Ukosefu wa takwimu sahihi unavyotishia ubora wa maji Tanzania

November 3, 2021 12:01 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link

Mkurugenzi Mtendaji Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, Renatus Shinhu akizungumza kwenye mafunzo ya siku mbili kuwajengea uwezo wasoma vipimo vya maji, wasoma vipomo hao wametoka bodi ya maji bonde la Ziwa Victoria na Tanganyika. Picha|Mariam John.


  • Inatokana na changamoto za wasoma vipimo vya maji.
  • Ukosefu wa ulinzi wa miundombinu ya maji wachangia pia.
  • Serikali kuwapiga msasa wwasoma vipimo.

Mwanza. Ukosefu wa takwimu sahihi za maji kwenye  vyanzo vya maji umetajwa kuwa sababu ya kukosekana kwa majibu yaliyo sahihi ya upatikanaji wa maji yaliyopo kwenye mito na mabwawa ncini Tanzania.

Kutokana na changamoto hiyo, Bodi ya Maji bonde la Ziwa Victoria imeendesha mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo na uelewa wa pamoja wa wasoma vipimo 30 kutoka bodi hiyo na ile ya Ziwa Tanganyika ili kutatua changamoto zilizokuwa zinawakabili wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Maji bonde la Ziwa Victoria, Renatus Shihnu akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo leo Novemba 3, 2021 amesema wasoma mita ni watu muhimu katika suala la rasilimali maji ambacho ni kichocheo cha maendeleo endelevu na kukuza uchumi wa nchi.

“Tunatarajia baada ya mafunzo haya wasoma mita watakuwa na uelewa wa pamoja katika kusoma vipimo na kuleta takwimu bora na si bora takwimu lakini pia watasaidia katika kuonyesha ubora wa maji kwenye mito na mabwawa,” amesema Shinhu.

Mkurugenzi huyo amesema mafunzo hayo pia yatawajengea uwezo wa kuwa walinzi kwenye vyanzo vya maji ili kulinda miundombinu isiharibiwe hususan vifaa vya kusomea takwimu ikiwemo mita.

“Kwenye vyanzo vya maji tunafunga vifaa vya kusomea maji na  vipimo vingine ambavyo visipolindwa vinaweza kuharibiwa na wakulima ambao hujishughulisha na shughuli za kilimo kando ya mito au wafugaji,” amesema.

Aidha, wananchi wametakiwa kutokufanya shughuli yoyote ya kilimo na ufugaji kando ya vyanzo vya maji ili kulinda na kutunza vyanzo hivyo visikauke kutokana na kuwepo kwa mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukame.

Amesema kufanya shughuli hizo kwenye vyanzo vya maji kunasababisha mchanga kuingia kwenye njia za maji hivyo kusababisha maji kutoonekana.

“Tunatoa wito kwa wananchi wasiendeleze shughuli za kilimo na ufugaji kwenye vyanzo vya maji na shughuli hizo ni vema zifanyike nje ya mita 60 ili kulinda na kuhifadhi mazingira,” amesema Shinu.

Mhandisi wa Rasilimali Maji bonde la Ziwa Tanganyika, Jastine Kamile amesema katika mafunzo hayo washiriki watafundishwa namna ya kusoma vipimo ili kupata takwimu zilizosahihi zitakazowasaidia katika kazi zao za kila siku.

Hata hivyo, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, Kleopa Kisovu amesema wanaimani baada ya mafunzo hayo watahakikisha wanafahamu namna ya kusoma takwimu na kuziwasilisha serikalini kwa ajili ya matumizi yao.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW