Unavyoweza kuboresha ufanisi wa ‘Smart TV’
- Ni kwa kufuta kache ili kuipa TV nafasi ya kutosha kuchakata maudhui na kuwezesha Programu kufanya kazi kifanisi.
Dar es Salaam. Televisheni janja ndiyo habari ya mjini kwa sasa, ikiwawezesha watumiaji kujiburudisha kwa kutazama vipindi, muziki na kuperuzi mtandaoni kwa kutumia intaneti.
Kwa wasiofahamu televisheni janja au ‘Smart tv’ ni runinga yenye uwezo wa kuunganishwa na mtandao wa intaneti na ina programu (Apps) zilizowekwa ndani yake, kama vile Netflix, YouTube, na huduma nyingine za mtandaoni. Runinga hii hufanya kazi kama simu janja ambazo kwa sasa zinaongoza zaidi kutumia intaneti nchini.
Licha ya umuhimu wake watumiaji wengi hukutana na tatizo la kifaa hicho kupungua kasi, kukwama kwama na kupunguza utendaji kazi wake kunakosababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo kujaa au kukithiri kwa kache (cache).
Kwa mujibu wa kamusi ya Kiswahili, kache ni mkusanyiko wa vitu vya aina moja vinavyohifadhiwa sehemu isiyofikika kwa ajili ya matumizi ya baadae.
Unaweza kusema kache ni kumbukumbu inayotunzwa kwa muda mfupi ambayo hufanya programu na maudhui unayotumia au kuangalia mara kwa mara kufunguka haraka.
Kadri unavyozidi kutumia TV sehemu ya kuhifadhi kache hujaa data zisizohitajika na kusababisha changamoto kama kupunguza kasi ya mfumo wake au kushindwa kuonesha vizuri vipindi unavyopenda.
Wataalamu wa teknolojia kutoka tovuti ya ZDNET ya Japan, wanashauri hatua muhimu na rahisi ya kufuta kache mara kwa mara ili kuhakikisha televisheni inafanya kazi kwa ufanisi.
Jinsi ya kufuta kache
Mchakato wa kufuta kache hutegemea chapa na aina ya TV janja unayotumia, baadhi ya chapa hutofautiana na nyingine lakini zote ni lazima ziwe na kipingele hicho muhimu.
Kwa wanaotumia TV za Samsung, anza kuiwasha kisha bonyeza menyu na uende sehemu ya mipangilio (settings) kisha usaidizi (support) alafu utunzaji wa kifaa (Device Care).
‘Screenshots’ zikionesha hatua za kufuata ili kufuta kache kwenye TV janja ya Samsung toleo la 2020 na kuendelea. Picha |Davis Matambo.
Ukifika katika hatua hiyo chagua kipengele cha ‘amuru hifadhi’ (manage storage) kisha uchague programu unayotaka kufuta kache yake na bofya tazama maelezo (view details), baada ya hapo bonyeza futa kache (clear cache) na utakuwa umetatua tatizo hilo.
Aidha, watumiaji wa TV za LG, baada ya kuiwasha wanaweza kubonyeza kitufe cha ‘home’ kwenye rimoti, kisha kwenda kwenye mipangilio (settings) ikifuatiwa na kipengele cha jumla (general) alafu, hifadhi (storage).
Malizia mchakato huo kwa kuchagua futa kache (clear cache) na utakuwa umeongeza ufanisi wa Tv tako.
Kwa Android/Google TV kama za Hisense na Sony nenda kwenye mipangilio (settings) kisha, programu (Apps). Chagua tazama programu zote (see all apps).
Baada ya hapo chagua programu unayotaka kufuta kache yake, malizia kwa kubofya futa kache (clear cache).
Ikiwa Tv yako haipo kwenye orodha hiyo hapo juu, hakikisha unasoma mwongozo wa mtumiaji wa TV husika ili kufuata maelekezo maalum, kwasababu, mchakato wa kufuta kache unaweza kutofautiana kati ya chapa mbalimbali na hata kati ya matoleo ya chapa moja.
Ni muhimu kuzingatia kuwa baadhi ya TV zinaruhusu kufuta kache za programu moja moja badala ya mfumo mzima, na pia kufuta kache kwa kawaida ni salama na hakuondoi data muhimu tofauti na kufuta data za programu ambapo husababisha kupoteza mipangilio au maelezo ya ku-log in.
Faida za kufuta kache
Mbali na kuongeza ufanisi wa TV janja kufuta kache kunaongeza usalama wa faragha kwa kufuta taarifa binafsi, kama vile nambari za akaunti au historia ya kivinjari (browser history).
Pia kufuta kache mara kwa mara kunaweza kutatua matatizo ya programu kama Netflix au Premier zinaposhindwa kufanya kazi au kutofunguka ipasavyo.
Ni vyema kufuta kache kila baada ya miezi michache au unapoona dalili kama TV kupungua kasi ya utendaji kazi wake, kutokufunguka kwa baadhi ya programutumizi kama Netflix au Amazon Premier ‘Apps’ na kupungua kwa nafasi ‘storage’.