Simulizi ya Deogratius Ndejembi: Kada wa CCM aliyepaa kiuongozi
- Anasubiri hatua muhimu ya kikatiba ya kupitishwa na Bunge ili ashike nafasi hiyo ya juu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Dar es Salaam. Â Deogratius Ndejembi, sasa anaingia kwenye orodha ya Watanzania wachache walioshika nafasi za juu za uongozi nchini baada ya kupendekezwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania.Â
Uamuzi wa kumpendekeza Ndejembi unakuja baada ya Dk Emmanuel Nchimbi kujiuzulu umakamu wa rais ikiwa ni siku 295 tu tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo Novemba mwaka jana.Â
Katika taarifa yake kwa umma ya kustaafu siasa na utumishi wa umma, Dk Nchimbi alieleza kuwa angeng’atuka madarakani Septemba 4, 2026. Hata hivyo, CCM kimemfuta uanachama kabla siku yake ya mwisho ofisini kutokana na utovu wa nidhamu na maadili.Â
Hata wakati Dk Nchimbi akipatiwa mkono wa ‘byebye’, Watanzania watakuwa wanajiuliza, Ndejembi ni nani hasa anayeenda kurithi mikoba ya kada huyo mwandamizi?Â

Huyu ni kijana wa CCM aliyekulia ndani ya chama hicho tawala ambacho kimekuwepo madarakani tangu nchi ipate uhuru takriban miaka 65 iliyopita.
Mzaliwa wa mkoa wa Dodoma, katikati mwa nchi, alianza safari ya uongozi wa kisiasa mwaka 2008 baada ya kuwa mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) akitokea katika ngazi ya wilaya.Â
Pamoja na kuwa UVCCM, Ndejembi alipata fursa ya kuwa mjumbe wa halmashauri kuu ya taifa NEC (Nationa Executive Council) ya CCM kati ya mwaka 2012 hadi 2017, kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa katika tovuti ya Bunge.Â
Kipindi hicho akijihusisha na shughuli za chama, Ndejembi pia alikuwa akifanya kazi katika kampuni mbalimbali za sekta binafsi zikiwamo A1 Outdoor, Smile Communication, Tigo sasa Yas na GSM Group, hatua hiyo ilimpa uzoefu katika usimamizi, mauzo na masoko kabla ya kuingia rasmi katika uongozi Serikalini.Â
Kada huyo aliyezaliwa Julai 12, 1983, alisoma Shule ya Msingi ya Cannon Andrea kati ya mwaka 1988 hadi 1995 kabla ya kujiunga mwaka mmoja baadaye katika shule ya sekondari ya Jamhuri ama Kigurunyembe na kuhitimu mwaka 1998.Â
Ndejembi mwenye Shahada ya Uhusiano wa Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Lincoln nchini Uingereza kabla ya kuwa Mbunge wa Chamwino mwaka 2020, aliteuliwa na hayati Rais Dk John Pombe Magufuli kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Dodoma mwaka 2016.
Mwanasiasa huyo mtiifu (Loyalist) wa CCM, anasubiri hatua muhimu ya kikatiba ya kupitishwa na Bunge ili ashike nafasi hiyo ya juu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan. Katika Bunge hilo linalotarajia kumpigia kura, asilimia 97 ni wabunge wa chama tawala, jambo linalomtengezea njia nyeupe kufikia cheo hicho.Â
Endapo atapitishwa na Bunge, Ndejembi atakua Makamu wa Rais wa tatu ndani ya kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na atakua makamu wa Rais wa 13 tangu Tanzania kupata uhuru wake.
Kabla ya kupendekezwa kuwa Makamu wa Rais, Ndejembi alikuwa ni Waziri wa Nishati, nafasi aliyoishika tangu mwishoni Novemba 17 mwaka jana baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 uliotawaliwa na vurugu zilizotokana na maandamano.Â
Tayari Ndejembi alikuwa na uzoefu katika Baraza la Mawaziri kwa kuwa kabla ya hapo aliwahi kuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, akihudumu kwa muda wa miaka miwili, na mnamo mwaka 2023 alihamia Ofisi ya Rais, TAMISEMI.Â
Kwa sehemu kubwa Ndejembi amepanda vyeo haraka haraka wakati wa uongozi wa Rais Samia.Â

Mwaka 2024 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, na punde tu Rais Samia akamteua kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Ndejembi ni miongoni mwa vigogo wa Serikali waliokosolewa vikali mapema Aprili mwaka huu baada ya bei ya mafuta kupanda katika kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa nchini kutokana na vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.Â
Wakosoaji hao wakiwemo watumiaji wa mtandao na viongozi wa vyama vya upinzani nchini, walimtuhumu kushindwa kusimamia ipasavyo sekta hiyo hitajika katika ukuaji wa uchumi.
Katika wadhifa wake huo mpya, huenda akakabiliwa na kibarua cha kumsaidia kikamilifu bosi wake Rais Samia katika kipindi ambacho kumekuwa na presha za kukuza uchumi ikiwemo kutengeneza ajira, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kudhibiti mfumuko wa bei.Â
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba, Ndejembi ni rahimu na mchapakazi na kwamba Rais Samia alikuwa na jicho la mwewe kumteua kiongozi huyo kuwa Makamu wa Rais.