Ubadhirifu unavyotishia uhai wa vyama vya ushirika Tanzania
- Hati mbaya zaongezeka katika vyama hivyo kutokana na dosari za mahesabu.
- Ukosefu wa elimu, maadili wachangia ubadhirifu kutawala katika vyama hivyo.
- Wadau waingilia kati kuokoa jahazi.
Dar es Salaam. John Mkama ni miongoni mwa wafanyabiashara wa jijini Dar es Salaam wenye shauku kubwa ya kuingia katika Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS).
Mkama, mkazi wa Bunju B jijini hapa, yeye na wenzake 20 tayari wameanza mchakato wa usajili wa Saccos yao katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
Huenda shauku ya kufaidika na chama chake ikakatishwa kama hakutakuwa na mifumo imara ya uongozi na usimamizi wa fedha.
Ukosefu wa usimamizi mzuri wa fedha ni miongoni mwa changamoto kubwa zilizopo katika vyama vya ushirika kwa sasa, jambo ambalo linaloibua maswali mengi kuhusu mstakabali wake siku zijazo.
Uchambuzi uliofanywa na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) wa ripoti ya Hali ya Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika kwa mwaka 2021/22 iliyotolewa Novemba 2022 na Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) inaonyesha kuwa mahesabu ya mapato na matumizi katika vyama vingi vya ushirika hayajakaa sawa.
Hali hiyo inatishia uhai wa vyama vya ushirika Tanzania na hatua zisipochukuliwa wananchi waliojiunga navyo watapata hasara na kushindwa kuchangia katika ukuaji wa uchumi.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa kwa mwaka 2021/22, vyama vya ushirika 2,075 (asilimia 34.5) ya vyama 6,005 vilivyokaguliwa mwaka huo vilipata hati mbaya. Hiyo ni sawa na kusema vyama vitatu kati ya 10 vilipata hati mbaya ya ukaguzi.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), hati mbaya hutolewa pale ambapo mkaguzi amepata ushahidi wa kutosha kuwa dosari ama moja moja au kwa ujumla zilizobainika wakati wa ukaguzi ni kubwa na zimeathiri sehemu kubwa ya taarifa za fedha hivyo kusababisha taarifa hizo kutokuwa sahihi.
Jambo la kushangaza ni kuwa idadi ya vyama vya ushirika vinavyopata hati mbaya imekuwa ukiongezeka mfululizo tangu mwaka 2018/19, licha mapendekezo mbalimbali kutolewa kupunguza hati hizo.
Mathalan, mwaka 2018/19 vyama 853 vilipata hati mbaya na mwaka uliofuata vikaongezeka hadi 1,670 na mwaka 2020/21 vikaongeza hadi 1,729 kabla havijaongezeka zaidi hadi 2,075 mwaka jana.
Wakati hati mbaya zikiongezeka, hati zinazoridhisha katika vyama hivyo zimekuwa zikiongezeka na kupungua. Hata hivyo, tangu mwaka 2018/19 hazijawahi kuzidi asilimia 10, jambo linaloibua maswali mengi kuhusu usahihi wa hesabu katika taasisi hizo muhimu.
Mathalan, mwaka 2020/21 vyama vya ushirika 357 vilipata hati zinazorishisha lakini mwaka uliofuata vikapungua hadi 339 (asilimia 5.6).

Vyama vya ushirika vilivyokaguliwa katika makundi tofauti tofauti ni Shirikisho la Vyama vya Ushirika nchini (TFC), Vyama Vikuu (UNION), Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS), Chama Cha Ushirika wa Kilimo na Masoko (AMCOS) na Vyama vinginevyo (kama vile vyama vya madini, nyuki, uvuvi).
Kuongezeka kwa idadi ya vyama vya ushirika vinavyopata hati mbaya inaweza kuwa ni ishara mojawapo kuwa kuna ubadhirifu unaoendelea katika taasisi hizo.
Chama Kikuu Cha Ushirika cha Wakulima Morogoro (MOFACU) ni moja ya taasisi zilizopata hati mbaya mwaka 2021/22.
Ripoti hiyo ya hali ya ukaguzi ya Coasco, inaeleza kuwa limbikizo la hasara la MOFACU limeongezeka hadi Sh629.8 milioni Machi 2021 kutoka Sh602.6 milioni huku uhai wa chama hicho ukiwa mashakani siku za usoni katika shughuli zake.
Chama hicho kushindwa kufanya shughuli za msingi za kuanzishwa kwake pamoja na kutokuwa na mpango mkakati wa biashara jambo linalosababisha chama kutokuwa na mapato yanayotosheleza gharama za uendeshaji.
“Chama kinaonyesha kuwa kina wadaiwa wa kibiashara kwa jumla ya Sh67.4 milioni lakini wadaiwa hao wamekuwa sinzia kwa muda mrefu na hawalipi madeni yao. Vilevile kuna bidhaa ghalani za Sh10.3 milioni lakini mali hizo zimekuwa ni salio tu vitabuni kwa miaka mingi na hazina ushahidi wa uwepo wake.
“Aidha, chama kina madeni ya muda mfupi makubwa kuliko mali za muda mfupi kwa uwiano wa 0.43:1 jambo linaoonyesha kuwa chama kipo kwenye hali mbaya kifedha,” inaeleza ripoti hiyo.
