Ukweli kuhusu video ya utekaji watoto Dar es Salaam

July 26, 2024 4:36 am · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni video ya tukio la kweli lililotokea mwaka 2022.
  • Tukio hilo lilitokea eneo la Bongoni katika mpaka wa Buguruni na Ilala, Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Hivi karibuni kumekuwa na taharuki katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania kutokana na matukio ya kuteka au kujaribu kuteka watoto yaliyoripotiwa kutokea.

Mathalani Julai 22,2024  baadhi ya wazazi na walezi wa watoto wanaosoma katika shule ya msingi Bryson iliyopo Mburahati Dar es Salaam walilazimika kufika katika shule hiyo kwa lengo la kuwachukua watoto wao baada ya kusambaa kwa taarifa za uwepo wa gari aina ya Noah inayosadikiwa kuwachukua wanafunzi wawili taarifa ambazo baadae zilibainika kuwa si za kweli.

Kutokana na uwepo wa matukio hayo baadhi ya watu wenye nia ovu wametumia muanya huo kusambaza taarifa za uzushi zinazohusiana na matukio ya kutekwa kwa watoto jambo linalochochea taharuki na kuondoa amani katika jamiii.

Kuanzia Julai 24 hadi 25, 2024 katika mitandao ya kijamii hususan WhatsApp na X (zamani Twitter) kumekuwa na video fupi inayosambaa ikimuonesha kijana mwenye umri wa miaka 16 aliyekamatwa akijaribu kuiba mtoto. Tukio hilo ingawa ni la kweli, lilitokea mwaka 2022.

Video hiyo inayosambaa bila maelezo yoyote zaidi, inaonesha kijana huyo akisema jina lake ni Frank mwenye umri wa miaka 16 kutoka Buguruni, akieleza kuwa alishirikiana na vijana wenzake waliowataja kwa majina ya Juma na Marinda.

Ukweli Halisi

Uchunguzi uliofanywa na Nukta Fakti umebaini kuwa tukio hilo lilitokea katika maeneo ya Ilala jijini Dar es Salaam takribani miaka miwili iliyopita na liliripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari vya hapa Tanzania. 

Mathalani, Azam TV kupitia chaneli yake ya YouTube ilichapisha habari hiyo Julai 23, 2022, ikiwa na kichwa cha habari ‘Mwizi wa watoto akamatwa Ilala Shariff Shamba akiiba mtoto.’ Katika habari hiyo, wananchi mbalimbali walihojiwa kuhusu tukio hilo.

Habari hiyo ilieleza namna kijana huyo alivyotaka kumuiba mtoto huyo hadi alivyokamatwa na kupelekwa kwenye kituo cha polisi pia, video hiyo ilieleza kuwa Kituo cha Polisi cha Pangani Ilala kilithibitisha kuwashikilia watuhumiwa hao.

Aidha leo Julai 25, 2024 Jeshi la Polisi Tanzania kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter) lilitoa taarifa ya kukanusha tukio hilo likisema, ‘Video hii ni ya Mwaka 2022. Ipuuzeni.

Ushahidi mwingine unaonesha kuwa video hiyo sio ya mwaka 2024 bali ni ya mwaka 2022 na unaweza kuipata kwenye Google au YouTube kwa kuandika maneno ‘Mwizi wa watoto akamatwa Ilala Shariff Shamba akiiba mtoto.

Bonyeza hapa kuona video hiyo ni ya mwaka gani

Nukta Fakti inaendelea kuiasa jamii kuwa makini na taarifa zinazopatikana kwenye mitandao ya kijamii na kufanya uhakiki wa habari kabla ya kuziamini na kuzisambaza.

Enable Notifications OK No thanks