Vuta nikuvute Harmonize, Diamond, Rayvanny YouTube
- Harmonize aongoza mtanange baina ya nguli hao.
- Diamond hashikiki kwa watazamaji wa nyimbo zake.
- Albamu mpya ya Rayvanny. Je itafua dafu?.
Dar es Salaam. Ndani ya siku 60, nguli wa muziki wa miondoko ya Bongo fleva Naseeb Abdul (Diamond), Raymond Shaban (Rayvanny) na Rajabu Abdul (Harmonize) wameendelea kuchuana vikali katika chati za mtandao wa Youtube huku spika za mashabiki wao zikishindwa kuchagua zisikike kwa muziki wa nani.
Kufikia leo Machi 4, 2020, wasanii hao wameendelea kuuwasha mtandao huo kwa nyimbo za video huku kila mmoja akijaribu kuzikonga nyoyo za mashabiki wake kikamilifu.
Uchambuzi programu ya Google Trends kuhusu kufuatiliwa kwa wasanii hao Youtube, mtanange baina yao sio haba licha ya kuwa Harmonize anaongoza kwa muda mrefu ikilinganishwa na wenzake.
Hata hivyo, bado msanii huyo ana kibarua kizito cha kuendelea kujiimarisha zaidi kwenye YouTube dhidi ya Diamond na Rayvanny.
Ushindani wa Harmonize, Diamond na Rayvanny kwenye mtandao wa Youtube, mstari wa umaarufu wa Harmonize ukiongoza . Picha| Google trends.
Harmonize anayetamba na kibao cha Hujanikomoa chenye watazamaji milioni 1.3 ameongoza kwa kufuatiliwa zaidi katika mtandao huo lakini idadi ya watazamaji wa kazi zake imemuangusha akilinganishwa na wenzake.
Huku mshale wake wa umaarufu kwenye Google trends ukigota kufikia asilimia 100 (kima cha juu zaidi) mara moja ndani ya siku 60, Rayvanny na Diamond hawajakifikia kilele hicho.
Kwa mahesabu ya jumla, Harmonize ana wastani wa asilimia 30, akifuatiwa na Diamond mwenye wastani wa asilimia 21 na Rayvanny akiwa na wastani wa asilimia 19.
Zinazohusiana
- Maisha ya msanii Harmonize mtandaoni nje ya Wasafi
- Pigo jingine kwa Rayvanny: Serikali ya Kenya yafungia wimbo wa Tetema
- Kwangwaru ya Harmonize inavyotikisa Youtube
Kwa upande wake Mkurugenzi wa lebo ya muziki ya Wasafi Classic Baby (WCB), Diamond ambaye sasa anatamba na kibao cha Jeje ambacho ndani ya siku sita, wimbo huo una watazamaji milioni 3.6.
Rayvanny ambaye mwezi Februari umekuwa wa kujaa harakati, ametoa albamu yake ya “Flowers” yenye nyimbo nane, kwa sasa anatamba na kibao cha Vumilia chenye wiki moja tangu kiwekwe hewani huku kikiwa na watazamaji zaidi ya 780,000 YouTube.
Tofauti hizi zinatokana na utofauti wa kutoa nyimbo baina ya wasanii hawa. Endelea kufuatilia chambuzi hizi kila mara.
Latest