Ukarabati wa shule kongwe ya Pugu waibua maswali ushirikishwaji, uwajibikaji wa miradi
- Baada ya viongozi wa wilaya, mkoa na shule kutokujua juu ya mkataba wa ukarabati wa shule hiyo.
- Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imesema kila kitu kipo wazi kwasababu wadau wote walishirikishwa tangu hatua za awali.
- Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji aahidi kulishughulikia jambo hilo.
Dar es Salaam. Kuna kila dalili ya mkanganyiko wa mawasiliano na ushirikishwaji katika ukarabati wa shule kongwe jijini Dar es Salaam baada ya uongozi wa Manispaa ya Ilala kukosa majibu juu ya ukarabati wa shule ya sekondari ya Pugu.
Sintofahamu hiyo imemlazimu Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji kuahirisha ukaguzi wa ukarabati wa shule kongwe ya sekondari Pugu jana (Februari 19, 2019) baada ya viongozi wa manispaa kushindwa kueleza kwa kina mradi huo unaotekelezwa na Serikali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa wanahabari, viongozi wa Mkoa, Manispaa ya Ilala na shule hiyo walieleza kuwa hawajui lolote kuhusu ukarabati huo unaogharimu zaidi ya Sh1 bilioni kwa madai kuwa hawajashirikishwa.
Mradi huo wa ukarabati wa shule hizo kongwe unatekelezwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) chini ya ukandarasi wa Shirika la Nyumba Tanzania (NHC) ambapo Pugu ni moja kati ya shule kongwe sita zilizopo Dar es Salaam zilizobahatika katika mchakato wa maboresho ya shule.
Hata hivyo, TEA imeiambia Nukta jambo tofauti ikibainisha kuwa tuhuma hizo za viongozi hao kutokushirikishwa si za kweli kwa sababu mchakato wote wa mradi ulikuwa shirikishi na mhusika mkuu alikuwa ni mhandisi wa Manispaa ya Ilala.
Kauli hiyo ya TEA, inayosimamia ukarabati wa shule kongwe nchini inaibua maswali lukuki juu ya mfumo wa ushirikishwaji na uwajibikaji katika utekelezaji wa mradi wa ukarabati wa shule hizo kongwe nchini.
Afisa Mipango wa Manispaa ya Ilala, Ando Mwankuga akieleza kutokuwa na taarifa ya utekelezaji wa maboresho ya shule kongwe ya sekondari ya Pugu baada ya Naibu Waziri wa Fedha, Dk Ashatu Kijaji kukataa kukagua ukarabati wa shule hiyo kongwe jana (Februari 19, 2019). Picha|Benny Mwaipaja.
Katika taarifa hiyo ya Wizara ya Fedha na Mipango, iliyotumwa na msemaji wake Ben Mwaipaja, Afisa Mipango Manispaa ya Ilala, Ando Mwankuga amesema mradi wa ukarabati wa shule ya Pugu umekuwa na changamoto kubwa kwa sababu hawajawahi kuona mkataba wake kuanzia mkoani hadi Manispaa ya Ilala pamoja na uongozi wa shule.
“Hatujui umegharimu kiasi gani na ni vitu gani viko kwenye mkataba huo jambo linalotuwia vigumu kuuelezea,” amesema Mwankuga.
Mwankuga ameeleza kuwa yeye ndiye mwenye taarifa ya miradi yote inayotekelezwa katika ngazi ya Manispaa ambayo kwa mujibu wa taratibu na kanuni hupitishwa kwenye vikao mbalimbali ikiwemo Kamati ya Ushauri ya Manispaa na Baraza la Madiwani na kuwa mradi huo wa ukarabati wa shule ya sekondari Pugu haujawahi kujadiliwa.
Zinazohusiana:
- Mbinu zitakazowasaidia watahiniwa darasa la saba kufanya vizuri.
- Mbinu zinazoweza kuisaidia Temeke kutokomeza sifuri elimu ya sekondari.
- Udanganyifu mitihani darasa la saba kujirudia tena mwaka huu?.
Ukiachana na kigogo huyo wa manispaa, hata mkuu wa shule naye amedai hana taarifa za msingi za ukarabati huo unaofanywa shuleni kwake jambo linaloibua pia maswali iwapo anajua kikamilifu kinachoendelea ama la.
Mkuu wa shule ya sekondari Pugu, Jovenus Mutabuzi alipoulizwa na Dk Kijaji ameeleza kuwa taarifa alizonazo ni za kuambiwa kwamba mradi huo umegharimu zaidi ya Sh900 milioni.
Alieleza kuwa hajawahi kushirikishwa kikamilifu kuhusu ukarabati huo na yeye amekuwa akiwaona mafundi kutoka NHC wakiingia kufanya kazi na kutoka shuleni hapo.
“Mimi naona tatizo kubwa hapa ni mawasiliano hafifu kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mamlaka ya Elimu Tanzania na Halmashauri Manispaa ya Ilala, ndio maana haya yote yamejitokeza,” amenukuliwa Mutabuzi katika taarifa hiyo.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji akisalimiana na kiongozi wa wanafunzi wa shule kongwe ya sekondari ya Pugu, Ramadhani Hamis, alipotembelea na kukagua maboresho ya Shule hiyo iliyopo Manispaa ya Ilala Jijini Dar es Salaam kabla ya kugundua sintofahamu iliyokuwepo katika ukarabati wa majengo ya shule hiyo.Picha|Benny Mwaipaja.
Uongozi wa TEA umeiambia Nukta kuwa Manispaa ya Ilala ilishirikishwa baada ya mchakato huo kuletwa kutoka Ofisi ya Rais-Tamisemi huku mkurugenzi akimtuma afisa wa elimu wa sekondari kwenda kumuwakilisha katika makabidhiano ya awali.
“Hatuwezi kufanya kazi bila kuwashirikisha nadhani mhusika hakuwepo kipindi wanaulizwa na ndio maana kumeibuka sintofahamu hiyo,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania, Bahati Geuzye.
Geuzye amesema mpaka sasa kila kitu kuhusu marekebisho hayo kipo wazi labda kama manispaa imeshindwa kujieleza kutokana na kutokuwepo kwa msimamizi kutoka manispaa ambaye ni mhandisi wa wilaya hiyo.
Katika ziara hiyo, Dk Kijaji aliamua kusitisha ukaguzi huo na kuahidi kulifanyia kazi suala hilo kutokana na wahusika kutojua mhusika ya ukarabati huo kuendelea katika shule hiyo.
“Kama hali ndiyo iko hivi! kila kiongozi hapa kuanzia mkoa, Manispaa hadi uongozi wa Shule mmeukana mradi huu kwamba hamuujui, wakati Mwalimu wa Takwimu wa Manispaa anasema anaufahamu pia juujuu, sasa mimi nitakagua nini? Tuondoke!,” amesema Dk Kijaji.
Wizara ya fedha inaeleza kuwa Serikali tayari imeshatoa zaidi ya Sh42 bilioni kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya sekondari 42 kati ya shule 88 kongwe zilizopo nchini kote
Latest