Udumavu kwa watoto utapungua, wazazi wakiongeza ubunifu
- Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile amewataka walimu na wazazi kuhakikisha watoto wanapata lishe bora ili kuinua viwango vya ufaulu.
- Amesema elimu bure haiwazuii wazazi kuwa wabunifu kuinua elimu ya watoto wao.
Dar es Salaam. Serikali imesema kuwa sera ya elimu bure siyo sababu ya wazazi na walezi kukosa ubunifu wa kuwasaidia wanafunzi kufanya vizuri darasani ikiwemo kuanzisha mikakati ya kuwapatia chakula katika maeneo yao.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Faustine Ndugulile aliyekuwa akizungumza leo (Januari 8, 2020) alipotembela Shule ya msingi Mnyigumba mkoani Iringa, amesema lishe bora kwa wanafunzi ni muhimu katika kujifunza darasani na afya zao.
“Elimu bure siyo sababu ya wazazi, walimu na shule kutokuwa wabunifu katika kuhakikisha wanajiongeza katika masuala ambayo yatasaidia wanafunzi kuongeza juhudi katika masomo na kuongeza ufaulu,” amesema Dk Ndugulile.
Amesisitiza kuwa elimu ya lishe inatakiwa kutolewa kwa wananchi hasa katika maeneo ambayo tatizo la udumavu na utapiamlo linaongezeka kwa kasi katika maeneo ya Nyanda za juu kusini ikiwemo mkoa wa Iringa ingawa mikoa hiyo inaongoza katika uzalishaji wa chakula.
“Niwapongeze Shule yenu ya Mnyigumba kwa kujiongeza nakupongeza sana Mkuu kwa kubuni kwa kulima mahindi na kuyatumia kupata chakula kwa ajili ua wananfunzi ili wazingatie katika masomo yao,” amesema Naibu Waziri huyo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akifurahia jambo na wanafunzi wa Shule ya Msingi Mnyigumba mkoani Iringa mara baada ya ziara yake Shuleni hapo kuangalia masuala ya Lishe. Picha| Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Pia amewataka maafisa maendeleo ya jamii kuweka mkazo katika kutoa elimu ya lishe hasa katika shule za msingi na sekondari nchini Tanzania ili kuondokana na tatizo la udumavu na utapiamlo kuwawezesha wanafunzi kutimiza ndoto zao za elimu.
Utafiti wa utafiti wa afya na idadi ya watu Tanzania (Tanzania Demographic Health Survey-TDHS) wa mwaka 2018 unaonyesha kuwa asilimia 31.8 ya watoto nchi wamedumaa kutokana na lishe duni.
Hiyo ni sawa kusema kwa kila watoto 100 basi takriban watoto 32 wameduma, jambo ambalo linawaweka katika hatari ya wao kuwa na vimo vifupi kuliko umri wao.
Zinazohusiana:
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Msingi Mnyigumba, Richius Mwamanga amesema kuwa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Rungemba kimewasaidia katika kuhamisha jamii katika ujenzi wa jiko la shule kwa ajili ya kupikia chakula ambapo limefikia katika hatua ya kupaua.
Ameongeza kuwa Shule imelima shamba la mahindi yaliyosaidia kutoa chakula kwa shule hiyo hivyo kusaidia wanafunzi hao kuzingatia masomo na kuongeza ufaulu wao.
“Tunakipongeza na kukishukuru Chuo cha Maendeleo ya Jamii Rungemba kwa kutoa hamasa na elimu kawa wananchi ili kuhakikisha wanabadili mawazo na kushiriki katika shughuli za maendeleo yao,” amesema Mwamanga.
Oktoba 4, 2019 katika ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa wadau wa lishe jijini Dodoma Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliutaja utapiamlo kama moja ya vikwazo vitakavyokwamisha Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025 kama lishe bora haitozingatiwa kwa Watanzania.
Latest