Tahariri: Kila la kheri kidato cha sita Tanzania, ‘vita’ imeanza
- Watahiniwa hao wameanza mitihani leo na watamaliza Julai 16, 2020.
- Watakiwa kufanya vizuri kupata fursa ya kuingia vyuo vikuu.
Wanafunzi wa kidato cha sita leo Juni 29, 2020 wanaanza mitihani ya Taifa kuhitimu ngazi hiyo ya elimu. Mitihani hiyo inatarajiwa kumalizika Julai 16 mwaka huu ni hitimisho la safari ya miaka sita ya elimu ya sekondari na kujiweka tayari kwa elimu ya juu ya vyuo na vyuo vikuu.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) Dk Charles Msonde katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, amesema maandalizi kwa ajili mitihani hiyo ikiwemo vijitabu vya kujibia, mitihani yenyewe na nyaraka zote zimesambazwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Mtihani huo utafanyika katika shule 763 na vituo vya watahiniwa wa kujitegemea 239. Watahiniwa 85,546 wamesajiliwa kufanya mtihani huo, kati yao 74,805 ni watahiniwa wa shule na waliobaki ni watahiniwa wa kujitegemea.
Dk Msonde amesema kati ya watahiniwa hao wa shule waliosajiliwa kufanya mtihani huo, wanawake ni 32,521 sawa na asilimia 43.47 ya watahiniwa wote. Necta imeonya kuwa haitasita kumchukulia hatua za kisheria mtu yeyote atakayehusika na udanganyifu wa mtihani na kuwataka wasimamizi na wanafunzi kuzingatia sheria na kanuni za mitihani.
Sisi Nukta (www.nukta.co.tz) tunawatakia kila la heri watahiniwa wote wafanye mtihani huo kwa mafanikio makubwa ili kutimiza ndoto zao za kwenda katika ngazi ya juu ya elimu ya vyuo na vyuo vikuu.
Jambo la msingi tunalotaka kuwakumbusha ni kwamba hakuna mafanikio yanayokuja kirahisi. Mitihani wanayofanya ni moja ya safari zao za mafanikio, kwa kifupi leo wameingia vitani kusaka elimu zaidi katika maisha yao.
Muhimu wanatakiwa kufanya mitihani hiyo kwa kujiamini na kuepuka vitendo vyovyote vya udanganyifu vitakavyosababishwa kufutwa kwa matokeo yao.
Mwanafunzi anayejiamini ni yule aliyejiandaa vizuri kabla ya mitihani na kuzingatia yote aliyofundishwa darasani ili kupata fursa ya kujibu kwa ufasaha maswali yote yaliyopo kwenye mitihani hiyo.
Katika kipindi hiki cha mitihani, wanafunzi wanashauriwa kupata muda mzuri wa kupumzika na kufanya mapitio ya waliyosoma muda wa miaka miwili kabla ya kuingia katika chumba cha mitihani.
Kuwahi katika chumba cha mitihani, kusoma na kujibu kwa ufasaha maswali ni hatua nyingine ya kufanya vizuri na kufaulu.
Mbali na kujiandaa kimasomo, tunawasihi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona kwa kuwa bado upo nchini. Wasisahau kunawa mara kwa mara na maji tiririka na sabuni na kujiepusha na mazingira yatakayofanya wapate corona kirahisi.
Wakati huu pia wazazi wanapaswa kuwatia moyo watoto wao ambao wanafanya mitihani kuwa watashinda na kuhakikisha wanakuwa salama kiafya na kiakili wakati wote wa mitihani.
Tunawatakiwa kila heri watahiniwa wote na tunaamini watafanya vizuri katika mitihani hiyo ikizingatiwa kuwa walimu walitimiza wajibu wao wa kufundisha na kuwaandaa kisaikolojia kukamilisha masomo kwa wakati.
Latest
