Mifumo ya kidijitali kupaisha uchumi 2019
Teknolojia ya dijitali inasaidia kuongeza ufanisi katika shughuli za utoaji huduma na uzalishaji wa bidhaa. Picha|Mtandao.
- Mifumo hiyo itasaidia katika ukuaji wa uchumi wa nchi za Afrika zilizo Kusini mwa jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania ambao umeendelea kuwa chini kwa miaka minne mfululizo.
- Kiwango cha ukuaji uchumi katika bara hilo kwa mwaka huu wa 2019 kinatarajiwa kuwa ni asilimia 2.8 lakini ukuaji wake hautakuwa wa kuridhisha.
- Tanzania nayo yajipanga kutumia vya vya ndani na nje vya mapato na uwekezaji kuchagiza ukuaji wa uchumi.
Dar es Salaam. Ripoti mpya ya Benki ya Dunia (WB) ya uchumi wa nchi za Afrika zilizo Kusini mwa jangwa la Sahara inaeleza kuwa ukuaji wa uchumi kwa nchi hizo umeendelea kuwa chini kwa miaka minne mfululizo ikilinganishwa na ongezeko la idadi ya watu licha ya matumaini ya ukuaji uchumi katika bara hilo kwa mwaka huu wa 2019 kuwa ni asilimia 2.8.
Wakati uchumi wa Afrika ukiendelea kuwa chini, baadhi ya nchini za bara hilo za Tanzania, Ethiopia, Rwanda, Ghana, Ivory Coast,Senegal, Benin, Kenya, Uganda, na Burkina Faso uchumi wake umeendelea kukua kwa kasi na kutoa somo kwa nchi zingine za bara hilo.
Ripoti hiyo mpya ya Benki ya Dunia iitwayo Pulse’s Africa ambayo hupima hali ya uchumi wa nchi za Afrika mara mbili kwa mwaka ilitolewa jana (Aprili 8, 2019) NewYork, Marekani imeeleza kuwa kutokana na sababu za ndani na nje ya nchi hizo, kiwango cha ukuaji kwa mwaka jana kimepungua hadi asilimia 2.3 kutoka asilimia 2.5 mwaka uliotangulia wa 2017.
Hali hiyo haitofautiani sana na miaka iliyotangulia ambapo ripoti hiyo imemabainisha kuwa sababu kubwa ya uchumi kuendelea kuwa chini ni madeni yasiyolipika ambapo mpaka mwishoni mwa mwaka 2018 karibu nusu ya nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara zilikuwa katika kundi ya nchi zenye uchumi mdogo huku zikilemewa na madeni ya nje yenye riba kubwa.
Pia imeeleza kuwa ukosefu wa utulivu na mikakati endelevu ya kuimarisha taasisi za ndani za uwajibikaji na uwazi, nayo ni sababu nyingine inayozikwamishwa nchi hizo kukua kiuchumi.
Hata hivyo, imeeleza kuwa kuna matumaini ya ukuaji wa uchumi katika eneo hilo ambapo mwaka huu uchumi utakuwa kwa asilimia 2.8 na utaendelea kukua lakini sio kwa kiwango kikubwa.
Soma zaidi:
- Karafuu yachangia kushuka kwa mauzo ya nje Zanzibar
- BoT yashusha tena riba kwa benki za biashara Tanzania
Kutokana na hali hiyo, nchi hizo ikiwemo Tanzania zimetakiwa kuwekeza katika uendelezaji wa mifumo ya dijitali ili kuwapa fursa wajasirimali na walaji kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi zao.
Mifumo ya kidijitali ni pamoja na usajili wa biashara kwa njia ya mtandao, matumizi ya huduma za kibenki kwa njia ya simu za mkononi na kutumia teknolojia ya kisasa katika shughuli za biashara ili kuleta matokeo chanya ikiwemo kuongeza ufanisi wa uzalishaji bidhaa na utoaji huduma za msingi.
Sambamba na hilo ni kutumia teknolojia ya dijitali katika sekta ya kilimo ambayo kinategemewa na nchi nyingi za Afrika ili kuongeza uzalishaji wa mazao na upatikanaji wa soko la ndani na la kimataifa litakalochochewa na uanzishwaji wa viwanda vya kutengeneza bidhaa.
Tanzania imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuimarisha na kukuza uchumi wake ikiwemo kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara kwa kuimarisha miundombinu ya barabara, bandari na usafiri wa anga ili kuvutia wawekezaji wengi.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2018/2019 na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2019/2020, katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2018, Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 6.7 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.2 katika kipindi kama hicho mwaka 2017.
Katika taarifa hiyo iliyowasilishwa bungeni Aprili 4, 2019, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema katika mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kuimarisha na kujenga misingi na mifumo imara ya ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa lengo la kuwa na mapato endelevu kwa ajili ya kugharamia matumizi yake na kusimamia jukumu lake la msingi la kutafuta mapato kutoka vyanzo vya ndani na nje na kusimamia kikamilifu matumizi ya fedha za umma kupitia bajeti ya Serikali itakayowasilishwa hapa Bungeni mwezi Juni 2019.