Tabia zinazoangamiza vijana mahali pa kazi – 2

December 5, 2019 7:38 am · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Miongoni mwa tabia hizo ni kujikweza, kutumia muda vibaya na utovu wa nidhamu unaoharibu sifa za maisha yaotabia hizi
  • Vijana wanaotaka kukua kitaaluma kibiashara wanapaswa kuziepuka

Jana tuliangazia sehemu ya kwanza ya tabia zinazokwamisha vijana kutimiza ndoto zao katika maeneo ya kazi au biashara zikiwemo za uvivu, ufitini na kukata tamaa mapema.

Leo tunaendelea na sehemu ya mwisho ya makala haya ambayo itagusia athari za vijana kujikweza katika nafasi zao.

1. Kujimwambafai

Katika maisha ya kawaida ya kazi au biashara kuna tabia ya baadhi ya vijana waliofanikiwa kujitukuza au kutaka kuonyesha umwamba kwamba wao ni wao. Kwa kuazima maneno ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete tunasema wana tabia ya “kujimwambafai”. Kwa kuwa ni mabosi au viongozi wanataka wakikohoa tu kila mtu awaogope.

Aina hii ya uhusiano inaua ndoto za vijana wengi hasa pale kwa bahati mbaya wanapoporomoka kutoka kwenye nyazifa zao au hali bora ya kifedha na kufulia.

Kujimwambafai kunaua vipaji na kunatengeneza uhusiano mbaya na wafanyakazi au wafanyabiashara wenzio. Hautakufa ukiwa mtu wa kawaida mwenye staha hata kama una madaraka au fedha za kuibeba dunia.


2. Kupoteza muda

Kuchati kwenye mitandao ya kijamii kama makundi ya Whatsapp au kupiga umbea wakati wa kazi ni moja ya masuala ambayo kwa sasa yanawapotezea muda vijana. Tabia hii imekuwa ikiwafanya washindwe kutimiza malengo yao ya kikazi au kibiashara na kuhatarisha vibarua au biashara zao.  

Baadhi ambao hujiona ni smati sana hujaribu kufanya vitu vingi kwa wakati mmoja bila mpango kamili wa kumaliza kazi husika jambo linalowafanya wachelewe kufanya shughuli zao za kipaumbele.

Wapo baadhi ambao hufanya kazi huku wakisikiliza muziki YouTube kama sehemu ya kiburudisho lakini uzoefu wangu unaonyesha kuwa tabia hiyo inapoteza sana muda. Kuna wakati utatakiwa kurudi YouTube na kutafuta muziki mwingine unaoupenda. Kitendo cha kwenda na kurudi kwenye mtandao huo kunafanya mtu apoteze dakika nyingi tu ambazo zingetumika kufanya na kumaliza kwa wakati.


Soma zaidi: 


Ili uweze kukua kikazi au kitaaluma unatakiwa uwe mtunzaji mzuri wa muda. Jiwekee ratiba imara isioterereka isipokuwa tu nyakati za dharura. ishi ratiba hiyo na wafanye rafiki na wafanyakazi wenzio waiheshimu.

Usiruhusu mtu akupotezee muda wako. Achana na wezi wa muda maarufu kwa kimombo ‘time stealers’ ambao kazi yao ni kuwapumzikia wenzao pale wanapokuwa hawana kazi ya kufanya.


3. Utovu wa nidhamu

Kuna baadhi ya watu wanahusianisha ujana na utovu wa nidhamu. Baadhi ya vijana wanaonekana wa hovyo kwa sababu ya kukosa nidhamu. Kutokana na nafasi zetu kikazi au kibiashara tumejikuta tukikosa heshima kwa wafanyakazi, wateja au washirika wetu wa biashara. Utovu wa nidhamu huzaa kiburi na chuki. Hufanya watu wakudharau na kukuona wa kawaida sana.

Kijana smati ni yule mwenye nidhamu ya kazi na maisha yake. Nidhamu hufanya kijana makini kuheshimu na kuheshimu wengine bila kujali uwezo au hali zao za kielimu. Kwa kifupi mtu wa namna hii huwa ni “konki wa mafanikio”. Vijana wengi waliofanikiwa wakiwemo mabilionea kama Mark Zukerberg wa Facebook huwezi kukuta wakiwa na skendo nyingi za utovu wa nidhamu ukiachana na changamoto za kampuni wanazoziongoza.

Nidhamu ya kazi ni msingi wa mafanikio kwa kila kijana. Utovu wa nidhamu huua mustakabari wa vijana wengi ulimwenguni. Picha|Tran Mau Tri Tam/Unsplash.​​​​​​​

4. Kutozingatia misingi ya kitaaluma

Kutokana mambo kuwa mengi katika kipindi ambacho muda ni mchache baadhi ya vijana wamejikuta wakiruka misingi ya taaluma zao na kuchulia kazi au biashara zao kama masuala ya kawaida. Tabia hizi za kukiuka miiko ya kitaaluma inafanya vijana waonekane watu wa hovyo wasiotakiwa kupatiwa madaraka.

Jaribu kumfikiria daktari kijana wa kiume ambaye kazi yake ni kutongoza tu mabinti wagonjwa kila wanapomuona. Daktari wa namna hii ni rahisi sana kuharibu mustakabari wa taaluma na maisha yake iwapo ataripotiwa na wagonjwa kwa uongozi au hata kushtakiwa kabisa mahakamani kwa masuala ya rushwa ya ngono.

Tabia kama hizo za rushwa katika kazi zinafanya vijana waharibu kazi na sifa ya taasisi wanazofanyia kazi. Hautakufa kama utafuata misingi na taratibu za kazi au biashara yako kwa kuingiza fedha halali na kupunguza tamaa.

Japo zipi tabia nyingi zinazokwamisha vijana, ila hizi ni baadhi tu ya zinazofanya ndoto zao zikwame kabisa. Semina za mara kwa mara na uimarishaji wa mfumo wa elimu za vyuo vikuu katika kutokomeza tabia kama hizi unaweza kuwasaidia vijana kuwa bora zaidi mahali pa kazi au katika kuendesha biashara zao.

Kwa maoni au ushauri tuma kwenda maoni@nukta.co.tz au Whatsapp 0677 088088.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV