Siasa ni makundi, ndiyo moyo wa mchezo wenyewe

April 9, 2025 6:29 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link

Siasa ni makundi ni magenge. Bila makundi, hakuna siasa. Bila tofauti za mitazamo, maslahi na matamanio, hakuna hoja, hakuna ushindani wa fikra, na hatimaye hakuna uhai wa kisiasa.

Vyama vya siasa si taasisi tupu ni majukwaa ya kuwakutanisha makundi ya watu wenye misimamo, mitazamo, na masilahi tofauti, lakini wenye lengo la pamoja: kusukuma mbele maono ya taifa kwa namna wanavyoamini ni bora zaidi. Afya, uimara na uhai wa chama hupimwa kwa namna kinavyoweza kuyatunza, kuyasimamia na kuyaendesha makundi haya kwa busara.

Makundi haya si ya kubuniwa tu; yanatokana na uhalisia wa kijamii. Yanawakilisha matabaka, maeneo, vipato, imani, na hata historia za watu. Kuyapuuza ni sawa na kuipuuzia jamii yenyewe. Kuyakandamiza ni sawa na kujaribu kunyamazisha sauti halali za wananchi. 

Kiongozi anapowabeza, kuwatukana au kuwavunjia heshima wale wanaounda makundi haya ndani ya chama, anakuwa hafanyi siasa bali anachochea mafarakano. Anapokemea tofauti badala ya kuziunganisha, anaharibu msingi wa chama chake. 

Uimara wa chama haupatikani kwa sauti kubwa au ushindi wa muda mfupi, bali kwa uwezo wa kuongoza makundi yenye misimamo tofauti kuelekea mwelekeo mmoja. Huu ndio mtihani wa kweli wa uongozi.

Kiongozi bora ni mzalendo wa ndani ya chama—anayejua kuwa kila kundi lina nafasi, lina mchango, na lina watu wanaolitegemea. Kuunganisha simba na panya, mamba na jogoo, ni sanaa ya siasa. Ukishindwa ndani ya chama, huwezi kabisa kushughulikia tofauti za kitaifa.

Kiongozi anapokemea tofauti badala ya kuziunganisha, anaharibu msingi wa chama chake. Picha hii si halisi imetengenezwa na akili unde (AI) kunogesha Muktadha.

Nchi yetu ina makundi mengi kila moja likiwa na sauti yake. Kuna wanaotafuta fursa, wanaoogopa kubaki nyuma, wanaoamini katika mabadiliko, na wanaolilia utulivu. Vyama vyote duniani vina magenge ya aina zote:  

Wapo mercenaries (watu wa kukodiwa ) wa siasa, waliolipwa kutetea au kushambulia, wapo wenye kiu ya madaraka wanaoamini ni zamu yao kuongoza, wapo wacha Mungu wa itikadi wanaoamini katika maadili na misingi ya chama kwa dhati.  

Hawa wote ni sehemu ya damu ya chama. Ukikataa kundi lolote, unajidhoofisha mwenyewe.

Wakati wa uchaguzi, si kila mpiga kura atapima hoja zako kwa weledi wa kitaaluma. Wapo wasomi, wapo wanaharakati, wapo mama lishe, wapo vijana wa bodaboda, wapo waumini wa ushabiki, na wapo pia “makenge” na “mamende” wote hawa ni binadamu, ni raia, ni wapiga kura. Na wote wana sauti.

Kiongozi mahiri anajua jinsi ya kuzungumza na kila kundi, kulielewa, na kulivuta kuelekea malengo ya pamoja. Siasa si ya watu “smart” peke yao. Kama unataka siasa ya watu waliopitia mjadala wa kitaaluma pekee, basi rudi ukafundishe chuoni. Uwanja wa siasa ni wa wote.

Siasa ni ushawishi, si hoja tu.  Ni mtandao, si kujitenga.  Ni uwezo wa kuunganisha tofauti, si kupigania usawa usiowezekana.   Ni sanaa ya kuongoza magenge mbalimbali kuelekea mwelekeo mmoja.

Mshindi wa kweli si yule aliyepigiwa kura nyingi pekee, bali ni yule aliyeweza kuyafanya makundi yote yajione kuwa ni washiriki wa ushindi huo.

Haya ni maoni binafsi na si msimamo wa taasisi, imeandikwa na Mike Mushi, Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks