Vikundi vya ujasiriamali: Nguvu mpya ya kuwainua vijana vijijini
- Vijana wachangamkia fursa kwa kujiunga kwenye vikundi kuweza kupata ajira na kujikwamua kiuchumi.
- Mashirika ya umma na yasiyo ya Serikali yaombwa kuwakumbuka vijana waliopo vijijini ili kuwafungulia fursa za kiuchumi.
- Bado elimu ya ujasiriamali kwa vijana wa vijijini inawafikia wachache wenye uhitaji wa kujua.
Lindi. Mambo yamebadilika. Vijana wameamka na kuanza kutafuta mbinu mbalimbali za kujikwamua kiuchumi ikiwemo kuunda vikundi vya kusaidiana ili kushirikiana kwa pamoja kujipatia kipato kitakachoweza kuboresha maisha yao.
Zamani ilizoeleka kuona wanawake kuunda vikundi vya kusaidiana kiuchumi lakini kwa sasa hadi vijana wanafanya hivyo ili kupambana na changamoto za ukosefu wa ajira.
Vijana watano katika kijiji cha Mchinga 1 mkoani Lindi wameunda kikundi cha kusadiana maaarufu kama “Getto Boyz Workshop” ambao wamejikita katika ufundi seremala ikiwa ni sehemu ya muhimu ya kutengeneza fenicha mbalimbali wanazouza kwa watu wanaowazunguka.
“Tulianza rasmi kufanya kazi kama kikundi mwaka 2014, tulikuwa tuna ukosefu wa dhana za kisasa na mtaji wa kununua vifaa vyote vinahitaji pesa,” anasema Habibu Mponda, mmoja wa wana kikundi.
Hata hivyo vijana hao hawakukata tamaa na kuendelea na kazi yao, mpaka pale Mtandao wa Asasi za Kiraia Mkoa wa Lindi (LANGO) ulipowapa pesa ya kujiendeleza katika biashara yao.
Lakini hatima yao ya kutaka kusaidiana imepelekea kuweza kufanya kikundi chao kama uwanja wa mafunzo kwa vijana wanaopenda fani ya ufundi seremala ili kutoka kimaisha

Baadhi ya vijana wanaounda kikundi cha Getto Boys ambao ni wakazi wa kijiji cha Mchinga 1 mkoani Lindi, kutoka kushoto ni Mohamed Selemani, Habibu Mponda na Henrick Nakua ambao wamejipanga kujikwamua kiuchumi kwa kazi ya ufundi seremala. Picha| Zahara Tunda.
Mwalimu Hassan (18) anayeishi katika kijiji hicho cha Mchinga 1 ni mmoja wa vijana waliofaidika na mafunzo yanayotolewa na kikundi hicho baada ya kumaliza darasa la saba na kushindwa kuendelea na masomo ya kidato cha kwanza.
“Nilikuwa nipo tu, mtaani nilipomaliza darasa la saba, baba akanileta nijifunze ufundi, mpaka sasa nashukuru siombi hela nyumbani na najifunza vitu,” anasema Hassan.
Hassan anasimama kama mmoja wa vijana wachache ambao licha ya kukabiliwa na changamoto nyingi lakini amegundua siri ya kujiajiri na kuachana na dhana ya utegemezi inayowakumba vijana wengi nchini.
Mwanzilishi wa kikundi hicho, Henrick Nakua (34) ambaye anatumia muda wake mwingi kuwainua vijana wenzake kama Mwalimu tangu mwaka 2004, anasema kuwa kunahitajika juhudi za serikali na watu binafsi kuelimisha vijana wa kijijini umuhimu wa kuwa na vikundi vya ujasiriamali.
“Tangu tumekuwa na kikundi na kupata ufadhili wa pesa, tumepiga hatua sana, mwanzo ilikuwa unakuta kwa mwezi tunatengeneza milango mitano na vitanda viwili,” anasema Nakua.
Lakini Nakua anaiambia Nukta kuwa kwasasa biashara yao imekuwa vizuri na wanapata wastani wa milango 10 kwa mwezi na kumudu oda mbalimbali kwa wakati za meza, viti, vitanda na makabati.
Akitoa shukrani kwa mtandao wa LANGO kwa kuwasaidia na anaomba mashirika mengine kwenda vijijini kuwaamsha vijana ambao bado hawaoni fursa za kuungana na kufanya kazi kwa pamoja.
Zinazohusiana: Vijana waanika fursa zilizojificha katika matumizi ya mitandao ya kijamii
Mikakati inayoweza kuwasaidia vijana kuepuka ukosefu wa ajira
Mkurugenzi Mtendaji wa LANGO, Sharifu Maloya amesema kutokana na changamoto mbalimbali zilizopo vijijini, wamekuwa wakitoa elimu ya kujitambua na ujasiriamali ili kwa watu wa vijijini kujikwamua kiuchumi.
“Kabla ya kuwasaidia vijana wenye vikundi tunawapa elimu ya utunzaji fedha na kisha tunawapa Sh500,000 kwa ajili ya mtaji, kama tulivyofanya kwa Getto Boys,” ameeleza Maloya.
Lakini bado kuna changamoto kwa vijana wengine ambao hawana mpango wa kujishughulisha na hawana elimu kuhusu fursa zinazopatikana katika vikundi vya kijasiriamali.
“Sijawahi kusikia kuwa mkikaa vikundi kuna fursa ya kupewa mitaji,” anasema Samwel Mussa Mkazi wa kijiji cha Mto Mkavu, Lindi.
Ni wakati sasa kwa vijana kuchukua hatua ya kuanza kujikwamua wenyewe na kuacha kuwasubiri wanasiasa kuwatengenezea mstakabali wa maisha yao. Umoja na ushirikiano katika kutatua changamoto zinazowakabili ndiyo silaha muhimu ya kufika katika kilele cha mafanikio.