Twaweza: Wazazi wengi hawajui matokeo halisi ya shule za watoto wao
- Zaidi ya nusu au asilimia 56 ya wazazi waliohojiwa na utafiti wa Twaweza walisema matokeo yenye ufaulu wa chini ya asilimia 51 ni “mazuri” na “mazuri sana”.
- Ni asilimia tano tu ya wazazi waliosema matokeo ya shule zao ni “mabaya” au “mabaya sana” kwa alama hizo za ufaulu.
- Hata hivyo, wazazi huangalia ufaulu wa matokeo ya kidato cha nne na uwepo wa walimu wenye ari ya kufundisha kama moja ya kigezo cha kupeleka watoto wao sekondari.
Dar es Salaam. Wakati wazazi wengi wakihamasika kupeleka watoto wapate elimu ya msingi, imebainika kuwa zaidi ya nusu ya wazazi hao ambao watoto wao wapo katika shule za msingi wanashindwa kutafsri kwa usahihi juu ya ufaulu wa matokeo ya mitihani.
Hali hiyo inatokea licha ya jitihada za Serikali na wadau wengine wa elimu kusambaza matokeo ya mtihani ya kuhitimu darasa la saba, kidato cha nne na sita kupitia tovuti mbalimbali ikiwemo ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) na mitandao ya kijamii.
Utafiti wa Sauti za Wananchi uliofanywa na taasisi ya Twaweza umeonyesha kuwa asilimia 56 ya wazazi waliohojiwa walishindwa kutafisiri matokeo ya watoto wao vyema yaliyokuwa na ufaulu wa chini ya asilimia 51.
Mkurugenzi Mtendaji wa asasi ya kiraia ya Twaweza, Aidan Eyakuze amesema uelewa wa wazazi katika kutambua matokeo sahihi ya ubora wa ufaulu katika shule za msingi zilizopo katika maeneo yao upo chini hususan maeneo ya vijijini.
Wanafunzi wakitazama matokeo yao ya kuhitimu elimu ya msingi. Picha na Maktaba.
Utafiti huo uitwao “Elimu Bora au Bora Elimu? Elimu waitakayo watanzania” uemeeleza kuwa upo utofauti mkubwa wa wazazi katika tasfri ya matokeo ya mitihani ya darasa la saba na matokeo halisi .
‘’Mathalani matokeo ya shule ya msingi yenye matokeo mabaya chini ya asilimia 51 ya ufaulu wazazi sawa na asilimia 56 walitasfri matokeo ya shule zao ni “mazuri” au “mazuri sana” huku asilimia tano tu ndio waliosema matokeo ya shule zao ni mabaya au mabaya sana,’’ anaeleza Eyakuze.
Anasema wazazi walipoulizwa kwenye shule za msingi zenye wa kiwango kizuri cha ufaulu wa asilimia 91, ni asilimia 15 tu ya wazazi waliosema matokeo ya shule ni mazuri sana. Robo yao au asilimia 26 walisema ni wastani au mabaya.
“Uboreshaji wa elimu ni jukumu la wote”
Wadau wanaeleza kuwa ili kuboresha elimu nchini kuna haja ya jamii nzima kuwajibika kwa kufanya mambo mbalimbali ikiwemo kupitia mfumo mzima wa elimu.
Mbunge wa zamani wa Bunge la Afrika Mashariki, Dk Perpetua Nderakindo anasema haitakiwi kuitegemea Serikali pekee yake katika kuboresha elimu hivyo ni lazima kuwe na ushirikiano wa pamoja na uwajibikaji katika kutengeneza mfumo wa elimu nchini utakaozaa matunda yanayotakiwa katika taifa.
“Dunia ya sasa inahitaji ushirikiano na naamini wazazi wanataka elimu bora kwa watoto wao hivyo ushirikiano, uwajibikaji na uwekezaji ni vya muhimu katika elimu yetu,” anasema Dk Nderakindo.
Hata hivyo, baadhi wanaeleza kuwa usimamizi mzuri wa shule nchini utasaidia kurudisha ubora wa elimu itakayowaandaa vijana kukabiliana na changamoto za ulimwengu wa sasa.
Meneja wa Utafiti na Sera wa asasi ya kiraia ya Haki Elimu, Bonaventure Godfrey amesema suluhisho ya changamoto hizo katika elimu moja wapo ni usimamizi bora wa shule nchini.
Anaeleza kuwa shule zote za msingi na sekondari zikisimamiwa vyema kwa Serikali kuwajibika ipasavyo wananchi au wazazi nao watawajibika.
“Mbali na kufutilia maendeleo ya shule na mtoto, njia nyingine za kuboresha elimu ni uwepo wa walimu bora, vifaa na uwekezaji katika elimu,” Bonaventure Godfrey.
Teknolojia kusaidia kuongeza uelewa wa matokeo
Ili kupunguza changamoto hiyo ya wazazi kushindwa kutasfri matokeo kwa ufasaha, baadhi ya wabunifu wamebuni teknolojia ambazo zinachambua takwimu za matokeo na kuwarahisishia wazazi na wadau wa elimu kufuatilia ufaulu wa shule zao ili kusaidia kufanya maamuzi.
Moja ya teknolojia hiyo ni tovuti ya Elimu Yangu ambayo imelenga kuwasaidia wazazi, walezi kujua shule bora za kuwapeleka watoto wao na zile za mwisho ili kusaidia kuziboresha kwa kutumia matokeo ya mitihani ya sekondari ambayo hutolewa na Necta.
Mbali na kuonyesha historia ya ufaulu wa shule husika, tovuti hiyo iliyotengenezwa na taasisi ya Code for Tanzania kupitia mradi wa Data Zetu pia inawasaidia wanafunzi waliohitimu kidato cha sita kubaini iwapo alama zao walizozipata zinafaa kwenda kusoma chuo kikuu ama la. Tovuti hiyo itaanza kupatikana ndani ya Nukta hivi karibuni.
Hata wakati nusu ya wazazi wenye watoto shule za msingi wakishindwa kutafsiri matokeo ya mitihani, utafiti huo wa Twaweza uliotolewa Mei 17 mwaka huu umeeleza pia kuwa takriban robo tatu ya wazazi au asilimia 72 wanazingatia uwepo wa walimu wazuri na ufaulu wa mtihani wa kidato cha nne kama vigezo muhimu vya kupeleka watoto wao shule.