Taxify ilivyojipanga kupunguza adha ya usafiri Dodoma
- Usafiri huo unaratibiwa mtandaoni unakusudia kupunguza gharama za usafiri na kuwaongezea abiria usalama.
- Watakaofaidika ni wale wanaotumia taski lakini madereva wa bajaj watalazimika kusubiri kidogo.
- Ni fursa ya kuimarisha sekta ya usafiri jijini ambayo inakabiliwa na changamoto ya ongezeko kubwa la watu.
Dar es Salaam. Wakazi wa Jiji la Dodoma wanaotumia usafiri wa taski huenda wakapata ahueni ya kupunguziwa gharama za nauli baada ya kampuni ya usafiri mtandaoni ya Taxify kuingia rasmi jijini humo.
Jiji hilo linakuwa kwa kasi hasa baada ya Serikali kuhamishia shughuli zake za utawala kutoka Jijini Dar es Salaam, jambo lililoongeza idadi ya watu na kuleta changamoto ya usafiri katika maeneo ya mjini ambako shughuli za kiuchumi na biashara huratibiwa.
Taxify ambayo imejiimarisha katika majiji ya Dar es Salaam na Mwanza wameamua kuingia Dodoma ikiwa ni sehemu ya kuongeza ushindani wa matumizi ya teknolojia ya kisasa kuwarahisishia wananchi huduma za usafiri popote walipo.
Kupitia huduma ya Taxify wateja wanaweza kupunguza gharama za usafiri ambazo wanatozwa na madereva wa taski za kawaida ambapo kampuni hiyo inayotumia simu janja kuratibu usafiri inawahakikishia usalama, urahisi na uhakika wa kwenda mahali popote kwa nauli wanayoweza kuimudu.
“Gharama ya usafiri itakuwa ni Sh450 kwa kilomita moja na kwa muda huu wa uzinduzi itakuwa ni Sh400 kwa Kilomita,” amesema Meneja Mkuu wa Taxify Tanzania, Remmy Eseka.
Eseka amesema nauli anayotozwa mteja hutegemea umbali, gharama za kumfuata alipo, tozo mbalimbali za barabarani lakini ni nafuu ukilinganisha na zile zinazotozwa na madereva wa kawaida hutokana na makadirio au maelewano kati ya dereva na abiria.
Baadhi ya wakazi wa Jiji hilo ambalo ndiyo Makao Makuu ya nchi wameiambia Nukta kuwa ikiwa Taxify imekuja kwa lengo la kuwapunguzia gharama za usafiri basi kwao itakuwa heri kwasababu wamekuwa wakitozwa gharama kubwa za taski wanapokuwa kwenye mizunguko ya katikati ya Jiji.
“Kwa maeneo ya Area C au D hadi mjini ni Sh.5,000 na ukiwa karibu mjini hapahapa unaweza kupanda kwa Sh.3,000,” amesema Emmanel Monga mkazi wa St Peters, Dodoma.
Monga pia amebainisha kuwa kuna baadhi ya maeneo kama Kisasa upatikanaji wa taksi ni changamoto hivyo kukiwa na huduma ya mtandao itarahisisha kupata usafiri kwa wakati.
Ufanisi wa Taxify unategemea madereva waaminifu ambao wanatakiwa kuunganishwa na huduma hiyo kwa njia ya simu janja zenye mfumo wa uhakika wa intaneti ambao unawezesha kufahamu eneo alipo mteja.
Ili kuharakisha huduma hiyo, Tafixy wamejitolea kuwakopesha simu madereva ambao watalipa kwa awamu kutokana na faida watakayopata kwenye biashara. Lakini madereva hao watalazimika kutoa asilimia 15 ya mapato yanayopatikana katika kila safari ili kuimarisha shughuli za uendeshaji wa huduma hiyo.
Licha ya neema kushuka kwa abiria wanaotumia taski, wale wa Bajaj watalazimika kusubiri kidogo wakati kampuni hiyo ikijipinga kutanua huduma zake katika Jiji hilo.
“Kwa bajaj bado sijasikia ila huku bado ushamba mwingi, inaweza ikasaidia kama wataleta na huku,” amesema Godwin Kweka, dereva wa bajaj jijini Dodoma.
Zinazohusiana:
- Mambo ya kuzingatia unapotumia Uber, Taxify.
- Idris alamba shavu uber.
- Njia za kuepuka foleni kali ya Dar es Salaam kwa kutumia teknlojia.
Taxify inaweza kusaidia kufungua milango ya fursa mbalimbali kutokana na kuamishwa kwa stendi kuu ya mabasi iliyokuwa katikati ya jiji na kupelekwa eneo la Nanenae ambalo liko nje kidogo ya mji.
“Nimewahi kuona tangazo la Taxify ila kama wameanza kutoa huduma itasaidia sana ila sijajua gharama zake zitakuwaje,” amesema Gladness Pesha mkazi wa jijini, Dodoma.
Awali kabla kuzindua rasmi kufanya kazi Dodoma huduma ya Taxify ilikuwa inapatikana zaidi katika jiji la Dar es Salaam na Mwanza ambapo iliingia Tanzania Desemba 8, 2017 kuchuana na kampuni nyingine ya Uber.
“Tunaendelea kupanua wigo wa huduma, na Mji Mkuu wa Dodoma ni mojawapo ya miji ya msingi katika soko letu. Tuna imani ya kwamba watanzania watanufaika na huduma zetu,” amesema Eseka.

Jinsi App ya Taxify inavyoonekana katika simu yako unapofanya huduma ya kuomba kufuatwa ulipo. Picha| Daily News.
Latest