Mmoja wa viongozi wa Chama cha Ushirika cha Tandahimba na Newala (Tanecu) ambaye hakutaka jina lake litajwe anasema vyama vya ushirika kuendelea kupata hati mbaya ni matokeo ya kutokufanyia kazi dosari zilizogundulika katika kaguzi zilizopita hivyo kufanya dosari hizo kuendelea kuwepo kwenye taarifa za fedha.
Soma zaidi:
-
Majaliwa aagiza elimu itolewe upangaji madaraja ya korosho
-
Serikali yatoa maagizo mazito chama cha ushirika Jeshi la Polisi
-
Chama ushirika Nyanza chatakiwa kuandaa mikakati ya kujitegemea
Sababu vyama vingi vya ushirika kupata hati mbaya
Ripoti ya ukaguzi ya Coasco kwa mwaka 2021/22 inaeleza kuwa kuongezeka kwa hati mbaya ni ishara kuwa utendaji katika vyama vya ushirika bado ni changamoto katika mfumo wa udhibiti wa ndani hususani katika uandishi wa miamala ya hesabu, utunzaji wa kumbukumbu za fedha pamoja na uandaaji wa taarifa za fedha kulingana na viwango vya Uhasibu vinavyokubalika.
Mchambuzi wa masuala ya uchumi na ushirika kutoka mkoani Mbeya, Kennedy Masika anasema vyama vingi vimekosa mifumo ya udhibiti wa ndani hivyo kushindwa kuandika miamala ya fedha kwa usahihi na ukamilifu.
“Hali hii imesababisha vyama vingi kuwa na tofauti za hesabu za hisa, akiba, amana na mikopo kutofautiana,” anasema Masika ambaye pia ni mfanyabiashara wa kahawa mkoani humo.
Anasema jambo hili husababisha watendaji wasio waaminifu kuweza kufanya ubadhirifu kwenye hesabu za mikopo na akiba za wanachama hivyo kusababisha hasara kwa chama na wanachama.
Ukaguzi wa taarifa za hesabu za Vyama vya Ushirika hapa nchini hufanyika kwa mujibu wa matakwa ya sheria ambayo yameelezwa na kifungu cha 55(3) cha Sheria ya Vyama vya Ushirika Na.6 ya mwaka 2013.
Kifungu cha 55(2) cha Sheria ya Vyama vya Ushirika ya mwaka 2013, kinavitaka Vyama vya Ushirika kutayarisha hesabu katika kipindi cha ndani ya miezi mitatu baada ya mwisho wa mwaka wa fedha na kuziwasilisha kwa mkaguzi (COASCO) kwa ajili ya ukaguzi.
Hiyo husaidia kufuatilia mwenendo wa mapato na matumizi ya vyama hivyo ili kuhakikisha vinaendeshwa kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizowekwa.
Mnada wa tumbaku uliofanyika hivi karibuni katika ghala la chama cha msingi Lupa Amcos mkoani Mbeya. Picha | TCDC.
Nini kifanyike?
Kutokana na vyama vingi vya ushirika kupata hati mbaya, baadhi ya wataalam wa uchumi na ushirika nchini wanashauri, vyama hivyo vijingewe uwezo zaidi ikiwemo kupewa mafunzo ya mara kwa mara ya kusimamia rasilimali zao ili kuepusha ubadhirifu.
“Elimu inahitajika sana kwa vyama vya ushirika kwa sababu wakati mwingine mambo yanayotokea ni kwa sababu watendaji hawana uelewa mzuri wa kusimamia rasilimali zao. Wakijengewa uwezo mapungufu yatapungua miaka ijayo,” anasema mdau wa masuala ya ushirika Hermes Rulagirwa.
Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Valency Karunde anasema mifumo ya vyama vya ushirika hasa ya mapato ikiimarishwa itasaidia kupunguza mianya ya ubadhirifu na kusaidia vyama hivyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi.
“Mfumo huu wa usimamizi wa vyama vya ushirika utatusaidia kupata taarifa kutoka kwenye vyama na kutoka kwa wadau mbalimbali wa ushirika kwa wakati na Serikali inategemea kupata taarifa hizo kwa wakati na kwa usahihi,” anasema Karunde.
Ripoti ya hali ya ukaguzi wa vyama vya ushirika ya Coasco, inapendekeza kuwa Mrajis wa Vyama vya Ushirika avichukulie hatua za kisheria na kinidhamu vyama vyote vilivyobainika kuwa na ubadhirifu wa fedha za chama na kuvifanyia ukaguzi maalum ili kuchukua hatua za kisheria kwa wahusika na kuleta nidhamu katika matumizi ya fedha za wanachama.
Naye Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika (Udhibiti), Collins Nyakunga anawataka viongozi wa vyama vya ushirika nchini kuhakikisha kuwa vyama vyao vinaondokana na hali mbali ya ukaguzi na kuhakikisha vitabu vya mahesabu vinaandaliwa ipasavyo na kukaguliwa na wakaguzi wa nje.
Nyakunga anasema kuwa ili kuondokana na changamoto zinazosababisha kupata hati mbaya inatakiwa viongozi wa vyama vikuu vya ushirika kutambua majukumu yao na kufanya kazi kwa kujali miongozo ya vyama vya ushirika.
Latest