Tanzania kuiuzia Malawi tani 7,000 za mbaazi ghafi
- Hatua hiyo inakuja baada ya Malawi kuwa na uhitaji wa zao hilo.
- Tayari mchakato wa oda iliyotolewa na Malawi umeanza kufanyiwa kazi.
- Lakini Serikali imesema inaendelea na jitihada za kujenga viwanda vya kuchakata zao hilo nchini.
Dar es salaam. Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya amesema Tanzania inakusudia kuuza tani 7,000 za mbaazi ghafi kwa nchi ya Malawi, ikiwa ni mkakati wa muda mfupi wa kutafuta masoko mbadala kimataifa.
Mhandisi Manyanya ameeleza azma hiyo ya Serikali bungeni jana (Mei 31, 2019) wakati akijibu swali la Mbunge wa Nachingwea, Hassan Masala ambaye alitaka kufahamu mikakati ya Serikali katika kuwakwamua wakulima wa mbaazi ikizingatiwa kuwa soko la zao hilo limekuwa likisuasua.
Akijibu swali hilo, Manyanya amesema Malawi imeonyesha dhamira ya kununua mbaazi ya Tanzania, baada ya Serikali kuzitembelea baadhi ya nchi za Afrika ikiwemo Malawi na Burundi ili kutafuta soko la zao hilo.
“Mkakati wa muda mfupi ni kutafuta masoko mbadala nchi za nje ambapo mbaazi ghafi zitauzwa. Jitihada hizo zimeanza kuzaa matunda kuanzia Machi 2019, kufuatia jitihada ya Serikali ya kutafuta mazao ya kilimo ikiwemo mbaazi katika nchi za jirani za Malawi, Burundi, Congo DRC na Zambia.
Zinahusiana:Kampuni yafungua mlango kununua chumvi ya wakulima Tanzania.
“Katika ziara hiyo nchi ya Malawi kwa mwaka huu imeonyesha uhitaji wa tani 7,000 na taratibu za kuhakikisha oda hiyo inatekelezwa zinaendelea,” amesema Mhandisi Manyanya.
Akizungumzia mkakati wa muda mrefu, amesema wanaendelea kuhamasisha jitihada za uwekezaji wa viwanda vya kukoboa na kuongeza thamani ya mazao ya mbaazi na mazao mengine ya jamii ya mikunde hapa nchini.
Amebainisha kuwa kampuni ya Mahashree Agro Processing Ltd kutoka nchini India inajenga kiwanda mkoani Morogoro ambapo hadi kufikia Juni mwaka huu, kiwanda hicho kinategemewa kuanza kazi huku kikiwa na uwezo wa kuchakata na kusindika tani 700,000 kwa mwaka.
Amesema viwanda vingine viwili vimeshaanza kufanya kazi vya Power Quality Exporters Limited kilichopo Dar es salaam na kiwanda cha Samson Agro Export limited.
Muonekano wa mbaazi baada ya kumenywa. Picha | Mtandao
Latest