Wahalifu wavamia mikutano inayofanyika mtandaoni

May 20, 2020 4:54 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Baadhi ya wadukuzi wanaingilia mikutano ya watu na kuweka maudhui yasiyofaa ikiwemo picha za ngono, jambo linalowatisha wahusika kufanya vikao mtandaoni. 
  • Kampuni zinazotoa huduma ya mawasiliano ya video mtandaoni zimeimarisha usalama na kuongeza usiri wa wateja wake.
  • Matumizi ya neno la siri na kuweka chumba maalum cha kidijitali kumewasaidia watumiaji wa mitandao. 

Dar es Salaam. Wakati kampuni nyingi zikifunga shughuli zake na kuwaruhusu wafanyakazi kufanyia kazi nyumbani, kampuni zinazotoa huduma ya mawasiliano kwa njia ya video nazo zimejipatia wateja wengi wanaotumia huduma zao.

Pia baadhi ya watu wenye nia mbaya wameanza kuingilia mazungumzo ya vikao na mikutano ya watu inayofanyika mtandaoni kwa nia ya kuvuruga kazi na hata kudukuwa taarifa muhimu za kampuni. 

Baadhi ya wadukuzi wanaingilia mikutano ya watu na kuweka maudhui yasiyofaa ikiwemo picha za ngono, jambo linalowatisha wahusika kufanya vikao mtandaoni. 

Hata hivyo, kampuni zinazotoa huduma hiyo ikiwemo Zoom Video Communications zinafanya kila jitihada kudhibiti vitendo hivyo kwa kuimarisha miundombinu yao ya mawasiliano ili kuhakikisha usiri wa wateja wao unazingatiwa. 

Kampuni hiyo yenye makao makuu Jijini California, Marekani haiwasaidii wafanyakazi pekee bali familia na hata wanafunzi wanoitumia kukutana na walimu mtandaoni kwa ajili ya kuelekezana mambo mbalimbali.

Mkurugenzi wa kampuni ya Zoom Video Communications  Eric Yuan amekiri uwepo wa changamoto hizo na kubainisha kuwa hatua za kuzitatua zimeshaanza kufanyika.

Yuan amesema hayo wakati akihojiwa na Shirika la Habari la CNN la Marekani na kuongeza kuwa, “tulienda kwa kasi kubwa sana…na tulikosea mahali.”

Hadi sasa Zoom imechukua hatua mbili kudhibiti watu kuingia kwenye mikutano isiyowahusu ikiwemo uwezo wa kiongozi kuweka neno la siri na kuwapatia wahusika wa mkutano huo tu pamoja na chumba cha kidijitali cha kusubiri kabla kikao au mkutano kuanza.


Zinohusiana


Mwendesha mkutano/ kiongozi wa mkutano ndio ataweza kuruhusu mtu kuingia kwenye mkutano hata baada ya kuweka neno la siri na kiunganishi cha mkutano.

Njia hiyo siyo tu itaondoa wageni wasiohusika kwenye mkutano, bali usalama wa watu wanaokuwa kwenye mkutano.

Hata hivyo,  migongano hiyo huenda imesababishwa na ongezeko la watumiaji wa mtandao huo ambapo kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Yuan, watumiaji wa mtandao huo kwa siku wamefika milioni 200 ilipofika Aprili1, 2020 kutoka watumiaji milioni 10 Disemba 2019.

Hiyo ni sawa kusema watumiaji wameongezeka mara 20 katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, jambo linalohitaji mifumo imara kuwalinda watumiaji na uvamizi wa kila namna.

Enable Notifications OK No thanks