Tanzania itakavyofaidika ziara ya Rais Samia nchini Ufaransa, Ubelgiji

February 9, 2022 1:47 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Itaimarisha uhusiano wa kimataifa.
  • Inaweza kupata fursa za kiuchumi na uwekezaji.

Dar es Salaam. Huenda Tanzania ikaendelea kufaidika na diplomasia ya kimataifa hasa katika sekta ya uchumi, baada ya Rais Samia Suluhu kuzulu mataifa mawili ya Umoja wa Ulaya (EU) wiki hii.

Rais Samia anatarajia kuondoka nchini kuelekea Ufaransa na baadaye Ubelgiji kwa ajili ya ziara ya kikazi katika nchi hizo.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano-Ikulu, Zuhura Yunus iliyotolewa leoFebruari 9, 2022 imesema akiwa nchini Ufaransa, Rais Samia atashuhudia utiaji saini mikataba baina ya Serikali ya Tanzania na Ufaransa katika sekta za miradi ya maendeleo, ushirikiano katika masuala ya uchumi wa bluu, usalama wa bahari, sekta ya usafiri na maendeleo endelevu.

Pamoja na masuala mengine, Rais Samia pia anatarajiwa kuzungumza na Watanzania waishio nchini Ufaransa kuhusu mambo mbalimbali ikiwemo umuhimu wa kuwekeza nyumbani.

Aidha, Rais Samia anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi na Serikali utakaojadili kuhusu rasilimali bahari duniani (One Ocean Summit).

Ukiwa umeitishwa na rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, kama kielelezo cha urais wa Ufaransa wa miezi sita wa EU, mkutano huo wa kilele wa siku tatu pia utazingatia juhudi za kuboresha utawala wa bahari kuu na kuratibu utafiti wa kisayansi wa kimataifa.

Balozi wa Ufaransa wa ncha za kaskazini na kusini na maswala ya baharini, Poivre d’Arvor amesema kuwa bahari inashughulikia zaidi ya asilimia 70 ya uso wa dunia, ni mdhibiti muhimu wa hali ya hewa, tajiri wa rasilimali, ufunguo wa biashara na kiungo muhimu kati ya mataifa.


Soma zaidi: 


Mkutano huo ambao umefunguliwa leo katika bandari ya Brest nchini Ufaransa pia utayaleta pamoja makampuni makubwa ya meli kama Maersk, CMA CGM na Hapag-Lloyd, ambayo yanachukua karibu asilimia 55 ya mizigo ya baharini duniani, pamoja na wanasayansi wakuu, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO), watunga sera na mashirika ya kimataifa.

Siku mbili za kwanza za mkutano huo zitakuwa za warsha na vikao 30 vya umma juu ya mada mbalimbali ikiwemo sayansi ya baharini, Mediterania, meli endelevu, bandari za kijani, na miji iliyo katika hatari ya kuongezeka kwa viwango vya bahari, zitakazowaleta pamoja watafiti 300, wajasiriamali na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa yakiwemo ya Umoja wa Mataifa (UN).

Mkutano huo wa ngazi ya juu utakaofanyika Ijumaa asubuhi utahusisha wakuu wa nchi na serikali kutoka mabara yote matano akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan.

Baada ya kukamilisha ziara nchini Ufaransa, Rais ataelekea Ubelgiji kwa ziara ya kiserikali.

Nchi hizo mbili zimekuwa na uhusiano wa karibu na Tanzania kwa muda mrefu katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu na maji ambapo Tanzania imekuwa ikipata mikopo na misaada kuimarisha huduma za kijamii kwa ajili ya maendeleo ya raia wake.

Enable Notifications OK No thanks