Uhaba, uchafu wa vyoo unavyohatarisha afya za wanafunzi Kyela
- Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa kama mazingira ya choo siyo safi na salama, uwezekano wa wanafunzi kukumbwa na magonjwa ya maambukizi ikiwemo kuhara ni mkubwa.
Kyela. “Mimi situmii vyoo vya hapa shuleni, huwa navumilia mpaka nirudi nyumbani, naogopa kupata magonjwa hasa UTI.”
Hayo ni maneno ya Luciana, mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Uhuru iliyopo Kata ya Mwanyanganya wilayani Kyela ambaye analazimika kurudi nyumbani wakati vipindi vya masomo vikiendelea darasani ili kufuata huduma ya choo.
“Nasema hivyo kwa sababu watu wakienda hamna maji wanajisaidia hivyo hivyo kinyesi wanakiacha. Sisi tunapoenda kudeki tunakutana na harufi kali,” anasema Luciana.
Hali hiyo ndiyo iliyomfanya Luciana (jina sio halisi) kuacha kutumia vyoo vya shule kwa kuogopa kupata maambukizi ya magonjwa na wakati mwingine hujizuia mpaka vipindi viishe, ndipo hukimbilia choo cha nyumbani chenye maji.
“Najizuia kutokwenda kukojoa chooni, naenda nyumbani. Japo nyumbani ni mbali kidogo lakini ni lazima ufanye hivyo kwa sababu mazingira ni machafu, najikaza nikitoka saa sita naenda nyumbani,” Luciana anamwambia Mwandishi wetu aliyekuwa ameitembelea shule hiyo katikati mwa Mei mwaka huu.
Luciana ni sehemu ya wanafunzi wengi wa shule za msingi wilayani Kyela katika Mkoa wa Mbeya ambao wanakosa huduma muhimu ya maji na vifaa vya usafi vyooni, jambo linalohatarisha afya na uelewa wa masomo darasani.
Shule ya Uhuru iliyoanzishwa mwaka 2013 ina kisima cha maji lakini hakijaunganishwa na mfumo wa kusambaza maji kwenye choo cha wanafunzi. Wanafunzi hulazimika kubeba vidumu vya maji toka nyumbani kwa ajili ya matumizi ya chooni.
Jambo lingine ambalo limekuwa likitishia afya na usalama wa watoto wa kike kama Luciana ni kukosekana kwa vifaa vya usafi kama ndoo za maji, sabuni na milango kwenye vyoo hivyo.
Usiri katika vyoo hivyo haupo kwasababu viko jirani na makazi ya watu ambapo wapita njia hushuhudia kinachoendelea kwenye vyoo hivyo jambo linalowapa ugumu kujisitiri wakiwa kwenye siku zao.
“Mazingira ya chooni siyo mazuri sana, chooni ukitoka unatakiwa unawe maji safi na sabuni. Kisima kipo lakini hamna vyombo vya kuwekea,” anasema Radhaki Abdallah (12), mwanafunzi wa darasa la sita shuleni hapo.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Jonas Frank amekiri shule yake kukabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo usafi wa vyoo.
Hali hiyo, anasema, “haijaathiri sana afya za wanafunzi” licha ya kuwepo kwa “wanafunzi wachache ambao wanapatwa na magonjwa ambayo wanatokanayo nyumbani”.
Hata hivyo, Mwalimu huyo amewatupia lawama wakazi wanaoishi jirani na shule hiyo kuwa wamekuwa na tabia ya kuvunja milango nyakati za usiku na kutumia vyoo hivyo vya shule.
“Usafi unazingatiwa huwa tunafanya usafi mara mbili kwa siku, jioni wanapoondoka wanasafisha vinabaki visafi lakini majirani tukiweka kufuri wanavunja basi tunarudia tena asubuhi,” anasema Mwalimu Frank.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo lililozunguka shule hii wanakiri kutumia vyoo hivyo na kwamba hali hiyo inatokana na matatizo ya maliwato yao.
Mkazi anayeishi karibu na shule hiyo, Imani Kanjoka anaiambia Nukta kuwa wakati mwingine wanalazimika kutumia vyoo vya shule kutokana na vyoo vyao kutitia na kujaa maji hasa wakati msimu wa mvua.
