TRA yawafunda wanahabari wa mtandaoni

May 30, 2024 4:55 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Yawataka kutoa taarifa sahihi kuhusu masuala ya kodi ili kuvutia uwekezaji.
  • Mfumo mpya wa ukusanyaji mapato TRA wanukia.

Dar es salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa elimu kwa waandishi wa habari za mtandaoni kuhusu umuhimu wa kodi na jinsi inavyoweza kuchangia ukuaji wa pato la Taifa.

Kaimu Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano TRA, Hudson Kamoga aliyekuwa akifungua semina kwa wanahabari jijini Dar es Salaam amewataka waandishi wa habari za mtandaoni kutumia vyema nafasi waliyonayo ya kufikia watu wengi kusambaza taarifa sahihi kuhusu kodi ili kuvutia uwekezaji nchini.

 “Tukiwa wazalendo wote kwa pamoja tutakuwa makini ni nini tunaipelekea dunia na nini waone…masuala ya kodi ni masuala nyeti yanarahisisha uchumi, biashara na kuvutia wawekezaji. Ni vizuri tukiwa tunaripoti tuwe na uelewa mpana,” amesema Kamoga.

Kupitia semina hiyo zaidi ya wanahabari 100 wa vyombo vya habari mtandaoni wamepatiwa elimu ya kodi itakayowawezesha kuandika habari za sekta hiyo kiusahihi.

Miongoni mwa mada zilizowasilishwa ni pamoja na uhakiki wa bidhaa zilizosajiliwa na mamlaka hiyo ambapo wanahabari wametakiwa kuwatadharisha wananchi juu ya bidhaa feki ikiwemo vinywaji ambavyo havijasajiliwa na mamlaka hiyo.

Kwa mujibu wa TRA bidhaa hizo ambazo wazalishaji wake hukwepa kodi kwa kutozisajili zinaweza kusababisha magonjwa mbalimbali kwa watumiaji ikiwemo yasiyo ya kuambukiza. 


Soma zaidi:Dar es Salaam kinara kwa idadi kubwa ya migogoro ya ardhi Tanzania


Itakumbukwa kuwa Waziri wa Afya Ummy Mwalimu aliyataja magonjwa yasiyoambukizwa ikiwemo kisukari kuwa miongoni mwa magonjwa 10 yaliyowatesa zaidi watanzania kwa mwaka 2023 na kutaka hatua  za kuyadhibiti kuchukuliwa.

“Zamani miaka mitatu tulikuwa hatuoni shinikizo la juu ya damu wala kisukari katika orodha ya magonjwa 10 yanayoongoza kwa wagonjwa wa nje, kwa hiyo ni jambo ambalo tutalielekeza kuona ni lipi tutafanya,” alisema Ummy Mwalimu Januari 10, 2024 jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Waziri Ummy magonjwa hayo yameongezeka siku za hivi karibuni kutokana na ulaji usiofaa pamoja na kukithiri kwa tabia bwete.

Ili kudhibiti uuzwaji wa bidhaa hizo TRA imewataka wanahabari kuwaelimisha umma jinsi ya kuthibitisha uhalali wa bidhaa kabla ya kuzitumia kwa kutumia mifumo ya kidigitali ikiwemo programu tumizi (app) zinazotumika kuhakiki msimbo (barcode) za bidhaa hizo zinazopatikana ‘play store’ na ‘App store’

Mada nyingine zilizowasilishwa katika semina hiyo ni pamoja na ushuru wa forodha na uchumi wa kidigitali ambao unaweza kuwasaidia waandishi wa habari na  mamlaka hiyo kukusanya mapato kutoka vyanzo vya kigitali ikiwemo mitandao ya kijamii kutoka ndani na nje ya nchi.

Kaimu Mkurugenzi wa elimu kwa mlipa kodi na mawasiliano TRA, Hudson Kamoga akisisitiza jambo wakakwti wa ufunguzi wa semina kwa waandishi wa habari wa mtandaoni. Picha|Tupo Digito.

Mfumo mpya wa ukusanyaji mapato TRA wanukia

Katika semina hiyo TRA pia imedokeza wanahabari juu ya ujio wa mfumo mpya wakukusanya mapato unaojulikana kama ‘Integrated domestic revenue system’ (IDRAS) utakaoanza kutumika Agosti, 2025.

Mfumo huo utaiwezesha TRA kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato ya na kuchangia katika ukuaji wa uchumi nchini.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Mtandaoni JUMIKITA Shaaban Matwebe amewataka TRA kufanya semina hizo kwa waandishi waliopo katika maeneo mengine nchini ikiwemo mikoani ili kuongeza uelewa wao katika kuripoti masuala ya kodi.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW