Vipaji vya Ruge viliinyima familia yake ‘kumfaidi’
- Amesema baba yake alikuwa na vipaji vingi ikiwemo uandishi na uchezaji mpira vilivyomfanya asiwe karibu na familia yake.
- Amesema majukumu ya kijamii aliyokuwa anafanya Ruge yaliwakosesha ‘kumfaidi’ baba yao.
Dar es salaam. Mtoto wa kwanza wa marehemu Ruge Mutahaba, Mwachi amesema baba yake alikuwa na vipaji vingi ikiwemo uandishi na kucheza mpira vilivyomfanya asiwe karibu na familia yake.
Akiongea kwa mojonzi huku akitokwa na machozi mara kwa mara wakati akitoa wasifu wa baba yake leo (Machi 2, 2019) katika shughuli ya kumuaga iliyofanyika katika viwanja vya Karimjee ambapo amesema Ruge alijihusisha zaidi na jamii kuliko familia na wao kama binadamu walitaka ‘kumfaidi’.
“Familia tangia zamani ilikubali kuwa Ruge sio wao peke yao na tunakiri kuna muda tuliona familia ya nje inafaidi kuliko familia ya ndani japo tulikuwa tunatambua alikuwa na majukumu mazito ya kazi lakini nasi ni binadamu tulitaka tumfaidi,” amesema Mwachi.
Vipaji na uwezo wake wa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja ulimfanya Ruge kukubalika na watu wengi ambao walitaka awasaidie kuendeleza vipaji vyao.
Amesema Ruge hakuwa na kipaji cha muziki pekee bali alitamba hadi kwenye soko la mpira wa miguu ambapo alikuwa ni mchezaji mzuri na kipaji hicho kingeweza kumfikisha mbali kwa sababu aliwahi kuchaguliwa kuingia katika timu ya mkoa wa Dar es Salaam katika mashindano ya shule za sekondari ya Umiseta.
Pia alikuwa na kipaji cha kuandika, Mwachi amesema maandishi yake yalikuwa yanainufaisha familia na wadogo zake na yalikuwa yanakimbizana na vitabu kama ‘Huli gamba’ na vitabu vya ‘Kufa na Kupona’ ingawa hakufanikiwa kuandika kitabu.

Rais John Magufuli akitoa heshima za mwisho kwa marehemu Ruge Mutahaba alipoongoza waombolezaji kuuaga mwili marehemu katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam leo Machi 2, 2019. Picha|Mtandao.
Mwachi amebainisha kuwa vipaji vyote vya baba yake vilishindwa kunawili kwa sababu damu yake ilikuwa kwenye muziki na alishikilia huko mpaka mauti yalipomkuta Februari 26, 2019.
“Ujasiliamali wa Ruge na muziki ulianza mbali sana tunakumbuka akiwa bado shule ya msingil aliandaa event (tukio) ya nyumba 10 iliyokuwa na waimbaji, sarakasi na maigizo na watu walikuwa wananunua tiketi na tiketi zilikuwa Sh5 na kuweza kujiingizia kipato,” amesema.
Soma zaidi: Watanzania wamlilia Ruge kila kona
Mwanzo, mwisho wa Ruge
Akieleza wasifu wa baba yake, Mwachi amesema alizaliwa Mei 1, 1970 huko Brooklyn, New York nchini Marekani akiwa ni mtoto wa kwanza kati ya watano katika familia ya Profesa Mutahaba.
Alipata elimu yake ya msingi kuanzia darasa la kwanza mpaka la sita katika shule ya Arusha School na baadaye alimaliza elimu ya msingi katika shule ya msingi Mlimani ya jijini Dar es Salaam.
Mwachi amesema baadaye aliendelea na elimu yake ya sekondari katika shule ya sekondari ya Forodhani na kuchaguliwa kwenda shule ya sekondari ya Pugu kwa ajili ya elimu ya kidato cha tano na sita .
Alipohitimu Pugu alienda nchini Marekani kwa ajili ya kuendelea na elimu yake ya chuo kikuu na kufanikiwa kuhitimu shahada yake ya kwanza ya Masoko mwaka 1995 katika Chuo Kikuu Cha San Hose nchini Marekani.
Baada ya kuhitimu masomo alirudi Tanzania kuendelea na shughuli zake ikiwemo kuupambania muziki.
“Baba alikuwa ni mtoto ambaye tangia zamani alikuwa anapata anachotaka kwa namna anavyojua yeye, tangu maisha ya utotoni Ruge na muziki wamekuwa kitu kimoja” amebainisha Mwachi.
Ruge Mutahaba amefariki na kuacha watoto watano na wadogo zake wanne