“Huku Kyela vyoo ni tatizo kwa kuwa vingi vinatitia na kujaa maji, sasa nitaacha kutumia vyoo vya shule wakati nina haja? Lakini tunajitahidi kujenga vyoo vyetu ili tusiwasumbue wanafunzi,” anasema Kanjoka.

Ukosefu wa milango katika vyoo vya shule ya msingi Uhuru hutoa mwanya kwa wakazi walio karibu na shule hiyo kutumia na kuviacha vikiwa vichafu. Picha| Daniel Samson.
Adha anayoipata Luciana na wenzie wakati wa kwenda msalaani siyo ya bahati mbaya.
Shule hiyo ni miongoni mwa zile zenye uhaba mkubwa wa vyoo wilayani Kyela ikiwa na wanafunzi 836 wanaotumia matundu nane tu ikiwa ni wastani wa wanafunzi 104 kwa kila tundu moja, jambo linaloteta changamoto ya usafi na kusababisha wanafunzi kupoteza muda wa masomo kutokana na kusubiriana wakati wa haja.
Mwongozo wa Serikali unaagiza tundu moja litumiwe na wasichana 20 (1:20) na kwa wavulana ni 25 (1:25)
Uhaba huo unasadifiwa na takwimu kutoka ofisi ya Afisa Elimu Takwimu wilaya ya Kyela zinazobainisha kuwa hadi kufikia mwaka 2017, wilaya hiyo ilikuwa na mahitaji ya matundu 2,470 lakini yaliyokuwepo ni 1,761.Hii ina maana kuwa wilaya hiyo inaupungufu wa matundu 29 ya vyoo kati ya 100 yanayohitajika kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma bora za afya. Hata hivyo, hali hiyo ni nafuu kidogo ikilinanishwa na miaka mitano iliyopita.
Mathalani, mwaka 2013 Kyela ilikuwa na upungufu wa matundu ya vyoo zaidi ya nusu (asilimia 58) ya yaliyokuwa yanahitajika. Mwaka huo, mahitaji yalikuwa 2,393 wakati upungufu ulikuwa vyoo ni 1,411.
Ili kumaliza kabisa tatizo hilo la uhaba wa vyoo, Kyela bado ina kazi kubwa ya kujenga vyoo vipya na kuhakikisha vinapata vifaa na mfumo wa maji, ikizingatiwa kuwa wakazi wengi wa wilaya hiyo wanakabiliwa na tatizo la maji na usafi katika maeneo hayo ya kujisaidia.
Wanafunzi hatarini kukumbwa na magonjwa, vifo
Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa kama mazingira ya choo siyo safi na salama, uwezekano wa wanafunzi kukumbwa na magonjwa ya maambukizi ikiwemo kuhara ni mkubwa.
“Magonjwa yanayowakumba zaidi wanafunzi ni kuhara, homa ya tumbo, UTI (Maambukizi ya njia ya mkojo) na minyoo. Tangu Januari hadi Mei tumewatibu watoto 40 kati ya hao 9 waligundulika na magonjwa hayo,” anasema Upendo George, Muuguzi katika Zahanati ya Mkombozi iliyopo jirani na shule ya Uhuru.
Anasema ili kuepukana na magonjwa hayo, vyoo vijengwe kulingana na mahitaji ya wanafunzi na kuhakikisha usafi unafanyika kila mara ili wapate huduma kwa wakati wote.
Takwimu za Msingi za Elimu Tanzania (BEST) mwaka 2016 zinaeleza kuwa uwiano wa tundu la choo kwa wanafunzi nchini katika shule za msingi za umma sio wa kuridhisha.
“Tundu moja la choo linatumika na wastani wa wavulana 57 kinyume na kiwango cha wavulana 25. Pia tundu moja linatumika na wastani wa wasichana 56 kinyume na wasichana 20 kwa tundu,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.
