Tanzania ukingoni kumaliza vifo vitokavyo na uzazi
- Serikali yalenga kufikia vifo 70 vya uzazi kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo 2030.
- Wizara ya Afya yaahidi kuifanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa Afrika.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan, amesema kiwango cha vifo vitokanavyo na uzazi nchini kimepungua hadi kufikia 76 kwa kila vizazi hai 100,000, hatua inayoifanya Tanzania kusogea karibu na lengo la Umoja wa Mataifa la kupunguza vifo hivyo hadi 70 ifikapo mwaka 2030.
Mafanikio hayo yanaakisi juhudi za Serikali na watumishi wa sekta ya afya katika kuboresha huduma za uzazi na mtoto, huku vifo vya watoto wachanga vikishuka kutoka 24 hadi 17 na vile vya watoto walio chini ya miaka mitano kutoka 43 hadi 28 kwa kila vizazi hai 1,000.
“Kwa hiyo Tanzania tuko 76, kwa hiyo tuna deni la sita tu. Nina hakika tukifika mwaka 2030 tutakuwa tumefanya vizuri sana,” amesema Rais Samia.
Rais Samia ameyasema hayo leo, Novemba 26, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza katika Mkutano wa Tatu wa Kitaifa wa Kisayansi kuhusu Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto Mchanga, Watoto, Vijana na Lishe, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC).
Mwaka 2023, Tanzania ilitunukiwa tuzo ya kimataifa ya Goalkeepers kutoka taasisi ya Gates Foundation, kufuatia mafanikio ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000, hatua iliyokuwa kielelezo cha jitihada za nchi katika kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto.
Tuzo hiyo iliongeza ari ya wataalamu wa afya kuendelea kufanya kazi kwa bidii, na kufanikiwa kupunguza kiwango hicho hadi kufikia vifo 76.
Awali akizungumza Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa ameeleza kuwa uteuzi wa Rais Samia kuwa Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Mama na Mtoto Februari 2022 ulitokana na kutambua juhudi na hatua zilizopigwa na Tanzania katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vile vya watoto.
Amesema tangu kukabidhiwa jukumu hilo, Rais Samia ameandaa mpango elekezi wa kinara, kuunda sekretarieti ya kuratibu utekelezaji wake na kusimamia mapitio ya sera na mikakati ya afya ya uzazi, mama, mtoto na vijana barani Afrika.
“Ahadi ya sekta ya afya ni kushirikiana na sekretarieti yako ya kinara, Africa CDC na wadau wengine ili Tanzania iwe nchi ya mfano na mahali ambapo Afrika inakuja kujifunza kwa vitendo,” amesema Waziri wa Afya.
Aidha, Rais Samia amesema Serikali inalenga kupunguza vifo vya watoto wachanga hadi 12 na vile vya watoto walio chini ya miaka mitano hadi 25 kwa kila vizazi hai 1,000 ifikapo mwaka 2030.

Katika hatua nyingine, amesema mpango elekezi wa jukumu lake kama Kinara wa Umoja wa Afrika kuhusu Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, uliozinduliwa Novemba 23 mwaka huu, utaimarisha ufuatiliaji, tathmini na uwajibikaji katika utekelezaji wa ajenda hiyo barani Afrika.
Aidha, ameitaka Wizara ya Afya kutambua halmashauri zinazofanya vizuri katika kupunguza vifo vya mama na watoto ili zitunukiwe katika mkutano wa mwaka ujao.
Ametaja Chalinze na baadhi ya maeneo ya Songwe au Mbeya kuwa miongoni mwa maeneo aliyopata taarifa za mafanikio ya kukaa miezi mitatu bila kifo cha mama wakati wa kujifungua wala mtoto.
Tanzania inatekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), yanayolenga kupunguza vifo vya uzazi hadi 70 kwa kila vizazi hai 100,000 na kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto ifikapo mwaka 2030.