriuari 2, 2020 imekamilisha uandikishaji wapiga kura katika kanda ndogo 12 kati ya 14 zilizopangwa katika awamu ya kwanza.
“Idadi ya wapiga kura walioandikishwa kuanzia kanda ndogo ya kwanza hadi ya kanda ya 12 walikuwa milioni 18.5. Jumla ya wapiga kura milioni 2.2 wamejitokeza kuboresha taarifa zao sawa na asilimia 11.4 ya idadi ya wapiga kura walioandikishwa mwaka 2015 katika kanda ndoto zote 12,” amesema.
Baadhi ya mikoa iliyopo katika kanda hizo ni pamoja na Kilimanjaro, Mara, Shinyanga, Rukwa, Singida, Tabora, Mtwara, Mbeya na Zanzibar.
Amebainisha kuwa idadi ya wapaiga kura wapya waliojiandikisha katika kanda zote 12 ni milioni 5.6 sawa na asilimia 31.8 ya idadi ya wapiga kura walioandikishwa mwaka 2015.
Hilo ni sawa na ongezeko la asilimia 13.8 ya makadirio ya awali ya asilimia 17.
Vilevile, idadi ya waliondolewa na kupoteza sifa ni 14,894 ambayo ni sawa na silimia 0.08 ya wapiga kura wote walioandikishwa mwaka 2015 wakiwemo waliofariki.
Ameitaka Nec iongeze kasi ya uandikishaji ili kuwafikia wananchi wote wapate kitambulisho cha mpiga kura kitakachowawezesha kupata haki ya kuwachagua viongozi katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu.
Latest
