Vyandarua zaidi ya 700,000 kupambana na malaria Rukwa
- Vitagawiwa chini ya kampeni maalum katika halmashauri zote nne za mkoa huo.
- Vitasaidia kupunguza maambukizi ya malaria mkoani humo.
- RC Wangabo asema Serikali iangalie miti shamba inayoweza kupambana na mbu.
Dar es Salaam. Vyandarua 719,254 vinatarajiwa kugawiwa kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa ikiwa ni muendelezo wa kampeni ya kudhibiti na kutokomeza ugonjwa wa malaria nchini Tanzania.
Katika kampeni hiyo inayotekelezwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) vyandarua hivyo vitagawanywa katika Halmashauri zote nne za mkoa huo uliopo Kusini Magharibi mwaka Tanzania.
Mwakilishi wa Wizara ya Afya Peter Gitanya amesema ugawaji vyandarua hivyo ni muendelezo wa kampeni za uhamasishaji zilizofanyika miaka ya 2009, 2010 na 2015/2016.
Vyandarua vitavyopelekewa Rukwa ni sehemu ya vyandarua milioni 7.1 vitakavyogawiwa katika Halmashauri 50 kutoka katika mikoa 10 nchini.
Amesema Bohari ya Dawa (MSD) itahusika na usafirishaji wa vyandarua hivyo kutoka maghala yao katika kila mkoa hadi kituo cha ugawaji katika kijiji ama mtaa husika.
“Halmashauri ambako kampeni itafanyika ni zile halmashauri ambazo zina kiwango cha chini cha umiliki wa vyandarua, chini ya asilimia 40 na pia maambukizi ya malaria yapo katika kiwango cha juu na cha kati,” amesema Gitanya.

Huenda kampeni hiyo ya ugawaji vyandarua ikaisaidia mkoa huo kupunguza zaidi kiwango cha malaria hasa kwa watoto wadogo.
Ripoti ya utafiti wa Viashiria vya Malaria (Tanzania Malaria Indicators Survey(TMIS) ya mwaka 2017 inaonyesha kiwango cha maambukizi katika mkoa wa Rukwa ni asilimia 1.8 kikiwa chini ya wastani wa kitaifa wa asilimia 7.3.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo amewataka wahusika wote wa kampeni hiyo kushirikiana kwa karibu katika kufikisha elimu kwa wananchi juu ya matumizi sahihi ya vyandarua.
“Ili mpango huu uweze kufanikiwa, tunahitaji tushikamane, tushirikiane kwa nguvu zote kufikisha elimu iliyo sahihi kwa wananchi, vinginevyo tusipotoa elimu kwa nguvu zote na watu wakaelewa tunaweza tukatwanga maji kwenye kinu,” amesema Wangabo.
Soma:
Watoto wa Kigoma waongoza kwa kuteswa zaidi na Malaria Tanzania – Ripoti
Miti shamba kutumika kufukuza mbu?
Wangabo ameishauri Wizara ya Afya kuona namna ya kufanya utafiti juu ya miti shamba inayotumika kufukuza mbu katika baadhi ya maeneo vijijini ili wananchi waweze pia kutumia miti hiyo kwa kuipanda maeneo ya nyumba zao na hatimaye kuwalinda na wadudu hao hatari.
Mkakati wa Tanzania ni kuhakikisha inatokomeza ugonjwa huo nchini kutoka maambukizo ya asilimia 7.3 hivi sasa hadi asilimia 1 ifikapo mwaka 2030.
Latest