Tanzania kutafuta mrithi wa Dk Ndugulile WHO
- Ni nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika ambayo mteule wake alikuwa Dk Faustine Ndugulile.
- Alifariki dunia usiku wa kuamkia Novemba 27, 2024 akiwa anapata matibabu nchini India.
- Rais Samia amesema ni dhamira ya Serikali ya kuhakikisha Tanzania inaendelea kuimarisha uwakilishi wake kimataifa
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itatafuta mwakilishi mwingine ili kugombea nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani kanda ya Afrika baada ya mteule wake Dk Faustine Ndugulile kufariki dunia.
Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika na Mbunge wa Kigamboni (CCM), Dk Faustine Ndugulile alifariki dunia usiku wa kuamkia Novemba 27, 2024 akiwa anapata matibabu nchini India.
Rais Samia amesema ni dhamira ya Serikali ya kuhakikisha Tanzania inaendelea kuimarisha uwakilishi wake kimataifa hata baada ya kifo cha Dk Ndugulile.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika shughuli ya kumuaga Dk Ndugulile katika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam amesema Serikali itaweka juhudi kubwa kutafuta Mtanzania mwenye sifa na uwezo wa kushindana katika nafasi iliyoachwa na Ndugulile ili kuendeleza heshima ya nchi.
“Nitumie fursa hii kugusia wajibu wetu kama nchi kuimarisha uwakilishi wa Tanzania ndani ya Afrika na kimataifa…katika safari yake hii ya mwisho ameweka heshima kubwa kwa nchi yetu kwa kupata nafasi ile, niseme kwamba Mungu amechukua amana yake…’”
“…lakini kwetu sisi ni kwenda mbele, tutaingia tena kwenye ushindani wa nafasi ileile. Tutatafuta Mtanzania mwenye sifa zinazoweza kushindana na ulimwengu, tutaingia tena na tutaweka nguvu ileile ili kuweka heshima ya nchi yetu,” amesema Rais Samia.
Serikali itafanya mchakato wa ushindani ili kumpata mwakilishi mwenye sifa zinazohitajika kushindana kimataifa na kuendeleza kazi kubwa aliyoiacha Dk Ndugulile.
“Ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba Watanzania wabobezi tunaweka kila aina ya nguvu ili waweze kutuwakilisha katika fani za kimataifa,” amesema Rais Samia.
Pia amempongoza Dk Ndugulile kwa mchango wake ulioweka heshima kwa nchi na kusisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushiriki kikamilifu katika maamuzi ya kimataifa.
“Dk Faustine katika safari yake hii ya mwisho ameweka heshima kubwa kwa nchi yetu kwa kupata nafasi ile. Mungu amechukua amana yake, lakini kwetu sisi ni kwenda mbele,” aliongeza.
Dk Ndungulile, ambaye ni daktari wa binadamu kitaaluma aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika Agosti 28, 2024.
Uteuzi wake ulitarajiwa kuridhiwa katika kikao cha 156 cha Bodi ya Utendaji wa WHO kitakachofanyika Februari 2025 huko jijini Geneva, Uswizi.
Baadhi ya viongozi waeleza mazuri ya Dk Ndugulile
Shughuli ya kumuaga Dk Ndugulile imehudhuriwa na viongozi mbalimbali, familia, na wananchi waliomkumbuka kama kiongozi aliyejituma na mzalendo aliyejitolea kwa maendeleo ya nchi. Mazishi yake yanatarajiwa kufanyika kesho Kigamboni, Dar es Salaam.
Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Akson amesisitiza kwamba kifo cha Dk Ndugulile kimeacha pengo kubwa, akieleza jinsi Taifa lilivyoendelea kumhitaji kwa michango yake muhimu na kumshukuru Rais Samia kwa juhudi za kuibua na kuendeleza vipaji vya Watanzania.
“Tulikuwa bado tunamuhitaji aendelee kutusaidia katika maeneo mbalimbali. Nitumie nafasi hii kukushukuru Rais Samia kwa namna ambavyo unaitumikia nchi yetu ikiwa ni pamoja na kutusaidia wananchi kuonesha uwezo wetu, ule ambao ulikuwa unazungumzwa hapa, hasa na wageni kutoka nje ambao wamekuja hapa kueleza namna ambavyo walikuwa na matarajio makubwa sana kuhusu utumishi ambao angeenda kuufanya Dk ndugulile,” amesema.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amemtaja Dk Ndugulile kama kiongozi aliyekuwa karibu na wananchi na mwenye kujali mahitaji ya watu wake.
“Ndugu waombolezaji wenzangu niwape pole wote…nimeshuhudia namna ambavyo amekuwa akishughulikia matatizo ya wananchi wa Kigamboni kwa kuitaka na kuishauri Serikali namna bora wa kuwahudumia,” amesema Majaliwa.