Usafiri, ubora wa bidhaa: Vizuizi ukuaji biashara mtandaoni Tanzania

August 23, 2018 8:55 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Sababu za bidhaa kuchelewa kumfikia mteja hutegemea  na eneo analoishi, gharama za usafiri, upatikanaji wa bidhaa na muda alioagiza.
  • Kampuni nyingi zinazotoa huduma ya biashara mtandaoni ni kiungo cha wafanyabiashara na wanunuzi wa bidhaa.
  • Ubora wa bidhaa na mfumo wa malipo ni changamoto nyingine inayohitaji ufumbuzi wa kudumu.

Dar es Salaam. Biashara ya mtandaoni ni mapinduzi ya teknolojia ambayo yanawazesha watu kununua bidhaa wakiwa nyumbani, hakuna haja ya kusafiri mpaka dukani kutafuta bidhaa unayoitaka, bidhaa inakufikia popote ulipo.  

Lakini kama zilivyo huduma nyingine, biashara ya mtandaoni ina changamoto zake ambazo zimekuwepo kwa muda mrefu ambapo hutofautiana kulingana na maeneo biashara hiyo inakofanyika ikiwemo ucheleweshaji wa kufikisha bidhaa kwa wateja.

Tanzania kama zilivyo nchi zingine za Afrika zimeanza kuipokea teknolojia hiyo lakini  bado kuna mambo muhimu yanayopaswa kuwekwa sawa kuifanya huduma hiyo kuwa na mwitikio mkubwa wa watu nchini.


Usafiri na usambazaji

Ujio wa biashara ya mtandaoni unadhaniwa kuwa ni suluhisho la kuokoa muda ambao mtu anatumia kwenda dukani lakini kwa baadhi ya bidhaa huchukua muda mrefu kumfikia mteja kutokana na ufanisi wa biashara yenyewe.

Nukta imebaini kuwa ili bidhaa iimfikie mteja huchukua kati ya siku moja hadi saba, tofauti na mtu kwenda kununua bidhaa dukani moja kwa moja na huipata siku hiyo hiyo. 

Hata hivyo, kampuni zinazotoa huduma hapa nchini zinabainisha kuwa mfumo wa uagizaji wa bidhaa mtandaoni ni tofauti na biashara zingine kwasababu hupitia mchakato mrefu ambao unatakiwa kuzingatiwa ili bidhaa isafirishwe na kumfikia mteja ikiwa salama na kwa wakati unaofaa.  

Kwa mujibu wa sera ya usafirishaji ya duka la mtandaoni la Zudua ambalo linaendesha shughuli zake nchini, mchakato wa kusafirisha bidhaa hadi kwa mteja huanza pale anapokuwa amekamilisha taratibu zote za kuagiza bidhaa ambapo hutofautiana kulingana na taratibu za usafirishaji, eneo analoishi mteja, njia ya kusafirisha na bidhaa iliyonunuliwa. 

“Muda wa kusambaza unatumika kama mwongozo tu na unategemea kukubalika na kupitishwa kwa bidhaa iliyoagizwa. Isipokuwa kama kuna hali isiyozuilika, tunafanya kila jitihada kutekeleza oda yako ndani ya siku saba tangu ulipoagiza bidhaa,” inaeleza sehemu ya sera ya Zudua.

Mchakato wa bidhaa kumfikia mteja aliyeagiza mtandaoni bado ni mrefu kwa nchi za Afrika kutokana na changamoto ya mipango miji. Picha| gstatic.com.

Pia kuchelewa kwa bidhaa kumfikia mteja kunategemea upatikanaji wa bidhaa husika dukani katika muda ambao mteja ameagiza bidhaa hiyo.

Kampuni nyingi zinazofanya biashara ya mtandaoni zinasimama kama kiunganishi cha wauzaji na wanunuzi wa bidhaa. Mawasiliano na taratibu za kuandaa bidhaa zinatakiwa zifuatwe kulingana na miongozo ya Serikali ya kusafirisha bidhaa. 

Mpangilio wa makazi nayo ni changamoto nyingine inayochelewesha bidhaa kufika kwa wakati ni ujenzi wa makazi usiozingatia mipango miji. Mathalani, maeneo mengi ya jiji la Dar es Salaam, makazi ya watu hayana mitaa na barabara zinazoweza kutambulika na kupitika kirahisi.

“Bidhaa zinazotolewa kwenye tovuti yetu zinasambazwa kwenye maeneo yenye anuani Tanzania,” inaeleza sera ya Zudua ikiwa ni njia ya kuepuka usumbufu wa kumfikishia bidhaa mteja ambaye anaishi maeneo yasiyo na anuani. 


Kwa wengine ni fursa…

Katika kuhakikisha wanamfikia kila mteja popote alipo bila kujali eneo analoishi, kampuni ya biashara mtandaoni ya Jumia Tanzania  wanatumia mawakala wenye uzoefu wa maeneo mbalimbali ambao humfikishia mteja bidhaa hadi mlangoni kwa kutumia mawasiliano ya simu na barua pepe.

“Timu ya operesheni na huduma kwa wateja inafanya kazi kwa umakini na ufanisi kuhakikisha bidhaa zinazopelekwa ndizo zilizoagiwa, zoezi hili limerahisishwa kupitia mawakala wa Jumia ambao humfikishia mteja bidhaa mpaka mlangoni kwake,” anaeleza Meneja Uhisiano wa Jumia Tanzania, Godfrey Kijanga. 

Licha ya mteja kufikishiwa bidhaa mahali alipo, analazimika kulipa gharama za usafiri kulingana na aina ya mzigo alioagiza.

Kutokana na changamoto za usafirishaji wa bidhaa zinazonunuliwa mtandaoni, wataalamu wa usalama mtandaoni wanashauri watumiaji wa mifumo hiyo ya manunuzi kutathmini bei ya bidhaa, gharama za usafiri kabla hawajafanya uamuzi ili kuepuka usumbufu wa kurudisha bidhaa kama hawajaridhika nayo.

Kulingana na Shirika la Ulinzi la walaji la British Columbia la nchini UIngereza linaeleza kuwa ikiwa mteja hajapata bidhaa kwa wakati anaweza kusitisha oda yake na kampuni husika inatakiwa kumlipa fidia kutokana na usumbufu alioupata.

Miamala ya fedha kwa njia simu inaweza kuharakisha ukuaji wa biashara mtandaoni nchini. Picha| sampi.co

Ubora wa bidhaa na uelewa mdogo wa watumiaji wa mfumo wa malipo kwa njia ya mtandao ni changamoto nyingine inayokwamisha ukuaji wa biashara ya mtandaoni nchini. Nukta inatambua kuwa baadhi ya malipo ya bidhaa iliyoagizwa mtandaoni hufanyika baada kumfikia mteja jambo linaloweza kuhatarisha usalama wa mnunuzi hasa kama ana kiasi kikubwa cha fedha. 

Kijanga wa Jumia Tanzania anabainisha kuwa wanaendele kutafuta suluhisho la changamoto zote ikiwa ni pamoja na malipo kufanyika kupitia simu za mkononi au benki ili kuepuka usumbufu wa kubeba pesa mkononi. 

“Kwa sasa malipo yanafanyika kwa njia mbili, ya kwanza ni pesa taslimu mara baada ya mteja kufikiwa na bidhaa, hii ni kutokana na changamoto ya Watanzania wengi kuwa wageni na mfumo huu mpya wa biashara pamoja na kuepuka wizi wa mitandaoni.”

“Njia ya pili ni kupitia Tigo Pesa, Tigo ni miongoni mwa washirika wa Jumia kwa upande wa malipo ya njia ya simu. Lakini ili kutoa fursa kwa wateja wengine ambao wanaweza kulipia kwa njia nyingine, hivi karibuni Jumia itazindua malipo kwa njia ya kadi za benki.”  

Hata hivyo, biashara ya mtandaoni haiwezi kuzuiwa na changamoto zilizopo, itaendelea kukua na kukubalika ikizingatiwa kuwa kila teknolojia ina changamoto zake zinazoweza kupatia ufumbuzi wa kudumu. 

Enable Notifications OK No thanks