Serikali yajipanga kukabiliana na mvua za El Niño
- Ni baada ya ya TMA kutangaza ujio wa mvua kubwa za El Niño kuanzia Septemba hadi Januari, 2027.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali imeanza kujipanga kukabiliana na mvua za El Niño zinazotarajia kuanza mwezi ujao katika mikoa mbalimbali nchini.
Nchemba aliyekuwa akizungumza wakati wa maswali na majibu bungeni Dodoma leo Agosti 27, 2026 amesema mbali na kutoa tahadhari Serikali imejipanga kurekebisha miundombinu ili kupunguza athari ya mvua hizo.
”Serikali imejipanga vyema kwa kuhakikisha maeneo yanayoweza kuwa na athari za mvua nyingi kuandaa au kutengenezea mifereji ili maji yaweze kwenda kwenye njia zake ili kuondoa uwezekano wa maji kulundikana;” amesema Nchemba akijibu swali na Mbunge wa jimbo la Bukoba mjini, Jonston Mtasingwa (CCM).
Kauli hiyo ya Nchemba imekuja ikiwa ni takribani siku 11 tangu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Ladislaus Chang’a, atoe tahadhari ya uwepo wa hali hiyo mbaya ya hewa itakayoambatana na mvua kubwa.
Chang’a, alisema kuwa ongezeko la mvua linatarajiwa zaidi Novemba 2026, huku mvua ambazo kwa kawaida huisha Desemba zikitarajiwa kuendelea hadi Januari 2027.

Mvua za juu ya wastani hadi wastani zinatarajiwa hususani katika mikoa nane pamoja na maeneo ya Kanda ya Ziwa Victoria kwa mujibu wa TMA. Picha/BBC Swahili.
“Mvua hizo zinaweza kusababisha mafuriko, unyevu kupita kiasi kwenye udongo, uharibifu wa mazao na miundombinu, pamoja na kuongezeka kwa magonjwa ya mazao na milipuko kutokana na uchafuzi wa maji,” ilionya TMA.
Sambamba na onyo hilo, jana Agosti 26,2026, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde aliwasihi wananchi kuweka akiba ya chakula walichovuna sasa ili kujihami na changamoto za kiuzalishaji zinazoweza kusababishwa na mvua hizo.
Aidha Nchemba amewarai Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya mvua hizo akiwataka kufanya tathmini ya maeneo wanayoishi ikiwa yanaweza kuathirika na mvua hizo.
“ Naomba kuchukua nafasi hii kutoa rai kwa watanzania wote kuwa na tahadhari na jambo hili tayari tumekwisha tahadharishwa ni wajibu wa kila mtanzania pia kufanya tathmini ya aina hiyo pale anapoishi kwa kuangalia mazingira ya mahali na hali hii ambayo tumetahadharishwa,” ameongeza Nchemba.