Tanzania kushirikiana na Korea kujenga chuo cha anga
- Ni kutokana na kuimarika na kukua kwa sekta ya anga
- Idadi ya abiria yaongezeka kwa asilimia 28 kwa miaka miwili
- Mchango wa sekta katika pato la Taifa wafikia asilimia 2.5 kutoka 0.9.
Dar es Salaam.Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema Serikali yake kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga cha Korea (Korean Aerospace University) inakusudia kujenga chuo cha masuala ya anga nchini Tanzania.
Rais Samia aliyekuwa akihutubia katika hafla ya kutunukiwa Udaktari wa Falsafa wa Heshima (Honoris Causa) katika sekta ya anga na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga nchini humo leo Juni 3, 2024, amesema sekta ya anga ya Tanzania imeendelea kukua ambapo kati ya mwaka 2021 mpaka 2023 idadi ya abiria imeongezeka kwa asilimia 28.
Shahada hiyo imetolewa leo katika hafla maalum iliyoandaliwa na chuo hicho na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Korea na Tanzania ikiwa ni kutambua mchango wake katika mabadiliko ya sera na uongozi wa kimantiki.
“Idadi ya ndege zinazofanya safari za kimataifa zimeongezeka kutoka 26 hadi 33, idadi ya wasafiri wa ndani imeongezeka kwa asilimia 26.5 baada ya Covid-19 kutoka abiria milioni 3 hadi kufikia milioni 3.8 kwa mwaka wa 2023,” amesema Rais Samia jijini Seoul.
Rais Samia ameongeza kuwa Serikali yake itaendelea kuwekeza kimkakati na hasa katika kufufua kampuni ya Air Tanzania Limited (ATCL) na kuendeleza miundombinu, ikiwemo mfumo wa kujenga rada, kukarabati na kupanua viwanja vya ndege kote nchini.
Itakumbukwa kuwa kabla mwaka 2016, ATCL ilikuwa na ndege moja inayofanya kazi ambapo hadi kufikia Machi 2024 zimeongezeka ndege 14 za abiria na moja ya mizigo ambapo ndege 6 kati ya hizo zimenunuliwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Kwa mujibu wa Rais Samia kufufuliwa kwa shirika hilo kumeleta manufaa mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa mapato kutoka Sh 23 bilioni mwaka 2016/17 hadi Sh380.4 bilioni mwaka 2022/23 jambo lililoongeza mchango wa sekta ya anga kwenye pato la Taifa kutoka asilimia 0.9 mwaka 2018 hadi asilimia 2.5 mwaka 2023.