Ujio mfumo wa taifa wa hali ya hewa kuchochea ujenzi wa viwanda nchini

August 25, 2018 11:02 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Utatekelezwa katika kipindi cha miaka saba kuanzia mwaka huu.
  • Utaboresha miundombinu na taarifa za hali ya hewa nchini.
  • Kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Kutoka kushoto ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye; Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Maafa, Prof. Fautin Kamuzora; Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Antony Mavunde na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), Dk Agnes Kijazi wakati wa uzinduzi wa Mfumo wa Taifa wa Huduma za Hali ya Hewa (NFCS) uliofanyika hivi karibuni.

Dar es Salaam. Serikali imezindua Mfumo wa Taifa wa Huduma za Hali ya Hewa (NFCS) unaolenga kuimarisha upatikanaji na matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa zitakazochochea maendeleo nchini.

Akizindua mfumo huo jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu, Antony Mavunde amesema  NTCS  itasaidia katika mipango ya Serikali ambayo utekelezaji wake unategemea muunganiko wa sekta mbalimbali. 

Mavunde amesema ikiwa taarifa zinazotolewa na mfumo huo zitatumiwa vizuri zitaisadia pia Tanzania katika mchakato wa ujenzi wa viwanda na kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025. 

“Ni dhahiri kuwa maandalizi ya mfumo huu yasingewezekana bila msaada wa Shirika la Hali ya Hewa duniani (WTO). Tunathamini taarifa za hali ya hewa hasa katika mchakato wa ujenzi wa uchumi wa viwanda,” amesema Mavunde. 

Mfumo wa NFCS umeandaliwa na wataalamu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi kwa kushirikiana na WTO inazitaka nchi wanachama kutengeneza na kutekeleza kikamilifu mfumo NFCS ikiwa ni mkakati wa kudhibiti athari za mabadiliko ya hali ya hewa duniani. 

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Agnes Kijazi amesema mfumo huo utasaidia kuongeza upatikanaji na matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika shughuli za sekta mbalimbali ikiwemo kilimo ambacho kwa kiasi kikubwa kinaathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa. 

Amebainisha kuwa mfumo huo unalenga kuboresha na kuimarisha utendaji wa miundombinu ya hali ya hewa iliyopo nchini ili kuhakikisha taarifa zilizotolewa zinakuwa sahihi kuwasaidia wadau wa maendeleo kufanya maamuzi katika maeneo yao 

“Hii itachangia sana kuboresha usalama wa chakula, kujiandaa na kupunguza athari za majanga,” amesema Dk Kijazi. 

NFCS itatekelezwa kwa miaka saba kuanzia mwaka huu (2018-2025) ambapo utahusisha shughuli mbalimbali ikiwemo tathmini ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa nchini  na njia sahihi za kukabiliana nayo.

Naye Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amesema wizara yake ni mtumiaji mkubwa wa taarifa za hali ya hewa hasa katika sekta ya ujenzi, “Huko tunakokwenda taarifa za hali ya hewa zitakuwa muhimu sana hata ujenzi wa reli ya kisasa unategemea hali ya hewa.” 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa WTO, Prof. Petteri Taalas amesema wataendelea kutoa ushirikiano kwa serikali ya Tanzania kwa kutoa mafunzo kwa watendaji na rasilimali fedha ili kuhakikisha mfumo wa NTCS unakuwa endelevu na unaleta matokeo chanya kwenye uchumi wa nchi. 

Enable Notifications OK No thanks