Tanzania, Malawi zafungua ukurasa mpya ushirikiano kibiashara

October 7, 2020 12:02 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Tanzania kufungua ofisi ya bandari Malawi kurahisisha shughuli za usafirishaji wa mizigo kupitia bandari za Dar es Salaam na Mtwara.
  • Zitasaini mkataba wa usafiri wa anga kukuza utalii na biashara. 
  • Pia zitajenga kituo cha pamoja cha mpakani kurahisisha usafirishaji wa mizigo na watu.  

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kufungua ofisi katika jiji la Lilongwe nchini Malawi ili kuwarahishia wafanyabiashara usafirishaji wa mizigo kupitia bandari za Mtwara na Dar es Salaam. 

Hatua hiyo itasaidia kuimarisha mahusiano ya kibiashara baina ya nchi hizo mbili yatakayosaidia upatikanaji wa mapato kwa ajili ya utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.

Rais Magufuli aliyekuwa akizungumza leo (Oktoba 7, 2020) Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati wa mapokezi ya Rais wa Malawi, Dk Lazarus Chakwera, amesema anataka kuona mahusiano ya nchi hizo mbili yakijikita zaidi katika masuala ya biashara, hivyo uboresha wa miundombinu ya usafirishaji ni muhimu.  

“Ndani ya mwezi mmoja, Wizara ya Uchukuzi ya Tanzania chini ya Mheshimiwa Kamwelwe (Mhandisi Isack Kamwelwe) kupitia Mamlaka ya Bandari (TPA) wafungue ofisi Lilongwe (Malawi) ili wafanyabiashara wasiangaike kuja Dar es Salaam kufanya mambo yao,” amesema Dk Magufuli.

Amesema ofisi hiyo itarahisisha mchakato wa usafirishaji wa mizigo ya wafanyabiashara wa Malawi wanaotumia bandari ya Dar es Salaam na ile ya Mtwara. 

Amebainisha kuwa ofisi hizo zitafunguliwa ndani ya muda mfupi kwa sababu amezungumza na Rais Chakwera kuharakisha mchakato wake.

Ikiwa ofisi hizo zitafunguliwa zitaongeza kasi ya mizigo ya Malawi inayopita bandari za Mtwara na Dar es Salaam na hivyo kuzifaidisha nchi zote mbili kimapato.  

“Malawi na Tanzania kwa sababu ni ndugu mmoja, Malawi ijihesabu kwamba ina bandari yake ambayo ni Mtwara pamoja na Dar es Salaam.

“Bandari ya Mtwara hivi sasa inafanyiwa ukarabati mkubwa na upanuzi. Ina uwezo wa kubeba tani 400,000. Itakapofika Desemba mwaka huu itakuwa na uwezo wa kubeba tani milioni 1,” amesema Rais Magufuli.


 Soma zaidi:


Ili kuimarisha zaidi mahusiano ya kibiashara na Malawi, Rais amesema watahakikisha miundombinu ya barabara zinazounganisha mpaka wa nchi hizo katika maeneo ya Ileje na Chitepa inajengwa kwa kiwango cha lami.

Hatua hiyo inaweza kuwasaidia wafanyabiashara kusafirisha mizigo kupitia reli ya Tazara hadi mkoani Songwe kabla ya kutumia malori kupeleka Malawi. 

Kwa sasa nchi hizo mbili zinaangalia namna ya kukufua mchakato wa kusaini mkataba kuhusu usafiri wa ndege utakaosaidia kukuza sekta ya anga na utalii ya nchi hizo mbili.  

Naye Rais Chikware amesema yote waliyozungumza na mwenyeji wake atahakikisha yanatekelezwa ili kuharakisha maendeleo ya nchi hizo mbili.

“Mimi na kaka yangu Magufuli tumekuwa na mazungumzo mazuri.  Ni muhimu tusitegemee nchi nyingine tu, kwa sababu Mungu ametupa rasilimali za kutosha kwa ajili ya kuendeleza Mataifa yetu wenyewe,” amesema Rais huyo ambaye yuko nchini kwa ziara ya siku tatu.

Ili kuongeza kasi ya biashara, amesema ni lazima kuwe na kituo cha pamoja cha huduma za mpakani kati ya nchi hizo mbili na kurahisisha usafiri wa watu na mizigo pamoja na huduma.

Hadi kufikia mwaka 2019/20 biashara kati ya Malawi na Tanzania imeongezeka hadi kufikia Dola za Marekani milioni 81 (Sh187.8 bilioni) kutoka dola milioni 60 (Sh139.2 bilioni) mwaka 2015.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW