Serikali yatoa maagizo mazito chama cha ushirika Jeshi la Polisi
- Chatakiwa kuongeza uwekezaji ili kupata fedha nyingi.
Mwanza. Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Jumanne Sagini amekiagiza chama cha ushirika wa akiba na mikopo cha Jeshi la Polisi Tanzania (Ura Saccos) kujikita kwenye uwekezaji ili kutunusha mfuko wao na si kutegemea mikopo na riba pekee.
Sagini akizungumza kwenye mkutano wa 14 wa chama hicho uliofanyika jijini Mwanza Oktoba 28, 2022, Waziri huyo amewataka kutumia mtaji uliopo kuanzisha fursa za kibiashara zitakazosaidia kukuza mfuko wao.
“Niwashauri muangalie fursa ambayo italipa na inakubalika kwenye katiba na sheria zenu. Mfano kufungua mgahawa kwa ajili ya chakula kama ipo kwenye sheria mnaweza kufungua na sisi tukawa wadau wenu na kikawaida hakuna biashara ya chakula isiyolipa,” amesema Waziri Sagini.
Naibu Waziri huyo amepongeza chama hicho kwa kupunguza riba kutoka asilimia 10 hadi kufikia asilimia 7.5 hali inayosaidia wanachama kujitokeza kukopa kwa wingi.
“Kupunguza kwa kiwango hicho cha riba kinatoa mwanya kwa wanachama kukopa mikopo yenye riba nafuu ambayo haitamletea mtu shida ya kuuziwa mali na vitu vyake.
“Pia hilo ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan ambaye aliagiza taasisi zote za kifedha kupunguza riba ili kutoa fursa kwa wananchi kukopa mikopo yenye riba nafuu,” amesema Sagini.
Zinazohusina:
- Kiswahili ndiyo mpango mzima kusaka wateja Tanzania: Ripoti
- Sababu zilizofanya Tanzania iporomoke viwango vya ufanyaji biashara duniani
Awali, Kaimu Mrajisi wa Ura Saccos, Josephat Kisamalala amesema toka chama hicho kilipoanzishwa mwaka 2006, kimefanikiwa kusajili zaidi ya wanachama 41, 000 na kwamba katika kipindi cha miaka 16 iliyopita zaidi ya mikopo yenye thamani ya Sh394.5 bilioni imeshatolewa.
“Tunajivunia kuwa na saccos inayoboresha maisha ya Watanzania lakini pia kupitia ukaguzi mkuu wa hesabu za Serikali, Ura imekuwa ni saoccos pekee ambayo ilitunukiwa hati safi na kutunukiwa cheti cha ubora,” amesema Kisamalala
Mwenyekiti wa Ura Saccos, Benedict Wakulyamba amesema hadi kufikia Septemba mwaka huu zaidi ya asilimia 90 ya watumishi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani wamejiunga na chama hicho.
Amesema Ura imekuwa nguzo imara kuhakikisha watumishi wa polisi na familia zao wanatumia vyema vipato vyao kuboresha ustawi wa maisha kiuchumi na kijamii kwa kutoa huduma zenye gharama nafuu.
“Chama hiki kimekuwa msaada kwa askari kuwa na utulivu wa kimawazo kwa askari kuwezesha kutekeleza majukumu yao bila kuwa na msongo wa mawazo kutokana na ugumu wa maisha,” amesema Wakulyamba.
Latest
