Viongozi, taasisi za Serikali zaagizwa kutumia mtandao wa TTCL
- Agizo hilo limetolewa na Rais John Magufuli ambapo amesema kwa kufanya hivyo watakuwa wanaliimarisha shirika hilo la simu nchini.
- Amesikitika Ofisi ya Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kutotumia mtandao huo.
- Amemtaka bosi wa TTCL, Kindamba kumpa orodha ya Mawaziri na makatibu wakuu wanaotumia mtandao huo.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amewataka viongozi na taasisi za Serikali ambazo bado hazijaanza kutumia laini za mtandao wa simu wa TTCL kwa ajili ya mawasiliano waanze mara moja ili kuliimarisha hilo na kumuenzi baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Katika hotuba yake baada ya kupokea gawio Sh2.1 bilioni la Serikali leo (Mei 21, 2019) kutoka TTCL, Rais Magufuli amesema shirika ni nembo pekee ya kumkumbuka baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na linatakiwa kuimarishwa kwa taasisi za Serikali kutumia huduma zake katika shughuli zao za mawasiliano.
Amesema anasikitishwa na baadhi ya taasisi za Serikali ambazo bado hazijaanza kutumia mtandao wa TTCL ikiwemo Ofisi ya Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu ambazo zilipaswa kuwa kielelezo katika kuthamini na kutumia vitu vya ndani.
“Nilisikitika sana niliposikia hata Ofisi yangu ya Rais haikutajwa na nimesikitikika pia hata Chama changu cha Mapinduzi hakikutajwa. Dk Bashiru (Katibu Mkuu wa CCM) yuko hapa, ni mzalendo anampenda baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere lakini hapa hakutajwa.
“Sisi serikalini we are silent (tuko kimya), siyo Ofisi ya Waziri Mkuu, Siyo Ofisi ya Makamu wa Rais, siyo Ofisi ya Rais, siyo Wizara ya Fedha hata Wizara yako ya Uchukuzi haikutajwa hapa. Is a shame! (ni aibu),” amesema Rais Magufuli.
Baada ya maneno hayo, Rais Magufuli aliwatazama wafanyakazi wa TTCL waliokuwepo katika hafla hiya na kuwahoji afanye nini huku akibainisha kuwa amekuwa akizungumza maneno zaidi kuliko vitendo ikizingatiwa kuwa yeye mwenyewe anatumia laini ya TTCL.
Ameipa mwezi mmoja Ofisi ya Rais ambayo anayoiongoza kuanza kutumia mtandao wa TTCL kwa sababu amebaini wapo watu kwenye ofisi yake ambao wanapingana na maagizo anayoyatoa.
“Kwahiyo inaonekana wapinga wapinga hawa hata kwenye ofisi yangu wapo. Sasa kama wananisikia kama wapo hapa na huwa wamezoea kunisindikiza nataka kipindi cha mwezi mmoja, unajua kujipa amri mwenyewe ni shida lakini ngoja nijipe tu, tuanze kutumia simu za TTCL,” amesisitiza Rais Magufuli.
Rais John Magufuli akipokea Gawio la Serikali la Sh1.2 Bilioni 2.1 kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Waziri Kindamba huku akishuhudiwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Omar Nundu katika hafla fupi iliyofanyika katika makao makuu ya Shirika hilo jijini Dar es Salaam. Picha|Michuzi.
Amewaagiza viongozi wa Serikali wanaolipiwa vocha ya mawasiliano na Serikali nao watumie laini za TTCL na ikiwa kuna mfanyakazi anataka kutumia mtandao mwingine basi ajilipie kwa pesa yake.
Amebainisha kuwa lengo siyo kuwazuia watu kutumia laini za mitandao mingine lakini hatua hiyo inalenga kukiimarisha chombo hicho cha mawasiliano cha Serikali.
“Tusipowaimarisha hawa TTCL hawatafika popote, hiki ni chombo chetu, sijasema msiwe na laini zingine lakini kwani kuna ubaya gani Serikalini wakasema kuna watu wanalipiwa kwa simu, ukitaka kulipiwa simu ni TTCL ukitaka ya kujilipia nenda mitandao mingine ni hela yako,” amesema Rais Magufuli.
Inayohusiana: TTCL yatoa gawio la Sh1.2 bilioni kwa Serikali ikiendelea kusaka mtaji mkubwa
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amemuagiza Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya simu ya TTCL, Waziri Kindamba kumuorodhedhea namba za Mawaziri na Makatibu Wakuu wote wanaotumia mtandao wa TTCL ili baada ya mwezi mmoja aangalie viongozi wanaolipwa mshahara wa Serikali ambao hawana namba za TTCL.
Pia amemtaka Kindamba kufanya hivyo kwa wafanyakazi wa TTCL nchi nzima kuhakikisha wanatumia mtandao wa kampuni hiyo ambapo kwa kufanya hivyo itakuwa ni uzalendo na kujali vitu vya ndani.
Baadhi ya taasisi zinazotumia mtandao wa TTCL ambazo Rais amezitaja ni pamoja na Jeshi la Polisi Tanzania, Jeshi la Wananchi Tanzania na Jeshi la Zimamoto Tanzania.
Latest
