Vicoba rasmi ndani ya Sheria ya huduma ndogo za fedha, upatu waondolewa

November 17, 2018 3:00 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Vikundi vya kusaidiana maarufu kama “Upatu” havitasimamiwa chini ya Sheria hiyo kwa sababu havijihusishi na biashara ya huduma ndogo za fedha.
  • Kanuni na miongozo mahsusi kuandaliwa kwa ajili ya kusimamia daraja la nne la vikundi vya kifedha vya kijamii (VICOBA).
  • Sheria hiyo inalenga kuwalinda wananchi wanaotegemea sekta ndogo ya fedha katika kuendesha maisha yao na shughuli za kiuchumi kwa ujumla.

Dar es Salaam. Serikali imesema kuwa vikundi vya kusaidiana maarufu kama “Upatu” havitasimamiwa chini ya Sheria mpya ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018 kwa sababu havijihusishi na biashara ya huduma ndogo za fedha.

Sheria hiyo ambayo imepitishwa jana bungeni (Novemba 16, 2018) itahusisha taasisi kama vile Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS), Taasisi za huduma ndogo za fedha zisizopokea na zinazopokea amana na vikundi vya kifedha vya kijamii, wakopeshaji binafsi na asasi za kijamii.

Ufafanuzi huo umetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango wakati akihitimisha hoja za mjadala wa Muswada wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018 ambapo amesema Sheria hiyo inalenga kuwalinda wananchi wanaotegemea sekta ndogo ya fedha katika kuendesha maisha yao na shughuli za kiuchumi kwa ujumla.

Itasimamia na kudhibiti biashara ya huduma ndogo za fedha, kuwawezesha watumiaji na watoa huduma kudhibiti changamoto zinazoweza kutokea wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

“Madhumuni ya Sheria hiyo ni kuwatambua watoa huduma ndogo za fedha kwa lengo la kuwasimamia, kupata takwimu, kuwalinda na kuwawezesha watumiaji wa huduma ndogo za fedha,” amesema Mpango.

Sheria hiyo imeweka utaratibu wa kuiwezesha Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kutoa elimu kwa watumiaji wa huduma ndogo za fedha hususan vikundi vya kijamii kwa lengo la kunufaika na fursa zilizopo.

Amesisitiza kuwa wakati BOT itakapolazimika kusimamia taasisi za huduma ndogo za fedha, taasisi hizo hazitatozwa fedha kugharamia majukumu ya Benki Kuu.


Zinazohusina: 


Akizungumzia maoni ya wabunge kuhusu daraja la nne la Sheria hiyo linalohusu vikundi vya kifedha vya kijamii (VICOBA), wakopeshaji binafsi na asasi za kijamii, Mpango amesema kuwa zitaandaliwa kanuni na miongozo mahsusi kwa ajili ya kusimamia daraja hilo.

“Sheria hii inaainisha shughuli mbalimbali zinazoweza kufanywa na mabenki na taasisi za fedha zinazoweza kusaidia katika kulea na kukuza watoa huduma wa daraja la nne. Miongoni mwa shughuli hizo ni pamoja na utoaji mikopo yenye msharti nafuu na elimu ya fedha,” amesema Mpango.

Serikali imejipanga kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa usimamizi wa daraja la nne ambapo Mwongozo kwa ajili ya maandalizi ya bajeti ya 2019/20 umetoa maelekezo kwa Halmashauri zote kutenga fedha kwa ajili ya kazi hiyo.

Bunge limepitisha muswada wa Sheria hiyo ambao umeundwa baada ya kujitokeza changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ndogo ya fedha ikiwemo taasisi za huduma ndogo za fedha kutoa mikopo kwa wananchi kwa vigezo na masharti magumu na hivyo kusababisha madhara kwa wananchi ikiwemo mali zao kuuzwa pasipo kufuata taratibu za kisheria.

Enable Notifications OK No thanks