Mtaalamu wa mipango miji, Mhandisi Levi Kasitu anaesema jiografia ya wilaya ya Kyela kuwa inachangia kukosekana kwa usafi kwenye vyoo kwa sababu kina cha maji kiko karibu na ardhi. Kutokana na hali hiyo, chemichemi za maji hupanda hadi juu ya ardhi na kulainisha udongo hatimaye vyoo vinajaa maji na kutitia.
Anashauri wanaojenga vyoo hasa katika maeneo ya shule kujengea kwa mawe tangu chini ya shimo jambo ambalo huenda baadhi likawa gumu kutokana na uwepo wa kipato kidogo.
“Wakisha chimba shimo la choo tunawashauri wajengelee kuanzia chini kabisa itakuwa iko salama na hawatapata changamoto wanazokabiliana nazo kwa sasa.”

Wadau wajitosa kuokoa jahazi
Katibu wa Muungano wa Asasi za Kiraia wilaya ya Kyela, Loth Mwangamba anasema Kyela inakabiliwa na changamoto nyingi za elimu lakini wanatumia rasilimali zilizopo kuboresha miundombinu ya shule ikiwemo vyoo.
“Tunatumia nafasi tulizonazo kuhakikisha tunapata wafadhili ambao wanaweza kusaidia kutatua tatizo hilo (la vyoo). Pia kuna Asasi moja ya The Mango Tree wamesaidia sana kwenye ujenzi wa vyoo, mimi mwenyewe nikiwa kama kiongozi nimeshiriki katika ujenzi wa shule sita za msingi na vyoo,” anasema Mwangamba.
Anaishauri Serikali kuendelea kushirikiana na Asasi za Kiraia wilayani humo katika kupanga vipaumbele vya elimu hasa ujenzi wa vyoo ili kuboresha mazingira ya kusomea kwa wanafunzi.
“Asasi za kiraia zimegawanyika kwenye maeneo kulingana, wengine kwenye mazingira, wengine kwenye afya, sasa unapokuwa muwazi kwenye huo muungano ni rahisi kwa asasi za kiraia kushirikiana kutatua tatizo la vyoo,” anasema Mwangamba.
Umoja wa Wabunge Wanawake wa Bunge la Tanzania nao wameanzisha kampeni maalum ya kuchangisha Sh3.2 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa vyoo vya mfano vya watoto wa kike vitakavyojengwa katika majimbo 264 ya uchaguzi nchini.
Mwenyekiti wa Umoja huo na Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM), Magreth Sitta amesema mpaka sasa wamepata kiasi cha Sh 2.3 bilioni ambapo gharama ya kila choo ni Sh 11 milioni na kukamilika kwa vyoo hivyo kutasaidia kupunguza tatizo la uhaba wa vyoo shuleni.
Serikali nayo yalia ukata kuwekeza kwenye miundombinu ya shule
Licha ya Serikali kuwa ndiye mwajibikaji mkuu katika kuboresha mazingira ya kujifunzia katika shule zote za umma nchini, nayo inalia na ukata kutokana na bajeti kutokidhi mahitaji ya sasa.
Mratibu wa Elimu kata ya Kyela, Hezron Mwaikinda, ambaye hapo awali alikuwa akisimamia Kata ya Mwanganyanga ilipo shule ya Uhuru, anasema bajeti inayotengwa kila mwaka kuboresha miundombinu haitoshi na wanaomba wafadhili kujitokeza kusaidia kuwajengea vyoo ili wanafunzi wapate mazingira mazuri ya kusomea.
Afisa Elimu mkoa wa Mbeya, Paulina Ndigeza anabainisha kuwa ujenzi wa vyoo unategemea mipango ya halmashauri katika kupanga vipaumbele katika elimu kulingana na fedha wanazopokea kutoka serikalini.
“Kitu ambacho kinafanyika kwenye masuala ya kujenga miundombinu; vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, matundu ya vyoo na mahitaji mengine ya shule, halmashauri inatenga bajeti kulingana na uwezo ambao uko kwa mwaka huo wa fedha,” anasema.
Choo cha shule ya msingi Uhuru wilaya Kyela kikiwa karibu na makazi ya watu ambapo wakati mwingine hutumia kujisitiri. Picha| Daniel Samson.
Latest