Ufanye nini pale mtoto anapomeza sarafu?

October 18, 2021 12:09 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Kikubwa cha kufanya ni kumfikisha kwenye kituo cha afya.
  • Pia kufanya jitihada za kujua kitu alichomeza.
  • Unaweza kuona dalili za kutokwa udenda mwingi, kukohoa na kupumua kwa shida.

Dar es Salaam. Kuna umri ukifika, watoto hupenda kujaribu vitu. Tuseme kuanzia mwaka mmoja na nusu hivi. Kwa watoto wengi kila kilichopo mbele ya macho yake hutafutiwa nafasi ya kuingia mdomoni.

Iwe mchanga, karatasi, kalamu na hata kiatu. Ilimradi kinashikika.

Hata hivyo, kwa baadhi ya vitu vinaweza kuwa hatari kwa maisha ya mtoto ni pamoja na pesa ya sarafu na vitu visivyotakiwa kuliwa tuseme mafuta, nafaka kubwa kubwa, zabibu na hata maputo.

Sarafu ni kitu kidogo na kinashikika pia na huenda rangi zake zikamvutia mtoto kuipeleka kinywani na hata kuimeza. Hali hiyo inaweza kumsababishia  mtoto kupaliwa.

Dalili za kuwa mtoto amemeza kitu ni pamoja na kutokwa na udenda, kukohoa pasi na kawaida, maumivu ya kifua, kushindwa au kupumua kwa shida na kutapika.

Inashauriwa kumuinamisha mtoto na kumpiga pole pole kwenye sehemu ya juu  ya mgongo kutoa sarafu hiyo. Picha| WikiHow.

Ufanye nini hali iyo ikitokea?

Kitu cha kwanza ni kuanza kufanya mpango wa kumpeleka mtoto kwenye kituo cha afya haraka iwezekanavyo kwani anaweza kupata changamoto ya kupumua kulingana na ukubwa wa sarafu.

Kwa mujibu wa mdau wa masuala ya afya, Dk Syriacus Buguzi amesema kama sarafu haijafika mbali, unaweza kumuinamisha mtoto na kumpiga polepole sehemu ya juu ya mgongo na inaweza kutoka.

“Isipotoka, inatakiwa umwahishe hospitali kwani kuna mambo mengi yanatakiwa kufanyika ikiwemo kuangalia kama inatembea au laa na hata ukubwa wake,” amesema Dk Buguzi.

Inashauriwa kujua wigo wa sarafu anayoweza kuwa amemeza mfano Sh50, Sh100, Sh200 au Sh500.

Tovuti ya masuala ya kiafya WebMd inaeleza kuwa, kuna vitu vingine havitakiwi kuvumilika hata kama mtoto haonyeshi dalili yoyote mbaya baada ya kuvimeza.

Vitu kama betri ndogo za saa, zinaweza kumuunguza utumbo mtoto ndani ya saa chache hivyo endapo ukijua ni nini mtoto amemeza hakikisha unampeleka hospitali haraka.


Unavyoweza kuzuia

Kikubwa ni kuweka umakini kwa mtoto wako pale anapokuwa anacheza na na hakiki vitu anavyochezea. 

Tovuti ya masuala ya watoto, children.com inashauri kuchukua tahadhari mapema ikiwemo kuhifadhi vizuri sarafu sehemu ambazo mtoto hafikii, kukaa na mtoto na kukagua kinywa chake mara kwa mara.

Kwa vitu vya kuchezea, inashauriwa kuhakikisha mabetri yamefungwa vizuri (kwa nati) na mtoto hawezi kufungua hata kama haupo karibu naye.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW