Tuzo za Samia Kalamu 2026 kufanyika Desemba, vigezo vipya vyatajwa 

June 1, 2026 1:38 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link

Arusha. Msimu wa pili wa Tuzo za Samia Kalamu Awards 2026 umezinduliwa rasmi huku kigezo kikuu kwa washiriki kikiwa ni kuwa na kitambulisho kinachotolewa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB).

Tuzo hizo zinazoandaliwa kwa ushirikiano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) na JAB, zinalenga kukuza uandishi wa habari za maendeleo na kuhamasisha uzalishaji wa maudhui yanayochochea mabadiliko chanya katika jamii.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tuzo hizo, Peter Mwasalyanda, akizungumza na waandishi wa habari Mei 31, 2026, amesema tuzo hizo zitaendelea kuwa chachu ya kukuza taaluma ya uandishi wa habari nchini.

“TCRA na Tamwa tunaamini kuwa Samia Kalamu Awards zitaendelea kuwa chachu muhimu ya kuendeleza taaluma ya uandishi wa habari hapa nchini kwa kuhamasisha uzalishaji wa maudhui yenye ubora, yanayozingatia maadili na yenye mchango chanya katika maendeleo ya Taifa,” amesema Mwasalyanda.

Kwa mujibu wa waandaaji, tuzo hizo zitahusisha makundi matatu ambayo ni Tuzo Maalumu za Kitaifa, Tuzo za Vyombo vya Habari na Tuzo za Kisekta, huku washindi wa makundi hayo wakitarajiwa kutangazwa na kukabidhiwa tuzo zao katika hafla itakayofanyika Desemba 2026.

Mwaka jana wanahabari wengi waliitokeza kushiriki katika tuzo hizo, akiwemo aliyekuwa Mratibu wa Dawati la Habari la Nukta Africa, Esau Ng’umbi, ambaye aligombea katika kipengele cha Fedha na Uchumi na kushika nafasi ya pili.

Vigezo vyatajwa

Mbali na vigezo vya jumla, waandaaji wamesema mwandishi wa habari anayetarajia kushiriki anapaswa kuwa raia wa Tanzania aliyethibitishwa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) kwa upande wa Tanzania Bara, huku kwa Zanzibar akitakiwa kutambuliwa na mamlaka husika.

“Pia awe na kitambulisho cha mwandishi wa habari na asiwe na rekodi ya kutiwa hatiani kwa kosa lolote la jinai,” amesema.

Kazi inayowasilishwa inapaswa kuwa moja iliyochapishwa, kutangazwa au kurushwa kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza katika chombo cha habari cha ndani au nje ya Tanzania ikiwa imefanyiwa utafiti wa kina unaojumlisha uchambuzi wa takwimu na kutumia vyanzo vya habari visivyopungua vinne.

Kazi hiyo pia isiwe imewahi kushindanishwa katika tuzo nyingine na iwe imechapishwa, kutangazwa au kurushwa kati ya Julai 1, 2023 na Juni 30, 2026.

Kwa upande wa Tuzo za Vyombo vya Habari, chombo kinachoshiriki kinapaswa kuwa na leseni halali iliyotolewa na mamlaka husika.

Waandaaji wameeleza kuwa kazi zitakazopitishwa na majaji zitapigiwa kura na waandishi wa habari pamoja na wananchi kupitia tovuti na ujumbe mfupi wa simu (SMS), ili kuhakikisha kunakuwa na uwiano kati ya weledi wa kitaaluma na maoni ya hadhira.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tamwa, Dk Kaanaeli Kaale, amewataka waandishi wa habari kujitokeza kwa wingi kushiriki katika tuzo hizo, akisisitiza kuwa hazilengi kuminya uhuru wao wa kufanya kazi.

“Niwaondoe wasiwasi watu wanaosema labda tuzo hizi zinawakamata waandishi wa habari na kuwaweka mfukoni, si kweli,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Nukta Africa yang’ara tuzo za EJAT 2025, yanyakua tuzo nne

Nukta Africa yang’ara tuzo za EJAT 2025, yanyakua tuzo nne

Nukta TV

Matumizi mabaya ya madaraka bado changamoto Utumishi wa umma

Matumizi mabaya ya madaraka bado changamoto Utumishi wa umma

Nukta TV

Ridhiwani Kikwete achukizwa na tabia hii ya baadhi ya Maofisa Rasilimali Watu.

Ridhiwani Kikwete achukizwa na tabia hii ya baadhi ya Maofisa Rasilimali Watu.

Nukta TV