Tanzania kujenga makumbusho ya marais ya Sh34 bilioni

September 30, 2024 6:38 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ujenzi wa makumbusho hayo yatakayojengwa mkoani Dodoma upo katika hatua za awali. 
  • Hadi sasa Serikali imeshatoa Sh1 bilioni na zaidi kwa ajili ya hatua za awali za ujenzi.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imetenga Sh34 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa mradi mkubwa wa makumbusho ya marais unaolenga kuhifadhi kumbukumbu za viongozi wakuu wa nchi pamoja na historia ya taifa.

Mradi huo uliopo katika hatua za awali, kwa mujibu wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, utajengwa katika eneo la Mtumba jijini Dodoma. 

Rais Samia amewaeleza wahudhuriaji wa hafla ya uzinduzi wa kitabu cha Edward Moringe Sokoine Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania leo Septemba 30, 2024 jijini Dar es Salaam kuwa ni muhimu kuweka kumbukumbu za viongozi wa nchi ili kizazi kijacho kijifunze kutokana na historia yao na maono waliyoacha.

Hayati Sokoine ni miongoni mwa viongozi wa Tanzania anayekumbukwa kwa uzalendo, utendaji kazi unaohimiza ufanisi, aliyekemea rushwa na uhujumu uchumi na mtu aliyependa kukuza uchumi kupitia kilimo. 

Hayati Sokoine alihudumu kama Waziri Mkuu kwa vipindi viwili. Awali aliongoza kuanzia Februari 13, 1977 hadi Novemba 7,1980, na baadaye kuanzia Februari 24,1983 hadi kifo chake Aprili 12,1984, baada ya kupata ajali ya gari huko Dakawa mkoani Morogoro.

Makumbusho ya Marais yanatarajiwa kuwa mradi muhimu katika kuhifadhi urithi wa viongozi wa Tanzania na kuongeza ufahamu wa umma juu ya historia ya taifa na michango ya viongozi katika kulijenga Taifa.

Viongozi mbalimbali pamoja na Wananchi waliohudhuria hafla ya Uzinduzi wa Kitabu cha Hayati Edward Moringe Sokoine kinachohusu Maisha na Uongozi. Picha/Ikulu Mawasiliano.

“Tumetenga Sh34 bilioni kwa ajili ya mradi huo na tumeanza mwaka huu kutenga bajeti ndogo kama Sh1 bilioni na kitu na eneo lile lina ukubwa wa hekari 50 pale Dodoma kwa hiyo hili tunalifanyia kazi,” amesema Rais Samia. 

Taarifa hiyo imekuja baada ya balozi Joseph Sokoine, mtoto wa Hayati Edward Sokoine, kuomba uwepo wa kituo maalumu cha kuhifadhi historia ya viongozi. 

Katika hotuba yake, Rais Samia amesema Sokoine alisisitiza matumizi ya kilimo cha kisasa kwa kushirikisha wataalamu wenye ujuzi wa kisasa.

“Leo hii SUA (Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine) inaendelea kuishi maono ya Sokoine ya kuzalisha wataalamu wengi wanaoendeleza sekta ya kilimo na mifugo,” ameeleza Rais Samia.

Awali makamu wa Rais Dk Philipo Mipango wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho alimuomba Rais Samia kuwawezesha viongozi waliopo hai ili waweze kuandika tawasifu zao kabla ya kufa.

Katika uzinduzi huo uliohusisha viongozi mbalimbali wa sasa na wa zamani, Waziri Mkuu mstaafu Jaji Sinde Warioba ameeleza kuwa baadhi ya watu walipotosha kuwa kifo cha Sokoine kilikuwa ni faida kwa Rais wa kwanza wa Tanzania Julius Nyerere, jambo ambalo si kweli. 

Kifo cha Sokoine ni miongoni mwa masuala yaliyoibua hisia kali wakati huo huku baadhi wakihusisha ajali hiyo na jaribio la kusitisha jitihada zake za kuwadhibiti wala rushwa. 

Mtoto wa hayati Sokoine, balozi Joseph Sokoine amemshukuru Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango kwa kutoa wazo la uandishi wa kitabu cha Maisha na Uongozi wa Hayati Edward Sokoine. 

Enable Notifications OK No thanks