Tigo yatangaza kuchukua umiliki wa Zantel

November 4, 2019 1:11 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Kampuni hizo zimeungana baada ya kukamilika kwa taratibu za kisheria na umiliki.
  • Lengo ni kuboresha huduma za mawasiliano nchini na kuimarisha soko la ushindani.
  • Mchakato wa kuunganisha kampuni hizo hautaathiri shughuli za kiutendaji lakini  kutakuwa na athari ndogo kwa wafanyakazi wa makampuni haya mawili.

Dar es Salaam. Kampuni za mawasiliano ya simu nchini Tanzania za Tigo na Zantel zimeungana rasmi baada ya kukamilika kwa taratibu za kisheria na umiliki ikiwa ni hatua ya kuboresha huduma za mawasiliano nchini. 

Kufuatia kukamilika kwa zoezi la umiliki, sasa makampuni haya yataunganisha shughuli zake za kiutendaji Tanzania Bara na visiwani Zanzibar. Umiliki huo ulihusu kuhamisha hisa kutoka Zantel kwenda Tigo.

Akizungumzia kuhusu muungano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Tigo, Simon Karikari amesema hatua hiyo ina manufaa makubwa kwa Taifa kwani inaongeza ushindani katika sekta ya mawasiliano nchini.  

“Ninaamini kuwa kuunganishwa kwa kampuni hizi – Tigo na Zantel kutajenga huduma jumuishi kwa Watanzania wote siku za usoni. Wateja wote wa Tigo na Zantel wataweza kufurahia huduma bora kutoka kwenye soko imara litakalosaidia kuchochea ubunifu kwenye sekta ya mawasiliano,” amesema Karikari. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Tigo leo (Novemba 4, 2019), muungano huu utawezesha kupanua wigo wa huduma pamoja na kuongeza ubora wa upatikanaji wa mawasiliano katika maeneo ya mijini na vijijini. 

“Vile vile muungano huu utasaidia katika usambazaji wa huduma za mawasiliano kwa makampuni na taasisi mbalimbali nchini na pia kupanua huduma za kifedha kwa njia ya simu za mkononi,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.  

Zoezi la kuunganisha taratibu za kiutendaji wa makampuni haya mawili zinatazamiwa kuanza hivi punde ambapo wateja wa Tigo na Zantel wataendelea kupata huduma bila usumbufu wowote kutoka mtandao husika kwani namba na laini za wateja hazitabadilika.


Zinazohusiana: 


Kampuni hizo zitatoboa katika anga la mawasiliano?

Kwa sasa kampuni hizo mbili ambazo zimeungana zina wateja wanaofikia milioni 12.8 ambapo kati yao wanaotumia huduma za  kifedha kwa njia ya simu za mkononi ni milioni 7.4.

Taarifa ya Tigo inaeleza kuwa, “kwa sasa soko la mawasiliano Tanzania limegawanyika sana hivyo kulikuwa na uhitaji wa kuunganisha makampuni haya.” 

Uchambuzi  wa takwimu za robo ya pili ya mwaka 2019 (Aprili-Juni) zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha kuwa hadi Juni, Tigo ilikuwa inamiliki asilimia 27 ya soko la mawasiliano na Zantel ikimiliki asilimia tatu.

Huenda kuunganishwa kwa makampuni hayo kutaongeza nguvu ya ushindani ikizingatiwa kuwa katika siku za hivi karibuni makampuni hayo yamekuwa yakipoteza idadi ya wateja kwa viwango tofauti. 

Mathalani. Tigo ambayo mwezi Machi ilikuwa na watumiaji milioni 12.5 walipungua hadi kufikia milioni 11.6 Juni mwaka huu. Kwa muktadha huo, Tigo imepoteza watumiaji 798,282. 

Lakini Tigo imebainisha kuwa kuunganishwa kwa shughuli za kiutendaji baina ya kampuni hizo kutaweka mazingira shindani na yenye tija kwa Taifa, kuchochea maendeleo na ubunifu katika sekta ya mawasiliano na zaidi kuimarisha uwezo wa makampuni haya ili kuyawezesha kutoa huduma zenye ubora wa kimataifa kwa wateja wao. 

Kwa sasa, Tigo na Zantel zitaendelea kujiendesha kama kampuni tofauti na biashara zitaendelea kama kawaida. Wakati zoezi la kuunganisha makampuni haya mawili likiendelea, kutakuwa na uhamishaji wa rasilimali ndani ya Tigo na Zantel ambao hautaathiri shughuli za kiutendaji lakini  kutakuwa na athari ndogo kwa wafanyakazi wa makampuni haya mawili. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW