UN Environment yaanza kutumia tovuti, mitandao ya kijamii ya Kiswahili
- Shirika hilo la mazingira duniani limezindua tovuti mpya na mitandao ya kijamii kwa lugha ya Kiswahili.
- Lengo ni kuwafikia mamilioni ya wazungumzaji wa lugha hiyo kote duniani.
- Jumuiya ya Afrika Mashariki nayo iko mbioni kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi.
Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikijipanga kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya Afrika Mashariki, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UN Environment) limezindua tovuti mpya na mitandao ya kijamii kwa lugha ya Kiswahili ili kuwafikia mamilioni ya wazungumzaji wa lugha hiyo kote duniani.
Mpango huo wa Tanzania ulitangazwa jana (Septemba 12, 2019) na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dak Harrison Mwakyembe ambaye amesema tayari Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) limepitisha Kiswahili kuwa lugha rasmi.
Amesema kinachosubiriwa ni baraka za wakuu wa nchi wa jumuiya hiyo yenye nchi wanachama za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.
Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa nalo jana limezindua tovuti mpya na mitandao ya kijamii kwa lugha ya Kiswahili, ikiwa ni hatua ya kuikuza lugha hiyo yenye wazungumzaji zaidi ya milioni 150 duniani.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Joyce Msuya amesema lengo ni kuwafikia mamilioni ya wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili kote duniani, kwani tovuti hiyo ya Kiswahili na mitandao ya kijamii vitatoa taarifa za mazingira, takwimu muhimu na kuelezea hadithi zitakazowahamasisha watu wanaofanya kazi kuboresha mazingira ya dunia.
“Tovuti hiyo pia itaeleza kuhusu mada muhimu zihusuzo matatizo ya mabadiliko ya tabianchi, bayoanuai, suluhu za kiasili, uchaguzi wa hali ya hewa na mengine mengi,” inaeleza taarifa ya Msuya iliyotolewa jana.
Soma zaidi:
- Kiswahili ndiyo mpango mzima wa kusaka wateja Tanzania: Ripoti
- Wageni kufunzwa Kiswahili katika Chuo cha Diplomasia
- Kiswahili chapendekezwa kuwa lugha rasmi ya SADC
Uzinduzi wa tovuti hiyo mpya ya Kiswahili na mitandao ya kijamii umefanyika siku chache kabla ya mkutano wa Umoja wa Mataifa wa kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ambao utafanyika jijini New York, Marekani Septemba 23 mwaka huu.
Shirika la UN Environment limekuwa ni sauti inayoongoza duniani katika masuala ya mazingira. Linatoa muongozo na kuchagiza wadau kulinda mazingira, kuhabarisha na kuyawezesha mataifa na watu kuboresha hadhi ya maisha yao bila kuweka rehani mustakabali wa dunia na vizazi vijavyo kimazingira.
Katika kufanikisha azma hiyo, UN Environment inafanya kazi kwa karibu na wadau wote zikiwemo Serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia, mashirika ya kimataifa na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa kote duniani.