Serikali yajipanga kudhibiti maandamano Desemba 9
- Yaagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha kuwa ukamataji wa watuhumiwa unafanyika kwa kufuata misingi ya sheria na kwa kuzingatia staha.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema imejipanga kudhibiti maandamano yaliyotangazwa kufanyika Desemba 9, 2025 kwa kuwa hayajakidhi matakwa ya kisheria na yanaashiria mipango hatarishi kwa usalama wa Taifa.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Desemba 8, 2025, Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene amesema mpaka sasa hakuna mtu yeyote aliyepeleka maombi ya kufanyika kwa maandamano kwenye mamkala husika kama sheria za nchi zinavyotaka na hivyo maandamano yanayopangwa kufanyika Desemba 9 si halali na hayatambuliki.
Aidha, Simbachawene ametoa wito kwa wananchi kutoshiriki kwa namna yeyote kwenye maandamano hayo akisisitiza kutojiunga na watu watakaojaribu kuandamana au kufanya uchochezi kwenye mitandao ya kijamii.
“Maandamano hayo ni haramu, hayaruhusiwi…maandamano tunayoyafahamu sisi ni yale yanayoombwa na mtu mahususi, na yanakuwa na ujumbe mahususi na yanasema shabaha yake ni nini, lakini yanaeleza yatafanyika wapi, yatatoka wapi hadi wapi’” amefafanua Simbachawene
Simbachawe amewahakishia wananchi kuwa vyombo vya ulinzi vimejipanga vyema katika kuhakikisha wanadhibiti maandamano hayo akitoa wito kwa wananchi kushirikiana na vyombo hivyo kutoa taarifa kwa vitendo vyovyote vinavyoashiria uvunjifu wa amani.
Katika hatua nyingine amemwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillus Wambura, kuhakikisha kuwa ukamataji wa watuhumiwa unafanyika kwa kufuata misingi ya sheria na kwa kuzingatia staha akifafanua kuwa aina ya ukamataji unaofanywa na baadhi ya askari ikiwemo kuvaa kininja, kutovaa sare rasmi za polisi na kwenda kuwakamata watuhumiwa majumbani usiku haukubaliki na unapaswa kusitishwa.
Ameongeza kuwa Jeshi la Polisi linapaswa kuzingatia uwiano kati ya ukubwa wa kosa na hatua zinazochukuliwa ili kuepusha matukio yanayoweza kuwatia hofu wananchi.
“Ukamataji ninaoupenda mimi ni ule wa kisheria. Askari anaenda, anaripoti kwa mjumbe, mtu anajulikana yupo kazini kwake. Ya nini uende kumkamata nyumbani kwake umevaa kininja? Tumekubaliana kwamba kuwe na ukamataji wenye staha,” amesema Simbachawene.
Marufuku iliyotolewa na Simbachawene kuhusu maandamano yanayopangwa kufanywa Disemba 9, 2025 ni muendelezo wa marufuku zinazoendelea kutolewa na vyombo mbalimbali vya usalama ikiwemo viongozi wa Serikali.
Itakumbukwa kuwa Disemba 5, 2025, Jeshi la Polisi pia lilitangaza kupiga marufuku maandamano hayo ambayo ni kwa muda sasa yamekuwa yakipigiwa chapuo na wanaharakati kwenye mitandao ya kijamii, likibainisha kuwa hayajakidhi matakwa ya kisheria na yanavishiria vya uvunjifu wa amani.
Maandamano yanayopigiwa chapuo kufanyika Disemba 9 ni maandamano ya pili kuitishwa mwaka huu baada ya yale ya Oktoba 29 kuacha alama katika maisha ya Watanzania yakisababisha uharibifu wa miundombinu, mali na vifo vya watu ambao mpaka sasa Serikali haijabainisha rasmi idadi kamili.
Latest